• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 8:55 PM
Brighton wang’oa mabingwa watetezi Liverpool katika raundi ya nne ya Kombe la FA

Brighton wang’oa mabingwa watetezi Liverpool katika raundi ya nne ya Kombe la FA

Na MASHIRIKA

SAFARI ya Liverpool kutetea ubingwa wa Kombe la FA msimu huu ilifikia mwisho baada ya Brighton kuwadengua katika raundi ya nne kwa kichapo cha 2-1 ugani Amex.

Ingawa Liverpool walitangulia kuona lango la wenyeji wao kupitia kwa Harvey Elliot katika dakika ya 30, Brighton walisawazishiwa na Lewis Dunk kunako dakika ya 39 kabla ya Kaoru Mitoma kufunga goli la ushindi sekunde chache kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa mechi kupulizwa.

Ushindi huo uliendeleza ubabe wa Brighton dhidi ya Liverpool waliokubali tena kichapo cha 3-0 katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ugani Amex wiki mbili zilizopita.

Licha ya kuagana na idadi kubwa ya wanasoka wa haiba kubwa muhula huu, Brighton bado wanatamba chini ya mkufunzi Roberto de Zerbi. Kikosi hicho kilichoagana majuzi na fowadi Leandro Trossard aliyeyoyomea Arsenal, pia kiliacha nje kiungo Moises Caicedo anayewaniwa na Arsenal pamoja na Chelsea.

Brighton walifuzu kwa raundi ya nne ya Kombe la FA muhula huu baada ya kuponda Middlesbrough 5-1 katika raundi ya tatu huku Liverpool wakitandika Wolves 1-0 kwenye marudiano ugani Molineux baada ya sare ya 2-2 uwanjani Anfield.

Japo Brighton waling’olewa na Spurs kwenye raundi ya nne ya Kombe la FA msimu jana, ushindi dhidi ya Liverpool unaweka hai matumaini yao ya kutinga robo-fainali za kivumbi hicho mara sita katika misimu sita. Man-City waliwabandua nje ya kipute hicho kwenye nusu-fainali mnamo 2018-19.

Liverpool sasa hawajapita raundi ya nne ya Kombe la FA katika makala manne yaliyopita ya kipute hicho ambayo wamenogesha wakiwa mabingwa watetezi.

Licha ya kupepeta Brighton 6-1 katika Kombe la FA mnamo 2011-12, Liverpool wameshinda mechi tano pekee za ugenini katika mashindano yote ya msimu huu na waliaga Kombe la FA katika raundi ya nne kwa mara nyingine mnamo 2016-17, 2017-18 na 2020-21.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Jinsi Manchester City walivyodengua Arsenal katika kipute...

Raila amtemea Ruto moto kuhusu kura

T L