• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 3:55 PM
Ruto asukumwa ajiuzulu kwa kumkaidi Uhuru

Ruto asukumwa ajiuzulu kwa kumkaidi Uhuru

CHARLES WASONGA na COLLINS OMULO

NAIBU Rais William Ruto ameendelea kuwekewa presha ajiuzulu la sivyo atimuliwe afisini kwa kumkosoa hadharani Rais Uhuru Kenyatta na ajenda zake.

Kwenye kikao na wanahabari Nairobi Jumanne, Naibu Kiongozi Chama cha Amani National Congress (ANC) Ayub Savula alitisha kudhamini hoja ya kumwondoa afisini Dkt Ruto bunge litakaporejelea vikao vya Februari ikiwa hatajiondoa kwa hiari.

Nao baadhi ya madiwani wa Nairobi walimtaka Naibu Rais ajiondoe serikalini badala ya kumkosea heshima bosi wake, Rais Kenyatta, kwa kumkosoa hadharani.

“Asipojiuzulu tutawasilisha hoja ya kumwondoa mamlakani kwa sababu amegeuka kuwa tisho kwa uthabiti wa nchi kwa kuendelea kumuasi Rais na kuvuruga ajenda za serikali,” Bw Savula akasema katika makao makuu ya ANC, mtaani Lavington.

Mbunge huyo wa Lugari, ambaye alikuwa ameandamana na maafisa wengine wa chama hicho kinachoongozwa na Musalia Mudavadi, alimkosoa Dkt Ruto kwa kutaja kauli ya Rais Kenyatta kuhusu urais wa mzunguko kama hatua ya kuendeleza ukabila.

“Ikiwa Rais Kenyatta anaendeleza ukabila mbona anataka uungwaji mkono kutoka kwa jamii ya Wakikuyu anakotoka kiongozi wa taifa?” akauliza Bw Savula akirejelea kauli ambayo Dkt Ruto alitoa Jumapili akipinga pendekezo hilo la Rais Kenyatta.

Akihutubu Jumamosi katika mazishi ya Mama Hanna Mudavadi, ambaye ni mamake Bw Mudavadi, katika kaunti ya Vihiga Rais Kenyatta alisema kwamba, makabila ya Wakikuyu na Wakalenjin pia yanapasa kuwapisha watu kutoka jamii zingine waliongoze taifa.

“Ruto aliapa kuwatumikia Wakenya kwa uadilifu kwa kumsaidia Rais kuendesha ajenda za serikali. Lakini Ruto amekwenda kando na kukaidi kiapo cha kuwa mwaminifu kwa Rais,” akaongeza Savula.

Nao madiwani wa Nairobi wakiongozwa na Naibu Spika Geoffrey Majiwa walimtaka Dkt Ruto ajiuzulu ikiwa “anahisi joto jikoni ni kali zaidi kiasi kwamba hawezi kumudu.”

Walimkumbusha Naibu Rais kwamba, mrengo wake wa Tangatanga ndio ulianza siasa za kikabila kwa kuzunguka kote nchini wakidai Wakenya hawako tayati kuongozwa na Rais mwingine Mkikuyu.

Madiwani walishangaa ni kwa nini wanachama wa vuguvugu hilo sasa wamebadili msimamo kufuatia kauli ya Rais ambayo walifasiri kumtenga Ruto ambaye anatoka jamii ya Wakalenjin.

“Ikiwa wamesahau, tungependa kuwakumbusha kuwa ni Kimani Ichung’wa (Mbunge wa Kikuyu), Moses Kuria (Gatundu Kusini) na Seneta wa Elgeyo Marakwet ambao mwaka mmoja uliopita walisema Kenya haiko tayari kwa Rais mwingine Mkikuyu,” akasema Bw Majiwa ambaye ni diwani wa wadi ya Baba Dogo.

“Wakati huo walidhani kuwa walikuwa wakimfanyia kampeni Naibu Rais ambaye sio Mkikuyu. Wakenya walipodinda kukumbatia propaganda hiyo, wakabadili wimbo na kuanzisha siasa za mahasla (masikini) kupiga vita viongozi ambao wazazi wao waliwahi kushikilia nyadhifa za uongozi nchini,” akaongeza.

Diwani wa Mugumoini Jared Akama alisema Kenya ina makabila 43 na sio lazima nchi hii iongozwe na makabila mawili na kwamba makabila mengine hayawezi kuongoza.

Akizungumza Vihiga Jumamosi, Rais Kenyatta alilaani siasa zinazoendelezwa na kundi la Tangatanga la kugonganisha matajiri na masikini.

You can share this post!

Mwanamume wa familia ya Rais Kenyatta auawa Gatundu

Aliacha kazi ya udaktari kufuga nguruwe na kukuza migomba