• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 9:50 AM
Raila ashikwa mateka

Raila ashikwa mateka

Na JUSTUS OCHIENG

Mgombea urais wa Azimio la Umoja One Kenya, Bw Raila Odinga anakabiliwa na wakati mgumu kuwaridhisha washirika wake katika muungano huo miezi minne kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

Viongozi wa vyama tanzu katika muungano huo wanaendelea kupigania ubabe katika ngome zao na kumfanya Bw Odinga kuwa ‘mateka’ wao.

Haya yanajiri hata kabla ya uamuzi kuafikiwa kuhusiana na jinsi muungano huo utakavyosimamisha wagombeaji mbalimbali huku vyama tanzu vikikataa maeneo kutengewa vyama vikubwa – Jubilee, ODM na Wiper.

Vyama vidogo katika muungano huo vinahisi kwamba vitafungiwa nje katika baadhi ya maeneo iwapo yatatengewa vyama vikubwa.

Hii inamaanisha kuwa vyama hivyo vikubwa vinavyoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta, Bw Odinga na Kalonzo Musyoka mtawalia vinakabiliwa na kivumbi kutoka kwa vyama vidogo katika uchaguzi mkuu ujao.

Bw Odinga anaonekana kung’ang’ana kuridhisha zaidi ya vyama 20 vinavyomuunga mkono lakini maslahi ya kila kimoja yanatishia kuvuruga muungano huo huku baadhi vikimlaumu kwa kutokuwa mwaminifu.

Kulingana na wachanganuzi wa siasa, kinachomtatiza zaidi Bw Odinga ni kumdumisha Bw Musyoka katika muungano huo pamoja na magavana watatu wa kaunti za Ukambani ambao kila mmoja ana chama chake– Charity Ngilu (Narc), Dkt Alfred Mutua (Maendeleo Chap Chap) na Prof Kivutha Kibwana (Muungano Party), ambao wamepeleka vita vya ubabe wa eneo lao katika Azimio.

Dkt Mutua wiki jana alielezea nia ya kushirikiana na mpinzani mkuu wa Bw Odinga- Naibu Rais William Ruto.

Hata hivyo, jana alisisitiza uaminifu wake kwa Bw Odinga baada ya kukutana na Baraza la Kitaifa la chama chake (NGC), lakini akataka kuwa mgombea-mwenza wa Bw Odinga, hali inayoweza kumkasirisha Bw Musyoka ambaye pia anamezea mate wadhifa huo.

Jana, chama cha Democratic Action Party – Kenya (DAP-K) kinachohusishwa na Waziri wa Ulinzi, Bw Eugene Wamalwa, kilitoa matakwa mapya katika muungano huo.

Naibu kiongozi wa DAP-K Ayub Savula alisema Bw Wamalwa anafaa kuwa mwanachama wa Baraza la Azimio linaloongozwa na Rais Kenyatta. Baraza hilo limetwikwa jukumu la kufanya maamuzi ya mwisho kuhusu muungano huo.

“Tunataka mkataba ambao Bw Musyoka na vyama tanzu vilitia saini katika KICC utolewe ili tuuchunguze,” Bw Savula alisema na kuongeza kuwa mgombea-mwenza wa Bw Odinga anafaa kuchaguliwa kwa njia ya uwazi kwa kupigiwa kura na wajumbe wa Azimio.

Wiki jana, Bw Odinga alikubali matakwa ya vyama vinane vilivyoungana chini ya vuguvugu la “Mwanzo Mpya” na kupanua Baraza la Azimio kuwa na wanachama 11, hali ambayo washirika wa Bw Musyoka walisema haikumfurahisha makamu rais huyo wa zamani.

Vyama hivyo vilikuwa Maendeleo Chap Chap cha Dkt Mutua’s MCC, Narc cha Bi Ngilu, Muungano cha Kibwana, Kenya Reform Party, Chama Cha Uzalendo, DAP-K, People’s Trust Party na Maendeleo Democratic Party.

Taifa Leo imebaini kuwa tayari Bi Ngilu ameshirikishwa katika baraza hilo ili kuhakikisha jinsia mbili zimewakilishwa.Mchanganuzi wa siasa Prof Gitile Naituli wa Chuo Kikuu cha Multi Media anasema presha ambayo Bw Odinga anapitia ni sawa na vitisho kwa kuwa baadhi ya viongozi wa vyama wamejaribu kujiunga na mpinzani wake Dkt Ruto akikosa kutimiza matakwa yao.

Alisema ni mapema mno kumkosoa Bw Odinga kwa kutokuwa mwaminifu.“Nafikiri Raila anayopitia ni vitisho vya kumsukuma akubali matakwa ya wanachama,” alisema Prof Naituli.

Mdadisi wa siasa Herman Manyora anasema kwamba huenda Bw Odinga presha nyingi kuliko zinazoshuhudiwa.

  • Tags

You can share this post!

Rivatex yataka wakuzaji waboreshe kilimo cha pamba

Migawanyiko DP Muturi akijiunga na Ruto

T L