• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 8:50 AM
Migawanyiko DP Muturi akijiunga na Ruto

Migawanyiko DP Muturi akijiunga na Ruto

DAVID MUCHUI

MIGAWANYIKO imeibuka ndani ya chama cha Democratic Party (DP), baada ya baadhi ya wanachama, kupinga hatua ya Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi, kujiunga na muungano wa Kenya Kwanza unaoongozwa na Naibu Rais William Ruto.

Naibu mwenyekiti wa kitaifa wa chama hicho, Bw Peter Ndubai aliambia Taifa Leo kwamba walishangazwa na hatua hiyo kwa sababu hawakuwa na habari zozote.

Wanachama wengine watatu wa DP pia wameandika barua kwa afisi ya Msajili Mkuu wa Vyama vya Kisiasa wakilalamika kuwa hatua hiyo haikuidhinishwa na Kongamano la Kitaifa la Wajumbe (NDC).

“Tunaomba afisi yake ikatae stak – abadhi ya makubaliano inayodai kuwa chama chetu cha DP kimejiunga na muungano wa Kenya Kwanza,” maafisa wa chama hicho walisema katika barua hiyo. Bw Ndubai alisema alipata habari za Bw Muturi kujiunga na Kenya Kwanza mnamo Jumamosi asubuhi akilaumu maafisa wa – chache kwa kupanga njama hiyo.

“Hatua hiyo imewashangaza wawaniaji wengi kote nchini ambao hawafahamu lolote kuhusu makubaliano ambayo yalitiwa saini na Kenya Kwanza kwa niaba ya DP.

Wameingiwa na wasiwasi kwamba hatua huenda ikachangia kutengwa kwao wakati wa uteuzi. NDC ilisema wazi kuwa mwaniaji wetu wa urais angeendelea mpaka debeni na kujiunga na muungano baada ya uchaguzi mkuu,” Bw Ndabai akasema.

Alisema kwa kuunda muungano baada ya uchaguzi mkuu, chama cha DP kingepata nafasi ya kujiimarisha kitaifa kwa kuwasilisha mgombea wa urais. Bw Ndubai ambaye anawania kiti cha ubunge cha Tigania Magharibi dhidi ya Mbunge wa sasa John Mutunga wa chama cha United Democratic

Alliance (UDA), alisema amejipata katika njia panda. Hata hivyo, alisema watakumbatia uamuzi huo ikiwa mkataba wa muungano utawafaa wagombeaji wanaowania kwa tikiti ya DP.

“Tutatoa maelezo ya kina baada ya kujua yaliyomo katika mkataba huo kwa sababu wakati huu tumeingiwa na wasiwasi mwingi. Wengi wetu hatukufahamu kwamba tulikuwa tunajiunga katika muungano,” akasema.

Spika wa Bunge la Kaunti ya Meru, Joseph Kaberia, ambaye anawania useneta kwa chama cha DP, alisema wanasubiri taarifa rasmi kutoka chama hicho kuhusu hatima ya wawaniaji ambao watakabiliana na wengine wa UDA.

“Nitatoa kauli kamili kuhusu hatua baada ya kupata maelezo ya kina kuhusu mkataba huo wa makubaliano,” Bw Kiberia akasema.

Katika barua ambayo Taifa Leo iliona, wanachama hao watatu wa DP, Wambugu Nyamu, Daniel Mumene na Kingori Choto, wanamtaka Msajili wa Vyama vya Kisiasa, Bi Anne Nderitu, kukataa stakabadhi ya muungano kati ya DP na Kenya Kwanza.

“Kufuatia makubaliano ya wajumbe katika NDC kwamba hatutabuni muungano kabla ya uchaguzi, tunashangazwa na tangazo la kiongozi wetu wa chama kwamba kimejiunga na Kenya Kwanza. Hii ni kinyume na msimamo wa wanachama uliowasilishwa katika mapendekezo ya NDC,” wakasema.

Lakini baada ya kutia saini mkataba huo wa muungano, Bw Muturi alisema hatua hiyo ilipata idhini kutoka kwa wanachama wa DP walimhimiza kushauriana na vyama vyenye maono sawa.

  • Tags

You can share this post!

Raila ashikwa mateka

Jubilee njiapanda maelewano kati ya wawaniaji yakifeli

T L