• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 9:17 PM
Raila atishia kususia kura mpya ikiagizwa

Raila atishia kususia kura mpya ikiagizwa

VALENTINE OBARA Na WINNIE ATIENO

MUUNGANO wa Azimio la Umoja One Kenya ukiongozwa na mwaniaji wake wa urais Raila Odinga, umeashiria hautakubali kushiriki marudio ya uchaguzi wa urais endapo agizo hilo ndilo litatolewa na Mahakama ya Upeo.

Ingawa mojawapo ya maombi ya Bw Odinga na mgombea mwenza wake wa urais, Bi Martha Karua kwa Mahakama ya Upeo ni kwamba Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) iamrishwe kuandaa uchaguzi upya, jana Jumatano Bw Odinga na wandani wake walisema uamuzi pekee watakaotambua ni ule wa kumtangaza yeye mshindi wa urais.

“Tunataka Wakenya wawe na subira. Vile Martha amesema, kesi iko mahakamani. Hatuwezi kuiongelea lakini mawakili wetu wakianza kuzungumza kule mtajionea ukweli. Tunataka kwanza mahakama iseme sisi ndio tulishinda na badala ya kutangaza turudi katika uchaguzi, tutangazwe washindi na tupewe cheti,” akasema Bw Odinga.

Seneta wa Mombasa, Mohamed Faki na Mwenyekiti wa ODM Kaunti ya Kilifi, Teddy Mwambire nao walitilia mkazo msimamo kwamba kile wanachotaka katika Azimio ni Bw Odinga kutangazwa mshindi wala si kuitishwa kwa marudio ya uchaguzi wa urais.

“Ile kesi iko mahakamani ni nzito sana. Hatutaenda kwa uchaguzi mwingine kwani rais na naibu wake wako hapa,” akasema Bw Mwambire.

Walikuwa wakizungumza katika Kaunti ya Mombasa, ambako walizuru kumpigia debe Abdulswamad Nassir kwa ugavana ambao uchaguzi umepangiwa kufanyika Jumatatu ijayo.

CHEBUKATI

Bw Odinga alitilia doa pia mamlaka ya Mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati na kumtaka amkabidhi mamlaka naibu wake, Bi Juliana Cherera.

Kulingana naye, Bw Chebukati hafai kusimamia chaguzi zijazo akidai kuwa yeye ni mshtakiwa katika kesi zinazopinga matokeo ya uchaguzi wa urais uliofanywa Agosti 9.

Lakini IEBC ilimkosoa Bw Odinga muda mfupi baadaye ikisema chaguzi za ugavana Mombasa na Kakamega zitasimamiwa na maafisa wakuu wa uchaguzi wa kaunti hizo, wala sio Bw Chebukati.

Bw Chebukati na naibu wake walitofautiana baada ya Bi Cherera na makamishna Francis Wanderi, Irene Masit na Justus Nyang’aya kukataa matokeo ya kura za urais, ambayo yalitumika kumtangaza William Ruto kuwa mshindi wa urais.

Mnamo 2017, Bw Odinga alikataa kushiriki marudio ya uchaguzi wa urais yaliyoagizwa na Mahakama ya Upeo akisema haingewezekana muungano wao wake wa National Super Alliance (NASA) kushiriki uchaguzi mwingine ikiwa bado ungesimamiwa na Bw Chebukati na makamishna wenzake waliokuwepo wakidai haki haingetendeka bila mabadiliko katika tume hiyo.

Siku ya marudio ya uchaguzi huo wafuasi wa Bw Odinga walizuia maafisa wa IEBC kuandaa kura hiyo huku katika maeneo mengine wakisusia.

Kuhusu chaguzi zinazosubiriwa kufanywa Jumatatu ijayo, Bw Odinga anakumbwa na changamoto ya kushawishi wafuasi wake kujitokeza kwa wingi katika ngome zake za Kakamega na Mombasa.

Hii ni kutokana na kuwa, wakati wa Uchaguzi Mkuu uliofanyika Agosti 9, kaunti hizo mbili zilikuwa miongoni mwa zile zilizovutia idadi ndogo mno ya wapigakura.

Katika Kaunti ya Mombasa, kura za urais zilizopigwa zilikuwa 281,113 licha ya kuwa kuna wapigakura 642,362 waliosajiliwa.

Takwimu hizo pia zinaonyesha kuwa katika Kaunti ya Kakamega, kura za urais zilizopigwa zilikuwa 509,281 ilhali wapigakura waliosajiliwa ni 844,709.

Bw Nassir alidai kuwa kuahirishwa kwa chaguzi za ugavana katika kaunti hizo mbili kulisababisha idadi ndogo ya wapigakura kujitokeza na hivyo kumnyima ushindi wa urais Bw Odinga.

Viongozi hao walitaka IEBC ifungue vituo mapema zaidi Jumatatu, kwa vile hakutakuwa na likizo hivyo basi wapigakura wapate nafasi ya kushiriki uchaguzi kabla ya kwenda kazini.

Chaguzi nyingine zilizokuwa zimeahirishwa ambazo zitafanywa Jumatatu ni katika maeneobunge ya Rongai (Nakuru), Pokot Kusini, Kitui Rural, Kacheliba pamoja na wadi za Kwa Njenga (Nairobi) na Nyaki Magharibi (Meru).

  • Tags

You can share this post!

Magavana wapya kurithi dhambi za watangulizi

VALENTINE OBARA: Pwani bado haijathamini wanawake kama...

T L