• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
Raila apanga mikakati ya kujizolea kura nyingi kaunti 7 ngome ya Ruto

Raila apanga mikakati ya kujizolea kura nyingi kaunti 7 ngome ya Ruto

NA ERIC MATARA

MGOMBEA urais wa muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya ameweka mikakati ya kuyeyusha umaarufu wa Naibu Rais William Ruto katika angalau kaunti saba za Rift Valley.

Kaunti hizo ni pamoja na; Nakuru, Narok, Samburu, Trans Nzoia, Kajiado, Turkana na Laikipia zenye angalau wapiga kura milioni tatu.

Duru katika kambi za Dkt Ruto na Bw Odinga zinasema kuwa wapanga mikakati katika kambi hizo mbili wanapanga kuhakikisha kuwa vinara hao wamezoa kura nyingi katika kaunti hizo.

Kama ishara ya kushindania kura hizo, wawaniaji urais hao wawili wamezidisha kampeni zao katika kaunti hizo.

Kwa mfano, katika wikiendi iliyopita Bw Odinga alikita kambi katika kaunti ya Narok, ili kuimarisha uungwaji mkono katika eneo hilo.

Alitumia suala la uhifadhi wa msitu wa Mau ili kuvutia jamii ya Wamaasai ambayo inathamini msitu huo kwa sababu ni chemichemi kubwa ya maji.

Mnamo Jumapili Bw Odinga alikariri kuwa anaunga mkono mpango wa Waziri wa Mazingira Keriako Tobiko wa kuhifadhi msitu huo.

“Nilipigania uhifadhi wa Msitu wa Mau mnamo 2009 na wakatisha kutonipigia kura. Lakini niliwaambia kwamba hata kama natalazimika kurejea Kibera kuuza mandazi, nilikuwa nimejitolea kufanya hivyo mradi tufaulu kuhifadhi Msitu wa Mau.

“Wale wengine hawawezi kutunza misitu yenu. Hao watu hawawezi kuaminika katika masuala ya uhifadhi wa mazingira,” Bw Odinga akaonya.

Akiongea katika maeneo la Loita, Entasekera na katika uwanja wa michezo wa William Ole Ntimama Bw Odinga alikariri kuwa serikali yake itayapa kipaumbele masuala ya uhifadhi wa mazingira.

Bw Odinga alidai kuwa waliofurushwa kutoka msitu wa Mau wanasubiri kwa hamu Dkt Ruto achaguliwe kuwa rais kisha warejee katika msitu wa Mau.

Ili kuimarisha uungwaji mkono katika kaunti za Narok, Samburu, Laikipia na Kajiado, Bw Odinga amekuwa akijinadi kama mwenye suluhu ya kudumu kwa changamoto za kihistoria za ardhi zinazoikumba jamii ya Maa kwa ujumla.

Kiongozi huyo wa ODM anatumia wandani wake kama vile Waziri Tobiko, Gavana wa Kajiado Joseph Ole Lenku, gavana wa kwanza wa kaunti hiyo David Nkedianye, Seneta wa Narok Ledama Ole Kina, Mbunge wa Narok Kaskazini Moitalel Ole Kenta, aliyekuwa Spika wa Bunge la Kitaifa Francis Ole Kaparo, Mbunge wa Kajiado ya Kati Elija Memusi miongoni mwa wengine.

Bw Kaparo anashirikiana na Gavana wa Laikipia Ndiritu Muriithi kuvumisha Bw Odinga katika kaunti hizo.

Wikiendi ijayo kikosi cha Kenya Kwanza kikiongozwa na Dkt Ruto kitatua katika kaunti ya Narok kujipigia debe.

Duru ziliambia Taifa Leo kwamba mirengo hiyo miwili inaendesha kampeni kali za kujijengea ushawishi katika kaunti zingine za Rift Valley kando za zile za jamii ya Maa.

  • Tags

You can share this post!

Kwekwe kuendelea kumpigia debe Boga

Viongozi wa Kenya Kwanza waahidi kuondoa mashine za kuvuna...

T L