• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 10:55 AM
Magavana wapya kurithi dhambi za watangulizi

Magavana wapya kurithi dhambi za watangulizi

NA WAANDISHI WETU

MAGAVANA wapya waliochaguliwa katika uchaguzi wa Agosti 9, wana mtihani mgumu kuweka mikakati itakayotatua changamoto mbalimbali zinazoachwa na wenzao wanaoondoka mamlakani.

Katika ukanda wa Pwani, magavana wanaotarajiwa kuapishwa leo ni pamoja na Bi Fatuma Achani (Kwale), Bw Issa Timamy (Lamu), Bw Gideon Mung’aro (Kilifi) na Bw Andrew Mwadime (Taita Taveta).

Changamoto kama vile kuchelewa kwa mishahara ya wafanyakazi wa kaunti, kodi za juu zinazoathiri biashara, hitaji la kufufua sekta muhimu kama vile utalii na viwanda na uimarishaji wa idara za kutoa huduma muhimu kama vile afya, zimetajwa kuwa miongoni mwa zile zinazowakodolea macho magavana wanaoingia mamlakani kuanzia leo.

Vilevile, imebainika baadhi ya magavana watarithi madeni chungu nzima kutoka kwa watangulizi wao.

Katika Kaunti ya Lamu, wakazi wamekuwa wakilalamikia ukosefu wa dawa na matibabu mengine muhimu katika hospitali na zahanati za umma.

Kaunti hiyo hadi sasa haina chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) kwenye hospitali zake, hali ambayo mara nyingi imelazimu wagonjwa wanaohitaji huduma hiyo kupewa rufaa hadi kaunti nyingine za mbali.

“Nimejionea hali mbaya ya miundomsingi hospitalini King Fahd. Dawa hakuna. Vyoo ni vichafu. ICU pia hakuna. Azma yangu baada ya kuingia ofisini ni kurekebisha haya na nihakikishe kuna ICU kwa manufaa ya watu wetu,” akasema Bw Timamy, alipozuru hospitali hiyo Jumanne.

Mbali na kizungumkuti cha afya, Bw Timamy, ambaye alikuwa gavana mwaka wa 2013 hadi 2017, pia anakabiliwa na changamoto nyingine ya hali duni ya usafi, utumizi wa kiasi kikubwa cha fedha katika mishahara badala ya maendeleo, na mipangilio duni kisiwani Lamu ambayo inadunisha kisiwa hicho kama kivutio cha kimataifa cha utalii.

Kwingineko, baadhi ya wakazi wa Kaunti ya Kilifi, wanamtaka Bw Mung’aro atimize ahadi yake ya kuhakikisha kwamba katika muda wa siku 100 za kwanza mamlakani, uhaba wa dawa katika hospitali za kaunti hiyo utakuwa umetatuliwa.

Katika miaka iliyopita, kaunti hiyo ilikumbwa na changamoto ya kukosa mfumo bora wa kufuatilia dawa zinavyoletwa na kutolewa hospitalini ili kuzuia wizi.

Wakazi wa Kilifi wametaja pia uhaba wa maji kama changamoto kubwa ambayo wangependa itatuliwe haraka na utawala unaoingia.

Kwa upande wake, Bi Achani ana changamoto ya kuendeleza na hata kuboresha zaidi mipango waliyoanzisha pamoja na gavana anayeondoka, Bw Salim Mvurya, alipokuwa naibu wake kwa miaka kumi iliyopita.

Ripoti za Kalume Kazungu, Alex Kalama, Maureen Ongala na Siago Cece

  • Tags

You can share this post!

Ruto awapongeza magavana wanawake walioapishwa

Raila atishia kususia kura mpya ikiagizwa

T L