• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 3:55 PM
AC Milan wazamisha chombo cha Spurs katika gozi la UEFA ugani San Siro

AC Milan wazamisha chombo cha Spurs katika gozi la UEFA ugani San Siro

Na MASHIRIKA

TOTTENHAM Hotspur watakuwa na mtihani mgumu wa kujinyanyua katika uwanja wao wa nyumbani watakaporudiana na AC Milan katika hatua ya 16-bora ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Machi 8, 2023.

Hii ni baada ya masogora hao wa kocha Antonio Conte kupokezwa kichapo cha 1-0 na Milan katika mechi ya mkondo wa kwanza ugani San Siro, Italia. Bao hilo la pekee na la ushindi lilijazwa kimiani na Brahim Diaz aliyeshirikiana vilivyo na Theo Hernandez.

Conte alilazimika kutegemea maarifa ya Pape Sarr na Oliver Skipp katika safu ya kati iliyokosa maarifa ya Pierre-Emile Hojbjerg anayetumikia marufuku na Rodrigo Bentancur anayeuguza jeraha la mguu.

Kutokuwepo kwa vigogo hao kulipunguza makali ya safu ya mbele iliyoongozwa na Harry Kane, Son Heung-min na Dejan Kulusevski.

Ushindi dhidi ya Spurs uliendeleza ufufuo wa makali ya Milan waliokuwa wamepiga sare mbili pekee kutokana na mechi tano za ufunguzi wa mwaka wa 2023 katika Ligi Kuu ya Italia (Serie A).

Spurs walishuka uwanjani San Siro wakitarajiwa kuweka kando maruerue ya kupigwa 4-1 na Leicester City katika pambano lililolipta la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Ingawa Milan ni wafalme mara saba wa bara Ulaya, mechi yao dhidi ya Spurs ilikuwa yao ya kwanza kusakata katika raundi ya muondoano ya UEFA tangu wabanduliwe na Atletico Madrid katika hatua ya 16-bora kwa jumla ya mabao 5-1 mnamo 2013-14.

Milan wameaga soka ya UEFA katika hatua ya 16-bora mara tano kutokana na misimu sita, ikiwemo 2011-12 ambapo walipepetwa 1-0 na Spurs. Hadi kufikia Jumanne usiku, mabingwa hao watetezi wa Serie A hawakuwa wamewahi kushinda Spurs katika mechi nne za awali katika mashindano yote.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Benfica watandika Club Bruges katika UEFA ugenini na...

Raila kutumia pia maombi kukabili KKA

T L