• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 7:12 PM
Raila ataja mbinu mpya za kukabili serikali ya Ruto

Raila ataja mbinu mpya za kukabili serikali ya Ruto

NA JUSTUS OCHIENG

KIONGOZI wa Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga, jana Jumapili alitangaza ratiba ijayo ya mikutano ya kupinga serikali huku ikiibuka kuwa maasi ya upinzani yanaweza pia kuhusisha kususia baadhi ya bidhaa na maandamano.

Muungano wa Azimio unafichua hilo baada ya serikali ya Rais William Ruto kutangaza mipango ya kufifisha biashara za rais mstaafu Uhuru Kenyatta na Bw Odinga.

Ratiba mpya ya mikutano ya Azimio imepangwa kuanza Ijumaa na kuendelea hadi Jumatatu wiki ijayo ingawa haijaonyesha maandamano yaliyotarajiwa kuanza Alhamisi, siku moja baada ya makataa ya siku 14 ambayo Bw Raila alimpa Rais Ruto.

Mnamo Februari 22, Odinga alimpa Rais Ruto siku 14 kufungua sava za uchaguzi mkuu wa 2022 na kupunguza gharama ya juu ya maisha lakini hakuna lililobadilika huku Kiongozi wa Nchi akitangaza juzi kwamba hakuna hitaji la kikatiba linalomtaka kufungua sava za Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Bw Odinga alisema mikutano ya Azimio itaanza upya Ijumaa Machi 10 katika kaunti ya Migori, kabla ya vinara wa muungano huo kuelekea kaunti ya Narok, Jumamosi Machi 11.

Jumapili Machi 12, Azimio itafanya mkutano wa hadhara katika Kaunti ya Mombasa na kuelekea Kilifi Jumatatu.

Mnamo Jumamosi iliyopita, Bw Odinga aliahidi kwamba Alhamisi wiki hii atatoa tangazo kubwa kuhusu mbinu zake zijazo za kisiasa, siku moja kabla ya siku ambayo angeanza maandamano aliyotangaza Februari 22.

Jana Jumapili, Taifa Leo ilibaini kuwa Bw Odinga anapanga kuzindua mbinu zaidi ya moja kuhusu mpango wake wa maasi ambao unaweza kuhusisha kususia bidhaa za kampuni zilizounga “kuingia mamlakani kinyume cha sheria kwa Rais Ruto”, kususia ushuru, maasi na maandamano barabarani.

Iwapo atatumia mbinu hizi, Azimio itaanza mipango ya kuhamasisha wafuasi wake kuhusu bidhaa mbadala za kutumia.

Hata hivyo, Kiongozi wa Wachache, Opiyo Wandayi, alihimiza Wakenya kusubiri kuzinduliwa kwa mwongozo wa maasi utakaotolewa na Bw Odinga baada ya ilani ya siku 14 aliyoipa serikali kukamilika.

Alipoulizwa iwapo maandamano yaliyopangwa yatafanyika pamoja na mikutano itakayofanyika maeneo tofauti nchini, Bw Wandayi alisema,“Tuna uwezo wa kuzidisha tukiendelea na mipango yetu.”

“Mawili hayo – mikutano na maandamano – hayatengani sana lakini Wakenya wasubiri mwelekeo wa wazi kutoka kwa kiongozi wa muungano,” Bw Wandayi alisema.

Akihimiza wafuasi wake kuwa tayari kudai “ushindi wao ulioibwa” wakati utakapofika, Bw Odinga alisema makataa ya siku 14 yatakapokamilika Jumatano, atatoa tangazo “litakalobadilisha mwelekeo wa nchi hii”.

Kiongozi wa Azimio alisema wametiwa nguvu na matokeo ya mfichuzi yanayoonyesha kuwa Azimio ilishinda urais kwa zaidi ya kura milioni 2.2 dhidi ya Rais Ruto wa Kenya Kwanza.

Seneta wa Vihiga, Godfrey Osotsi alisema ingawa hafahamu tangazo la Bw Odinga, Alhamisi, kiongozi huyo wa ODM ana mpango mpana wa kukabili serikali ya Kenya Kwanza.

“Maandamano si lazima yawe kwenda barabarani. Kuna mambo mengine kama kususia bidhaa na ushuru na pia maasi ambapo umma unahimizwa kukataa kutii serikali,” akasema Bw Osotsi.

  • Tags

You can share this post!

Mbunge taabani kwa matamshi yake kuhusu wenye ardhi na...

David de Gea alegea na kukubali mabao 7 yaingie Salah...

T L