• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
Raila kutumia pia maombi kukabili KKA

Raila kutumia pia maombi kukabili KKA

NA CHARLES WASONGA

KINARA wa Azimio la Umoja-One Kenya Raila Odinga ametangaza mapambano mapya dhidi ya serikali ya Kenya Kwanza na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Bw Odinga jana Jumatano alitangaza kuwa muungano huo utafanya maombi nje ya makao makuu ya tume hiyo yaliyoko jumba la Anniversary, katika barabara ya University Way, Nairobi.

Kiongozi huyo wa upinzani alisema maombi hayo yatafanyika wiki ijayo baada Azimio kufanya mikutano ya hadhara kaunti za Kisii na Kisumu.

“Wiki hii tutakuwa Kisii siku ya Ijumaa, Februari 17. Baadaye tutaelekea Kisumu Jumamosi Februari 18. Ni baada ya hapo ambapo tutafanya maombi,” Bw Odinga akasema alipokutana na maseneta wa Azimio afisini mwake, Nairobi.

Hata hivyo, kiongozi huyo wa Azimio hakutoa tarehe kamili ambapo Azimio itafanya maombi hayo aliyosema yanalenga kuhakikisha kuwa Wakenya watapata IEBC ambayo “italinda haki za raia wote”.

“Maombi haya yatakuwa yakiendeshwa sambamba na mikutano ya hadhara kote nchini kukosoa serikali ya Kenya Kwanza. Tutafanya maombi hayo huku tukishinikiza Kenya Kwanza kushusha bei ya chakula, mafuta, karo na mahitaji mengine muhimu kwa Wakenya,” akasema Bw Raila.

“Tutaombea IEBC ili tupate tume ambayo italinda haki za watu wetu na maombi hayo yatafanyika mbele ya makao makuu ya IEBC siku fulani wiki ijayo,” akakariri.

Kiongozi huyo wa Azimio alishikilia kuwa ni yeye aliyeshinda uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

“Hatufai kokosa kuangazia masuala haya kila mara. Ni kweli kwamba tulipata kura milioni 8.1 na wale wengine walipata kura milioni 5.9 pekee. Huu ni ukweli ambao hauwezi kufichwa chini ya zulia,” Bw Odinga akasema.

Muungano wa Azimio umekuwa ukifanya mikutano ya hadhara sehemu mbalimbali nchini ukiwaelezea wafuasi wake jinsi ulivyopokonywa “ushindi” na IEBC.

Bw Odinga alianza kufanya mikutano hii mnamo Januari 22, mwaka huu baada ya kutolewa kwa ripoti ya mfichuzi mmoja aliyedai kuwa Rais William Ruto hakushinda kwa njia halali. Mfichuzi huyo alidaiwa kuwa mfanyakazi wa IEBC.

Kufikia sasa, Bw Odinga ameongoza mikutano mitatu katika maeneo ya Kamukunji, Jacaranda na Kibra jijini Nairobi pamoja na eneobunge la Mavoko, Kaunti ya Machakos.

Wiki jana, Bw Odinga aliwaongoza viongozi wa Azimio kwa mkutano wa hadhara mjini Busia, magharibi mwa Kenya.

Kwa kuitisha mkutano wa maombi, Bw Odinga na wenzake wanaonekana kuiga mfano wa mrengo wa Kenya Kwanza ambao umekuwa akifanya mikutano ya maombi ya kutoa shukurani kwingi nchini.

Mnamo Jumapili wiki jana, Rais Ruto aliwaongoza viongozi wengine wa Kenya Kwanza katika mkutano wa maombi mjini Nakuru. Aidha, Jumanne, Kiongozi wa Taifa aliongoza maombi ya kitaifa uwanjani Nyayo kuombea mvua baada ya kiangazi kirefu kushuhudiwa nchini.

Wakati huo huo, aliyekuwa Waziri wa Ulinzi, Eugene Wamalwa ameidhinishwa kuwa kiongozi wa chama cha Democratic Action Party of Kenya (DAP-K). Hii inafuatia uamuzi wa Kamati Kuu (NEC) ya chama hicho, katika mkutano uliofanyika katika makao makuu ya chama Nairobi.

Chama hicho pia kilimwidhinisha Bw Wamalwa kuwa mgombea urais kwa tiketi ya DAP-Kenya katika uchaguzi mkuu wa 2027.

  • Tags

You can share this post!

AC Milan wazamisha chombo cha Spurs katika gozi la UEFA...

Borussia Dortmund wapepeta Chelsea 1-0 katika hatua ya...

T L