• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 8:50 AM
Ruto aenda kinyume na ahadi ya mahasla

Ruto aenda kinyume na ahadi ya mahasla

ONYANGO K’ONYANGO NA CHARLES WASONGA

NAIBU Rais William Ruto ameonekana kuwachezea shere mahasla kwa kuahidi kuwapa nyadhifa serikalini wandani wake walioshindwa katika kura ya mchujo Aprili iwapo atashinda urais.

Hii ni licha ya kwamba awali, aliahidi kuwa serikali yake italenga kuwaimarisha walalahoi kiuchumi kwa kuwapa vyeo na ufadhili na sio kugawa vyeo kwa wanasiasa matajiri.

Akihutubu katika Kongamano la Kitaifa la Wajumbe wa UDA (NDC) katika uwanja wa Kasarani, Dkt Ruto aliahidi kuwa serikali yake itatoa nafasi kubwa kwa watu wa tabaka la chini.

“Serikali ambayo itaundwa na UDA, pamoja na marafiki zetu katika Kenya Kwanza, ni ile ambayo mama mboga na wanabodaboda ndio watakuwa na usemi mkubwa. Mahalsa watapewa nafasi ya kujiinua kiuchumi na kibiashara,” akasema.

“Sisi sio kama wale washindani wetu katika Azimio ambao haja yao kuu ni kubadilisha Katiba ili kuunda vyeo vya kuzawadiwa viongozi matajiri. Lengo lao kuu ni kugawana mamlaka miongoni mwao na hawajali masilahi ya watu hawa wadogo,” Dkt Ruto akaongeza.

Lakini sasa Dkt Ruto anaelekea kuvunja ahadi hiyo kwa kuahidi kuwatunuku nyadhifa washirika wake waliokosa tikiti za kuwania nyadhifa za udiwani, ubunge, useneta na ugavana kwa tiketi ya chama cha United Democratic Alliance (UDA).

Duru zilieleza Taifa Leo kuwa wengine wao pia wameahidiwa kandarasi katika serikali ya kitaifa na serikali za kaunti ambazo zitaongozwa na magavana wa UDA na vyama tanzu katika muungano wa Kenya Kwanza (KKA).

Dkt Ruto alitoa ahadi hizo katika msururu wa mikutano aliyofanya wiki jana na washindi na walioshindwa katika mchujo wa UDA.

Mikutano hiyo ilifanyika katika makazi yake rasmi ya Naibu Rais mtaani Karen, Nairobi.

Wanasiasa hao waliotoka ngome zake za Rift Valley na eneo la Mlima Kenya, pia walihimizwa kushirikiana kuwezesha UDA kushinda viti vingi.

VYEO NA KANDARASI

Mbunge Maalum Cecily Mbarire, ambaye alishinda tiketi ya UDA kuwania ugavana wa Embu, alithibitisha kuwa washindani wao waliahidiwa vyeo na kandarasi za umma endapo Kenya Kwanza itashinda na kuunda serikali ijayo.

“Dkt Ruto amekuwa akiwatuliza walioshindwa kwa kuwaahidi nyadhifa na zabuni endapo tutashinda urais katika uchaguzi ujao. Hii itahakikisha kuwa kila mtu anahisi kuthaminiwa katika chama chetu,” akasema.

Bi Mbarire alishikilia kuwa watakaofaidi ni wale waliopoteza katika mchujo wa UDA na wakaendelea kujitolea kuunga mkono washindi kuelekea uchaguzi mkuu ujao.

“Kelele hazisikiki ndani ya UDA kwa sababu Naibu Rais ameamua kuwapatanisha washindi na walioshindwa,” akaongeza.

Mbunge wa Keiyo Kusini, Daniel Rono, ambaye ni miongoni mwa waliopoteza katika mchujo wa UDA na aliyepatanishwa na mshindani wake mbele ya Dkt Ruto, pia alithibitisha kuwa aliahidiwa cheo serikalini. Lakini hakutaja cheo chenyewe.

“Wengine wetu tumeahidiwa kazi serikalini. Wale ambao watakosa nafasi hizo watapewa kandarasi katika asasi za umma kulingana na sheria za utoaji zabuni serikalini,” akasema munge huyo anayehudumu muhula wa kwanza.

Chama cha UDA, kinachoongozwa na Dkt Ruto, kilikuwa na jumla ya wawaniaji 5,700 waliong’ang’ania tiketi zake kuwania nyadhifa mbalimbali katika uchaguzi mkuu ujao.

Lakini wiki jana, chama hicho kilitoa vyeti vya uteuzi kwa wawaniaji 1,745 pekee kwa walioshinda kuwania ugavana, useneta, ubunge na udiwani kwa tiketi ya UDA.

Hii ina maana kuwa jumla ya wawaniajia 3,900 walikosa tiketi na ndio wale ambao Dkt Ruto ameahidi kuwatunuku vyeo na kandarasi serikalini.

Inaonekana kuwa wafuasi wengine wa UDA, ambao hawakushiriki mchujo huenda wasiwe na nafasi bora ya kufaidi kwa nyadhifa na kandarasi.

  • Tags

You can share this post!

Pasta amezea mate kiti cha Wetang’ula

WANDERI KAMAU: Rais na naibu wake wamemkosea heshima Mzee...

T L