• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 5:50 AM
Raila yuko tayari kufika kortini

Raila yuko tayari kufika kortini

Na CHARLES WASONGA

MPASUKO katika Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ni miongoni mwa masuala ambayo yataangaziwa katika kesi ya kupinga uchaguzi wa urais itakayowasilishwa mahakamani na Azimio la Umoja-One Kenya kesho Jumatatu.

Mnamo Jumamosi, mgombea urais wa muungano huo, Raila Odinga alidokeza kuwa, suala hilo ndilo litakuwa mojawapo ya mihimili ya kesi hiyo itakayowasilishwa katika Mahakama ya Juu, kabla ya saa nane adhuhuri.

“Hadi sasa, hatuna Rais mteule. Uliposikiza yale ambayo makamishna wa IEBC waliokaidi mwenyekiti wao walisema baada ya kuondoka Bomas, utaelewa kuwa kulikuwa na shida,” Bw Odinga akawambia wanahabari nyumbani kwake Karen, Nairobi baada ya kukutana na viongozi wa kidini.

Bw Odinga alitaja ushindi wa mpinzani wake kama wa “muda mfupi tu” akielezea imani kuwa utabatilishwa na majaji wa Mahakama ya Juu.

Mnamo Jumatatu, mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati alimtangaza mgombea urais kwa tiketi ya chama cha United Democratic Alliance (UDA) William Ruto kuwa mshindi katika uchaguzi wa urais kwa kuzoa kura 7,176,141, sawa na asilimia 50.49 ya kura zilizopigwa.

Alifuatwa kwa karibu na Bw Odinga aliyepata kura 6,942,930, sawa na asilimia 48.85 za kura hizo.

Lakini dakika chache baadaye, makamishna wanne wa tume hiyo, wakiongozwa na naibu mwenyekiti Juliana Cherera walipinga matokeo hayo wakisema “hatukuhusishwa katika kuyafikia.”

Bi Cherera aliyeandamana na makamishna Francis Wanderi, Justus Nyang’aya, na Irene Masit wataunga mkono mrengo wa Azimio.

Kwa upande wa utetezi ambao utaongozwa na mawakili wa Dkt Ruto, atashirikiana na Mbw Chebukati, Boya Molu na Profesa Abdi Guliye kuthibitisha kuwa ushindi wa Dkt Ruto ulikuwa halali.

Hii ina maana kwamba, kwa mara ya kwanza katika historia ya IEBC, itakabili kesi ya kupinga matokeo ya urais, iliyoisimamia, ikiwa imegawanyika kuwili.

Kimsingi, mshtakiwa mkuu katika kesi itakayowasilishwa katika Mahakama ya Juu kesho ni IEBC.

Mshirikishi wa Kitaifa wa kundi la waangalizi wa uchaguzi, ELOG, Mulle Musau anasema mgawanyiko katika IEBC utalemaza utetezi wa tume hiyo mbele ya majaji saba wa Mahakama ya Juu wakiongozwa na Jaji Mkuu Martha Koome.

Kwa upande wake, wakili Kibe Mungai anasema licha ya kuwepo kwa migawanyiko katika IEBC, mrengo wa Azimio bado una kibarua cha kushawishi Mahakama ya Juu kwamba, mitandao ya kiteknolojia ya KIEMs ilivurugwa, kulikuwa na vituo bandia vya upigaji kura, baadhi ya kura kutoka maeneo bunge fulani hazikujumuishwa katika hesabu ya mwisho na kulikukwa na hitilafu za kura za urais na zile ambazo zilipigiwa wawaniaji wa nyadhifa nyinginezo.

“Kimsingi, ikiwa mawakili wa Azimio watafaulu kuwashawishi majaji wa Mahakama ya Juu kuwa hitilafu hizi zilikuwa na uwezo wa kuathiri matokeo ya uchaguzi wa urais, basi bila shaka majaji hao watabatilisha ushindi wa Dkt Ruto,” akasema Bw Muigai ambaye ni wakili wa masuala ya kikatiba.

Bw Mungai anaongeza kuwa matokeo ya uchaguzi wa urais, yaliyotangazwa na Bw Chebukati, pia yanaweza kubatilisha ikiwa Mahakama Juu itagundua dosari katika fomu 34A zinazotumiwa kutoa matokeo katika vituo vya kupigia kura.

Mawakili wa Azimio, akiwemo Ndegwa Njiru, wametoa hakikisho kwamba ushahidi walio nao unatosha kubatilisha ushindi wa Dkt Ruto.

Ndani ya siku 14, kuanzia kesho, Jumatatu, mawakili hao watakabiliwa na kibarua ya kushawishi Jaji Mkuu Bi Koome kwamba ushindi wa Dkt Ruto ni haramu.

  • Tags

You can share this post!

Akida kuongoza mashambulizi ya PAOK dhidi ya Rangers Klabu...

Harry Kane atambisha Tottenham dhidi ya Wolves katika EPL

T L