• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:50 AM
Raila akemea Chebukati

Raila akemea Chebukati

NA CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa Azimio la Umoja-One Kenya Raila Odinga amekana madai ya aliyekuwa mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Wafula Chebukati kwamba wafuasi wa mrengo huo walijaribu kumhonga abatilishe hesabu za kura za urais mwaka 2022.

Akiongea Jumapili, Januari 29, 2023 katika uwanja wa Jacaranda, Nairobi Bw Odinga alidai Bw Chebukati na waliokuwa makamishna Abdi Guliye na Boya Molu pia walimtembelea nyumbani kwake.

Waziri Mkuu huyo wa zamani alitisha “kumwanika” Bw Chebukati kwa kutoa picha za kumwonyesha akiwa kwake (Raila) kabla ya kutangaza matokeo ya uchaguzi wa urais Agosti 15, 2022.

“Chebukati alidai eti watu wetu walitaka kumhonga pamoja na Guliye na Molu. Nataka kuwauliza kwa nini walikuja nyumbani kwangu?” Bw Odinga akauliza.

“Nini walikopa kutoka kwangu? Wanafaa kujua kwamba nina picha zao, na wakinichezea, nitatoa picha hizo,” akaeleza alipohutubia maelfu ya wafuasi wake.

Bw Odinga alikuwa akijibu madai ya Bw Chebukati kwamba aliyekuwa Katibu Mkuu wa Jubilee Raphael Tuju alijaribu kumhonga ili abadilishe matokeo ya uchaguzi na kumtangaza kiongozi huyo wa Azimio.

Bw Chebukati alitoa madai hayo juzi alikuwa akihojiwa na wakili wa Kamishna wa IEBC aliyesimamisha kazi Irene Masit, Donald Kipkorir anayechunguzwa na jopokazi.

Jopokazi hilo linaloongozwa na Jaji wa Mahakama ya Rufaa Aggrey Muchelule, linamchunguza Bi Masit kwa madai kuwa alikiuka sheria kwa kupinga matokeo ya urais yaliyotangazwa na Bw Chebukati Agosti 15, 2022.

Bi Masit anadaiwa kutenda kosa hilo akiwa pamoja na makamishna wenzake waliojiuzulu Juliana Cherera, Justus Nyang’aya na Francis Wanderi.

  • Tags

You can share this post!

Ruto kufungua semina ya Bunge la Kitaifa na Muungano wa CPA...

Rais Ruto kuzuru Pwani tena siasa ikizidi kurindima

T L