• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 8:50 AM
Viongozi wa Kenya Kwanza waahidi kuondoa mashine za kuvuna majanichai

Viongozi wa Kenya Kwanza waahidi kuondoa mashine za kuvuna majanichai

NA KENYA NEWS AGENCY

VIONGOZI mbalimbali wa muungano wa Kenya Kwanza wakiongozwa na mwaniaji mwenza wa William Ruto, Rigathi Gachagua wametoa wito kwa kampuni za chai Kaunti za Kericho na Bomet kuondoa mashine za kuvuna majanichai na kurejesha maelfu ya vibarua waliopoteza kazi kutokana na uzinduzi wa mashine hizo.

Viongozi hao sasa wanadai kuwa wataondoa mashine hizo na kuwarejesha kazini wafanyakazi hao endapo watachaguliwa.

Bw Gachagua akiandamana na maseneta Aaron Cheruiyot (Kericho) na Moses Wetangula (Bungoma), walisema kuwa maelfu ya wakazi wa maeneo hayo hawana kazi jambo linalowafanya baadhi yao kuishi kwa ufukara.

Kadhalika, mwaniaji wa kiti cha ugavana kupitia tikiti ya UDA, Eric Mutai, aliwahakikishia wakazi wa Kaunti ya Kericho kuwa serikali yake itahakikisha kuwa waliopoteza kazi yao kutokana na uzinduzi wa mashine hizo watapata kazi.

Wakazi wa maeneo hayo wamekuwa wakilalamika kuwa tangu mashine hizo kuzinduliwa, wanalipwa kati ya Sh2 na Sh4 kila kilo, jambo linalofanya baadhi yao kushindwa kuwalipia wana wao karo na kujikimu.

Mashine moja inachukua nafasi ya wafanyakazi zaidi ya 600 na inatumia lita moja ya petroli kuvuna zaidi ya hekari tatu kwa siku.

Kwa upande wake, William Sossion, alilalamika kuwa uzinduzi wa masomo ya CBC umevuruga masomo ya kawaida nchini na kusema kuwa mfumo huo wa elimu unanuia kufaidi wachache.

“Tukipata ushindi katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9, tutahakikisha kuwa sekta ya elimu imeboreshwa,” akasema Bw Sossion.

Viongozi hao pia walitoa wito kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini (IEBC) na Waziri wa teknolojia (ICT), Ubunifu na Masuala ya Vijana, Joe Mucheru, kuhakikisha kuwa mitambo yote yanafanya wakati wa uchaguzi.

“Serikali inafaa ihakikishe kuwa kuna usalama kabla, wakati na hata baada ya uchaguzi. Kadhalika, serikali ihakikishe kuwa mitambo yanafanya kazi kisawa sawa ili kusiwe na masuala ya uwizi,” akasema Bw Sossion.

Viongozi wengine waliohudhuria hafla hiyo ya maombi ni Gavana wa Kericho, Profesa Paul Chepkwony, Gavana wa Bomet, Hillary Barchok, aliyekuwa Gavana wa Bomet, Isaac Ruto, mwaniaji wa kiti cha uwakilishi wa jinsia ya kike Beatrice Kemei, Mbunge wa Ainamoi Benjamin Langat, Mbunge wa Emurua Dikir Johana Ngeno, Mbunge wa Belgut, Nelson Koech almaarufu Sonko, Mbunge maalum wa Soin-Sigowet na Jaji Kemei miongoni mwa wengine.

  • Tags

You can share this post!

Raila apanga mikakati ya kujizolea kura nyingi kaunti 7...

Aliyeiba kipakatalishi kanisani atupwa jela miaka mitatu...

T L