• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 5:50 AM
Raila apinga sera za serikali ya Ruto

Raila apinga sera za serikali ya Ruto

NA CHARLES WASONGA

RAIS William Ruto na kiongozi wa Azimio Raila Odinga wamekuwa wakitofautiana hadharani kuhusiana na masuala mbalimbali katika kile kinachooneka kutoa mwelekeo kuhusu mkondo wa siasa nchini katika muhula wa kwanza wa utawala Kenya Kwanza (KKA).

Bw Odinga ameendeleza kasi ya kupinga sera, maongozi na maamuzi ya serikali ambayo kwa mtazamo wake yanalenga kuwaumiza wananchi wa kawaida mbali na kuendeleza ukiukaji wa katiba na utawala mbaya.

Waziri huyo mkuu wa zamani amepinga mtindo wa serikali wa kukabiliana na changamoto kama vile gharama ya maisha, mauaji ya kiholela yanayotekelezwa na polisi, mageuzi katika idara ya mahakama, utozaji ushuru wa juu, mageuzi katika uwekaji akiba ya uzeeni, na kuondolewa kwa marufuku dhidi ya vyakula vilivyozalishwa kisayansi (GMO).

Amekuwa akisisitiza kuwa serikali ya Kenya Kwanza inarejesha nchi katika enzi za utawala wa kidkteta wa Kanu ambapo uhuru na haki za raia zilikandamizwa huku Rais Ruto akisema anataka kuleta uhuru nchini.

Majuzi, wawili hao walikinzana vikali kuhusiana na uchunguzi unaoendelea kuhusu mauaji ya kiholela ambayo yamekuwa yakitekelezwa na polisi.

Rais Ruto alisema serikali haitahusisha mashirika ya kigeni katika uchunguzi wa visa hivyo vya mauaji tata, anavyopendekeza Bw Odinga.

“Hatuhitaji ushauri kutoka kwa shirika la Scotland Yard kuondoa au kuvunjilia mbali vikosi vinavyohusika na mauaji katika huduma ya kitaifa ya polisi. Tunachohitaji kufanya ni kuheshimu katiba yetu,” Rais Ruto akasema Alhamisi katika majengo ya Mahakama ya Upeo, wakati wa uzinduzi wa ripoti kuhusu hali ya Idara ya Mahakama 2021/2022.

Akiongea Jumatano katika hoteli ya Serena, Nairobi, Bw Odinga pia alipendekeza kuwa serikali ipanue uchunguzi wa mauaji ya kiholela kujumuisha mauaji yaliyotekelezwa katika muhula wa kwanza wa utawala wa Jubilee.

“Uchunguzi unaondeshwa na serikali wakati huu hauongozwi na nia njema. Tunapinga mauaji ya kiholela. Visa vinapasa kuchunguzwa na mashirika ya kigeni kama vile Scotland Yard waliochunguza mauaji ya Ouko (aliyekuwa Waziri wa Kigeni Robert Ouko),” Odinga akasema.

Akaongeza: “Uchunguzi huo pia upanuliwe kujumuisha mauaji ya mashahidi wa kesi za ICC, afisa wa IEBC Chris Msando na wengine waliouawa kinyama.”

Wiki mbili zilizopita Rais Ruto aliamuru kuvunjiliwa mbali kwa kikosi maalum katika Idara ya Upelelezi wa Uhalifu (SSU) kwa tuhuma kuwa baadhi ya wanachama wake walihusika katika utekaji nyara na kutoweka kwa raia wawili wa Kihindi, Mohamed Zaid na Zilfiqar Khan waliowasili nchini kusaidia Dkt Ruto katika kampeni.

Bw Odinga pia ametofautiana na Rais Ruto kuhusiana na mpango wa serikali ya KKA kupanua mawanda ya ushuru na kuongeza viwango vya ushuru ili serikali ipate fedha za kufadhili shughuli zake, pasi kutegemea mikopo.

Aidha, kiongozi huyo wa Azimio amepinga pendekezo la Rais kwamba kiwango cha mchango kwa Hazina ya Kitaifa ya Malipo ya Uzeeni (NSSF) kiongezwe kutoka Sh200 kwa mwezi hadi Sh2,000.

“Ni kinyume cha Katiba kwa serikali kuwaongezea Wakenya mzigo wakati huu ambapo wanazongwa na makali ya njaa na kupanda kwa gharama ya maisha,” Bw Odinga akasema alipohudhuria hafla ya mazishi katika eneo bunge la Seme, kaunti ya Kisumu.

Rais Ruto amesema kuna mpango wa serikali yake kuongeza mapato ya ushuru kutoka Sh2 trilioni wakati huu hadi Sh3 trilioni ifikapo Juni 30, 2023, na Sh6 trilioni kufikia 2027.

Aidha, kiongozi huyo wa Azimio amepinga pendekezo la Rais kwamba kiwango cha mchango kwa Hazina ya Kitaifa ya Malipo ya Uzeeni (NSSF) iongezwe kutoka Sh200 kwa mwezi hadi Sh2,000.

Bw Odinga anapendekeza mageuzi katika Idara ya Mahakama ili iweze kutoa maamuzi ya haki.

“Mahakama imegeuka kuwa asasi ambayo haizingatii haki katika maamuzi yake. Kwa hivyo, sisi kama Wakenya tuko na uwezo wa kuifanyia mageuzi,” akasema akirejelea uamuzi wa Mahakama ya Upeo uliodumishwa ushindi wa Rais Ruto.

Lakini kwa upande wake, Rais Ruto amekariri kujitolea kwa Serikali yake kuiongezea Sh3 bilioni katika mgao wa bajeti “ili iweze kuharakisha kusikilizwa na kuamuliwa kwa kesi za ufisadi.”

Bw Odinga amemlaumu Dkt Ruto kwa kile anadai ni kuwachezea shere Wakenya kwa kutopunguza gharama ya maisha kwa kupunguza bei ya unga kutoka Sh230 hadi Sh70 kwa paketi moja ya kilo mbili alivyoahidi wakati wa kampeni.

Aidha, amepinga uamuzi wa serikali wa kuondoa marufuku dhidi ya ukuzaji, uagizaji na uuzaji vyakula vilivyozalishwa kisayansi (GMOs) akisema ni hatari kwa afya ya Wakenya.

“Ruto aliahidi kupunguza bei ya unga hadi Sh70 lakini hajafanya hivyo mpaka sasa, zaidi ya siku 40 baada ya kuingia mamlakani. Amekuwa akikwepa suala hilo kila mara ilhali Wakenya wanaendelea kuumia kwa kulala njaa,” Bw Odinga akasema mwezi Oktoba, alipofanya ziara ya kukutana na wafuasi katika mtaa wa Mathare, Nairobi.

Lakini Bw Ruto alijibu kwa kukariri kuwa serikali yake imeweka mpango wa kupunguza gharama ya maisha kwa kupunguza gharama ya uzalishaji chakula kwa kupunguza bei ya mbolea hadi Sh3,500 kutoka Sh6,000 kwa gunia la kilo 50.

  • Tags

You can share this post!

PAUKWA: Bobu amtoa kijasho Harara baraza la wazee

Shujaa yatiwa kundi la kifo Dubai Sevens

T L