• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 12:42 PM
Raila amtemea Ruto moto kuhusu kura

Raila amtemea Ruto moto kuhusu kura

NA BENSON MATHEKA

KIONGOZI wa Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga anaonekana kufaulu kumwekea mtego Rais William Ruto kupitia maagizo anayowapa wafuasi wake kwenye mikutano anayoandaa huku akiendelea kutoa madai kwamba alishinda uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022.

Rais Ruto amelazimika kujibu madai hayo akisema nia ya Bw Odinga ni kushinikiza handisheki ili apate mgao wa serikali, madai ambayo waziri huyo mkuu wa zamani amekanusha.

Wachanganuzi wa siasa wanasema kwamba lengo la Bw Odinga kutoa ripoti aliyohusisha na mfanyakazi wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) na kukataa kumtambua Dkt Ruto kama rais, ni mtego ambao viongozi wa serikali ya Kenya Kwanza wanaonekana kuingia.

Kufikia Jumapili, maafisa wa IEBC na viongozi wa Kenya Kwanza hawakuwa wamesema chochote kuhusu ripoti hiyo inayoonyesha kwamba huenda Bw Odinga alishinda uchaguzi wa urais.

Kimya chao kinaweza kufasiriwa na wananchi kama ishara ya kushtuliwa na ufichuzi huo wala hawana uhakika kuhusu mbinu ya kuchukua ili kuupinga bila kumfanya Odinga kumwaga mtama zaidi.

Hata hivyo, mkurugenzi wa uchunguzi wa uhalifu (DCI) Bw Mohamed Amin aliyeingia ofisini baada ya Rais Ruto kumfuta kazi Bw George Kinoti, ameanzisha uchunguzi unaolenga kubaini uhalali wa ripoti hiyo ambao unaweza kumlazimisha kumuita Bw Odinga na viongozi wengine wa Azimio ili kuandikisha taarifa.

Hatua hiyo inaonekana kumpa nguvu Bw Odinga ambaye jana Jumapili, alipuuza hatua ya Bw Amin ambaye kulingana naye, anafanyia kazi serikali ya Kenya Kwanza aliyoapa hataitambua.

Hii imemfanya Bw Odinga kuibua madai mapya kwamba aliyekuwa mwenyekiti wa IEBC, Bw Wafula Chebukati na waliokuwa makamishna Boya Molu na Profesa Abdi Guliye walienda kwake kabla ya kutangaza matokeo ya kura ya urais.

Bw Raila aliutaka Umoja wa Mataifa kutuma wachunguzi kubaini ukweli wa mambo kuhusu uchaguzi huo wa Agosti 9.

“Tunataka Umoja wa Mataifa kutuma wakaguzi huru nchini, na hii inafaa kufanyika ndani ya wiki mbili na iwapo Ruto hatakubali hilo kufanyika Wakenya watachukua hatua wanayotakja,” Bw Odinga alisema.

Kiongozi huyo wa ODM alisema kuwa Azimio inaamini kwamba Kenya Kwanza ilihonga Bw Chebukati na mrengo wake katika IEBC ili kuiba kura zake.

“Mimi nina video ya Chebukati na wenzake Boya Molu na Abdi Guliye katika nyumba yangu kabla ya kutangaza matokeo. Wakicheza, nitaitoa ili waseme walitaka nini kwangu,” alisema Bw Odinga.

Katika mkutano wa jana uwanjani Jacarada, Nairobi, Bw Odinga alionekana kukaza mtego kwa Rais Ruto kwa kumwambia athubutu kumchukulia hatua alivyoashiria.

Wiki jana, Rais Ruto alimwambia Bw Odinga kuwa anafaa kumzoea kama rais wa tano wa Kenya na kuacha kusema hamtambui kama rais.

“Ninataka kumwambia Ruto, wewe hutujui, hutujui, uliza ‘Nyayo’, nguvu za wananchi ni sauti ya Mungu,” alisema kauli inayoonekana kumthubutu Rais Ruto kuzuia mikutano yake ambayo amepanga katika uwanja wa Kamukunji mtaani Kibra, Machakos, Nakuru, Kisumu, Turkana, Garisa na Kisii miongoni mwa maeneo mengine kabla ya kuanza alichoashiria kuwa maandamano barabarani ambapo huenda makabiliano yakazuka.

“Sifanyi haya kwa sababu ya Raila Odinga, ni kwa sababu yenu vijana, akina mama na wazee wa nchi hii ambao wanaumizwa na gharama ya maisha inayozidi kuongezeka kutokana na ushuru wa kiholela wa bidhaa. Tunataka vijana wakae imara na kujitokeza kwa mapambano,” alisema.

Alidai kuwa Kenya Kwanza imepokonya Bunge jukumu la kusimamia mashirika ya serikali ili ipate kuyapora na kuyauza.

Kauli hii na ile ya wafuasi wake kususia ushuru inaonekana kuwachochea ili wakaidi serikali kupitia maandamano yanayoweza kuvuruga ajenda za serikali.

Katika tamko lingine linaloashiria mtego fiche aliowekea serikali ya Kenya Kwanza, Bw Odinga alisema “ mabalozi wa kigeni waliniambia yanayofanyika Kenya hayangevumiliwa kama yangefanyika katika nchi zao”.

Aidha, alidai kuwa Bw Chebukati, jaji Aggrey Muchelule anayesimamia kamati ya kuwachunguza ‘Cherera 4’, na spika wa Bunge, Bw Moses Wetang’ula wana uhusiano wa kiukoo.

  • Tags

You can share this post!

Brighton wang’oa mabingwa watetezi Liverpool katika...

Raila: DCI haiwezi kufanya uchunguzi huru kwa sababu Amin...

T L