• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Rais Ruto ampiga Raila chenga

Rais Ruto ampiga Raila chenga

MOSES NYAMORI Na CHARLES WASONGA

RAIS William Ruto amefanikiwa kumpiga chenga kiongozi wa upinzani Raila Odinga kwa kumshawishi asitishe maandamano huku akiendelea kupuuza matakwa ya muungano wa Azimio.

Dkt Ruto anaendelea kumpotosha Bw Odinga kwamba amekubali mazungumzo kuendelea kwa lengo la kushughulikia matakwa hayo kama vile kupunguzwa kwa gharama ya maisha, uteuzi wa makamishna wapya wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kwa njia jumuishi miongoni mwa matakwa mengine.

Kwa mfano, bei ya unga haijashuka hadi Sh100, kwa paketi moja ya kilo mbili. Paketi hiyo ingali inagharimu zaidi ya Sh200.

Hii ni licha ya kwamba, mnamo Aprili 22 na Aprili 23, 2023 akiongea katika kaunti za Narok na Machakos, mtawalia, Rais Ruto aliahidi kuwa bei ya unga wa mahindi ingeshuka hadi Sh150 baada ya mahindi ambayo serikali iliagiza kutoka ng’ambo kuwasili katika bandari ya Mombasa.

Lakini tangu wakati huo, bei ya unga haijateremka hadi angalau chini ya Sh200.

Badala yake, Rais Ruto anapigia debe Mswada wa Fedha 2023, unaopendekeza kutoza ushuru wa asilimia 10 kwa malighafi yanayotumiwa kutengeneza bidhaa za chakula kama unga ikiwemo karatasi za kuupakia.

Kwa mujibu wa Chama cha Watengenezaji Bidhaa Nchini (KAM), ushuru huu utachangia kupanda zaidi kwa bei ya unga kuanzia Julai 1, 2023.

“Ushuru wa asilimia 10 kwa karatasi za kupakia unga na bidhaa nyinginezo za vyakula, unaopendekezwa katika Mswada wa Fedha wa 2023, bila shaka utasababisha kupanda kwa bei ya unga ikiwa mswada huo utapitishwa bungeni,” ikasema KMA kwenye taarifa kwa vyombo vya habari Alhamisi.

Isitoshe, mswada huo unapendekeza kutoza ushuru wa Sh5 kwa kilo moja ya sukari, hatua ambayo itachangia kuongezeka zaidi kwa bei ya bidhaa hiyo ambayo tayari imepanda hadi Sh220 kwa kilo jijini Nairobi.

Bei ya mafuta pia inatarajiwa kupanda hata zaidi baada ya mswada huo kupendekeza kuongeza ushuru wa ziada ya thamani (VAT) inayotozwa bidhaa hiyo kutoka Sh8 hadi Sh16 kwa lita moja ya petroli, dizeli na mafuta taa.

Mnamo Jumanne, Rais Ruto aliongoza mkutano wa kundi la wabunge wa Kenya Kwanza katika Ikulu ya Nairobi ambapo aliwarai kupitisha mswada huo, unaopendekeza pia kukata asilimia 3 ya mishahara ya wafanyakazi kufadhili ujenzi wa nyumba, bila kuufanyia marekebisho yoyote.

Kinaya ni kwamba, Rais anaposhinikiza kupitishwa kwa mswada huu, unaopendekeza kupandisha gharama ya maisha, amekuwa akimrai Bw Odinga kuunga mkono mchakato wa mazungumzo ya maridhiano yanayoendeshwa na kamati ya wabunge 14.

Jana Ijumaa, Bw Odinga na viongozi wa Azimio waliokutana Yatta, Machakos, waliendelea kuwarai wabunge wao na Wakenya kwa ujumla kukataa mswada huo. Miongoni mwa masuala ambayo kamati hii yenye uwakilishi wa wanachama saba kutoka kila mrengo (Kenya Kwanza na Azimio) inapasa kujadili na kuafikia kwayo ni kupunguzwa kwa gharama ya maisha.

Aidha, Taifa Leo imebaini kuwa japo mazungumzo hayo yanayumbayumba kutokana na tofauti miongoni mwa wanachama wa mirengo hiyo miwili, jopo lililoteuliwa kuendesha shughuli ya uteuzi wa mwenyekiti na makamishna wa IEBC limekuwa likiendelea kuchapa kazi kama kawaida.

Hii ni licha ya kwamba, Bw Odinga na wenzake katika Azimio, wamekuwa wakishikilia kuwa jopo hilo livunjwe na mchakato huo kuanzishwa upya.

Taifa Leo imebaini kuwa, wanachama wa jopo hilo linaloongozwa na Dkt Nelson Makanda wamekuwa wakikutana kupanga shughuli ya uteuzi wa makamishna. Hii ni ishara kwamba, Rais Ruto amekuwa akitumia mchakato huo wa mazungumzo kumdhibiti Bw Odinga.

Dkt Makanda alithibitisha kuwa yeye na wenzake sita walikutana kwa njia ya mtandao, kupanga shughuli ya uteuzi wa makamishna wa IEBC.

  • Tags

You can share this post!

Koech, Were, Nusra na Mweresa watawala riadha za KDF siku...

Lautaro Martinez aongoza Inter Milan kupepeta Fiorentina na...

T L