• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 4:26 PM
Koech, Were, Nusra na Mweresa watawala riadha za KDF siku ya mwisho

Koech, Were, Nusra na Mweresa watawala riadha za KDF siku ya mwisho

Na AYUMBA AYODI

TINEJA Simon Koech aliduwaza mshindi wa medali ya shaba ya Olimpiki wa mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji Benjamin Kigen, akitawala mbio hizo kwenye riadha za majeshi (KDF) zilizokamilika Ijumaa uwanjani Ulinzi Sports Complex.

Mshindi wa medali ya shaba ya Jumuiya ya Madola mbio za mita 10,000 Kibiwott Kandie alinyakua taji la mita 5,000, siku mbili baada ya kutawala mbio za umbali wa mita 10,000.

Watimkaji wa mbio za kuruka viunzi Wiseman Were na Rukia Nusra walitangazwa mwanariadha bora mwanamume na mwanamke katika mashindano hayo ya siku tatu, mtawalia.

Mashindano hayo yalishuhudia wanariadha 40 wakichaguliwa kuwakilisha KDF kwenye mashindano ya kitaifa yatakayofanyika Juni 22-24 ugani Moi Kasarani.

Waziri wa Ulinzi Aden Duale na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Francis Ogolla walihudhuria mashindano hayo ambapo bingwa wa kitaifa mbio za kuruka viunzi za 400m na 110, Were, alihifadhi mataji yake pamoja na kuibuka bingwa wa 400m na kupokezana vijiti 4x400m. Nusra alinyakua mataji ya 100m kuruka viunzi, 100m, 200m na kupokezana vijiti 4x100m.

Vivian Chebet alitawala mbio za 800m na 400m naye Cornelius Tuwei akatawazwa mfalme mpya wa 800m.

Mtaalamu wa mbio za 400m, Boniface Mweresa, alitumia fursa ya kukosekana kwa bingwa mtetezi Samuel Imeta kutia kibindoni mataji ya 100m na 200m.

Judy Jeruto na Daniel Munguti walinyamazisha mabingwa watetezi Judy Kiyeng na Charles Simotwo katika mbio za 1,500m, mtawalia.

Koech, ambaye alitwaa nishani ya shaba kwenye Riadha za Dunia za chipukizi wa Under-20 mwaka 2021, alimtoka Kigen ikisalia mizunguko miwili na kukata utepe kwa dakika 8:28.02.

Mkazi huyo wa kaunti ya Bomet alifuatwa kwa karibu na Kigen (8:34.41) aliyeshuhudia utawala wake wa miaka mitano ukifika kikomo. Wesley Langat aliridhika na nafasi ya tatu (8:34.95).

“Inafurahisha kunyakua taji langu la kwanza baada ya kufuzu kutoka chuo cha makurutu mwaka jana,” alisema Koech anayepata motisha kutoka kwa mabingwa wa Olimpiki Ezekiel Kemboi na Conseslus Kipruto na mshindi wa medali ya dunia ya U-20 Leonard Bett.

Alisema kuwa ndoto yake ni kurejesha mataji ya dunia na Olimpiki nchini Kenya ambayo Mmoroko Soufiane El Bakkali alitwaa mwaka 2021 na 2022.

TAFSIRI: GEOFFREY ANENE

  • Tags

You can share this post!

Chakula kibovu: Mpishi shuleni Mukumu afunguka

Rais Ruto ampiga Raila chenga

T L