• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 8:55 AM
Raila kupewa mamlaka iwapo Mswada utapita

Raila kupewa mamlaka iwapo Mswada utapita

NA JUSTUS OCHIENG

HUENDA afisi ya kiongozi rasmi wa upinzani ikabuniwa nchini ikiwa mchakato mpya wa marekebisho ya Katiba utafaulu kuijumuisha humo.

Taifa Leo imeona stakabadhi inayopendekeza kumpa mshikilizi wa wadhifa huo mamlaka makubwa, ikiwemo nafasi ya kuhutubia Bunge kila mwaka, kuteua wanachama katika tume za kikatiba na kupata ufadhili kutoka kwa Hazina ya Kitaifa.
Inatarajiwa kuwa ofisi hiyo itashikiliwa na kiongozi wa Azimio la Umoja-One Kenya, Bw Raila Odinga.

Mswada huo, ambao unalenga kubadilisha Katiba kupitia Bunge, pia unapendekeza kubuniwa kwa wadhifa wa naibu kiongozi rasmi wa upinzani.

Afisi hiyo pia itakuwa na mamlaka na uwezo wa kutafuta ufadhili kutoka sehemu zingine, ikiwemo wafadhili, ili kuongezea katika mgao wake wa fedha kwa ajili ya kugharamia shughuli zake.

Kulingana na Kipengele cha 92A (3) ya mswada huo kielelezo, kiongozi rasmi wa upinzani ataruhusiwa kutambua na kuteua “wafanyakazi ambao watamsaidia kutekeleza majukumu yake na wafanyakazi hao watalipwa kutoka kwa mfuko wa umma kulingana na viwango vilivyowekwa na Tume ya Mishahara (SRC).”

Mswada huo pia unanuia kurekebisha Kipengele 260 cha Katiba kuhusu maana ya “Afisa wa Serikali” kwa kushirikisha kiongozi wa upinzani.

Duru ndani ya Azimio ziliambia Taifa Leo kwamba vinara wa muungano huo, Bw Odinga na Kalonzo Musyoka, walifahamishwa kuhusu mipango ya kuwasilishwa kwa mswada huo, wakati wa mkutano wa Kundi la Wabunge wa Azimio mnamo Jumanne.

Wawili hao wanatarajiwa kupokea nakala za Mswada baada ya kuandikwa na kuchapishwa.

Jana Jumatano, wandani wa Bw Odinga hawakutaka kutoa kauli zao kuhusu pendekezo hilo huku mshirika mmoja wa Bw Musyoka akithibitisha kuandaliwa kwa mswada huo.

“Ni shughuli inayoendelea. Tuzungumze Ijumaa baada ya Mswada kupewa vinara wetu,” mshirika huyo, ambaye aliomba tulibane jina lake, alihoji.

Kulingana na mswada huo kielelezo, mshikilizi wa afisi hiyo anatakuwa “Afisa wa Serikali” na atakingwa dhidi ya mashtaka, hali inayoifanya kuwa mojawapo ya afisi zenye mamlaka makubwa nchini.

“Mshikilizi wa afisi ya kiongozi rasmi wa upinzani hatashtakiwa katika mahakama yoyote nchini kwa muhula wao wote,” unaeleza.

Hata hivyo, Kipengele 92A (1) (n) kinafafanua hivi: “Mshikilizi wa afisi ya kiongozi rasmi wa upinzani hatakingwa dhidi ya mashtaka kwa kosa ambalo afisa huyo anaweza kushtakiwa chini ya mkataba ambayo Kenya imetia saini na inayozuia kinga kama hiyo.”

Kwa mujibu wa Mswada, kinara wa upinzani pia atawasilisha malalamishi ya umma, kupiga msasa matumizi ya fedha na akaunti za umma na kusaka maelezo kuhusu sera na maagizo ya serikali.

Kiongozi huyo pia atateua mwakilishi ambaye ataketi katika kamati mbalimbali za uteuzi wa washikilishi wa tume mbalimbali za kikatiba.

  • Tags

You can share this post!

GWIJI WA WIKI: DJ Kezz

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Tunisia wakosa kuingia 16-bora...

T L