• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
JAMVI: Ruto hatarini kupoteza chambo chake kisiasa

JAMVI: Ruto hatarini kupoteza chambo chake kisiasa

VALENTINE OBARA na PATRICK LANG’AT

NAIBU Rais William Ruto yuko hatarini kupoteza ushawishi ambao amepata miongoni mwa wananchi wa tabaka la chini kufikia sasa.

Hii ni baada ya wapinzani wake wa kisiasa kuvamia chambo alichokuwa akitumia kunasa imani za wananchi hao kisiasa.

Kwa muda mrefu sasa, Dkt Ruto anayepanga kuwania urais mwaka ujao amekuwa akitumia falsafa ya kuinua kiuchumi wananchi wa matabaka ya chini anayewatambua kama ‘hustlers’, kama mbinu ya kujenga uchumi wa nchi endapo ataunda serikali ijayo.

Falsafa hii ilikosolewa na wapinzani wake wa kisiasa kama mbinu ya kusababisha mgawanyiko unaoweza kuleta vita kati ya matajiri na maskini nchini.

Lakini kwa wiki chache zilizopita, vigogo wengine wa kisiasa nchini wameonekana wakianza kushabikia falsafa hiyo hiyo ya kutilia maanani kuinua uchumi wa raia mashinani kama njia ya kuboresha uchumi wa kitaifa.

Kiongozi wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga, mwenzake wa Wiper Kalonzo Musyoka na kiongozi wa Amani National Congress (ANC), Bw Musalia Mudavadi katika hotuba zao wameanza kusisitiza kuhusu umuhimu wa serikali kuwekeza zaidi katika mbinu ambazo zitainua walalahoi kiriziki.

Ijapokuwa hatua hii huenda ikafanya raia ambao walikuwa wameanza kumtazama Naibu Rais kama mkombozi wao waone kuna viongozi wengine wenye uwezo wa kuwatendea yale ambayo Dkt Ruto alikuwa akiwaahidi, naibu rais na wandani wake wamejipiga kifua kwamba hiyo ni ishara tosha wapinzani wake wameingia baridi.

Kulingana na Seneta wa Murang’a, Bw Irungu Kang’ata, ambaye ni mmoja wa wandani wakuu wa Dkt Ruto, wapinzani wa naibu rais wamegundua kwamba ujumbe wake ulikuwa unapokewa vyema na raia wa kawaida.

“Ujumbe huo sasa umewapa wanasiasa wengine ajenda ya kuzungumzia. Hii ni hatua nzuri kwa vile inafanya siasa iwe ya kujadili masuala muhimu badala ya mambo ya kibinafsi na ukabila ambazo ni hatari kwa utulivu wa nchi. Inaridhisha kuwa Ruto ndiye alianzisha mazungumzo aina hii,” akaeleza.

Bw Odinga ambaye kwa siku kadhaa sasa amekuwa akionyesha dalili za kujiandaa kuwania urais 2022, alisema hitaji la kuinua wananchi wa ngazi za chini kiuchumi ili kukuza uchumi wa kitaifa ni mbinu inayowezekana kutekelezwa.

Katika taarifa alizotoa wiki iliyopita, Bw Odinga alieleza kuwa ukuaji wa uchumi wa nchi hustahili kufaidi kila mmoja bila ubaguzi, badala ya kunufaisha watu wa tabaka la juu pekee.

Kulingana naye, mpango huu unaweza kutekelezwa kwa kulenga wakazi wa maeneo ya mashambani na wafanyabishara wadogo mijini.

“Biashara ndogo ndogo ndizo uti wa mgongo kwa ukuaji wa uchumi. Huwezi kutegemea uwekezaji unaotoka nchi za kigeni pekee. Si jukumu la wawekezaji wa kigeni kuja nchini kukuza uchumi. Lengo lao ni kupata faida na kuzirudisha katika nchi zao. Lakini mwekezaji wa humu nchini atarudisha faida hizo kujenga uchumi wa nchi hii,” alisema Bw Odinga.

Kwa upande wake, Bw Mudavadi ambaye ameanzisha kaulimbiu ya ‘Uchumi Bora’ anapopanga kuwania urais mwaka ujao hushikilia kuwa uchumi wa nchi umezorota na unahitaji mikakati kabambe kufufuliwa ili kunusuru hali ya kiriziki kwa wananchi.

Sawa na Bw Odinga, kiongozi huyo wa ANC alisema katika taarifa kwamba hakutakuwa na mafanikio makubwa ikiwa serikali itaendelea kujishughulisha na utekelezaji wa miradi mikubwa wakati ambapo raia wa ngazi za chini wangali wanateseka kujitafutia riziki yao ya kila siku.

“Ni vizuri kujenga barabara na reli za kisasa, na pia viwanda vikubwa vya kuzalisha umeme. Lakini, je, hayo yote yatakuwa kwa manufaa gani wakati ambapo wananchi hawana uwezo wa kugharamia huzuma zinazotokana na miradi hiyo kwa sababu tumepuuza kuinua uwezo wao kupitia kwa miradi kama vile kilimo, afya na usambazaji maji safi?” akauliza Bw Mudavadi.

MASHINANI

Akiwa katika ziara ya kukagua miradi ya maendeleo eneo la Ukambani, Bw Musyoka alisisitiza kwamba amekuwa katika mstari wa mbele kutetea maendeleo ya mashinani kwa muda mrefu.

Hata hivyo, alisema misimamo yake haifanani ya ile ya Dkt Ruto, akieleza kuwa naibu rais ana falsafa ya kuwapa wananchi vya bwerere wala si kupeleka maendeleo ambayo yatawainua kiuchumi kwa muda mrefu.

“Kiongozi kama mimi sio kwenda kupeleka vitu na wilibaro. Sio kupeana vitu vya bwerere bali maendeleo ya kikweli kuanzia chini. Ni kupotosha watu unapowapa wilibaro kisha unadai hiyo ni njia ya kukuza uchumi kutoka chini. Aina hiyo ya kisiasa ni ya kuwapa wananchi vya bwerere na tulitoka huko,” akasema.

Licha ya kuwa misimamo hii inaweza kumvurugia Dkt Ruto hesabu zake za kunasa wapigakura wa mashinani kupitia kwa falsafa aliyoanzisha, naibu rais na wandani wake husema kilicho muhimu ni kwamba sasa viongozi wanajadiliana kuhusu mbinu wanazonuia kuinua uchumi badala ya kushambuliana kwa misingi ya ubinafsi ambayo haitakuwa na manufaa kwa umma.

Hata hivyo, baadhi ya wandani wa wapinzani hao wa Dkt Ruto walidai kuwa falsafa inayoenezwa na vigogo hao watatu ni tofauti na ile ya naibu rais.

Kulingana nao, falsafa ya naibu rais ilinuia kuwapa raia vitu vya bwerere ili wampigie kura uchaguzini na hilo halingewasaidia wananchi katika miaka ya usoni.

Kwa upande mwingine, wanadai kuwa falsafa ya vinara wao inagusia kwa mapana na marefu jinsi watakavyowekeza katika uchumi wa mashinani ili raia wa ngazi za chini wawe na pesa mifukoni mwao.

“Wao wamezoea kupiga domo bila mpango kwa njia ambayo maoni yao hupotea punde tu wanapoambiwa wajieleze kwa kina. Huu ni wakati ambapo watu wanafaa kukoma kupiga domo na waanze kueleza kwa kina jinsi watakavyoinua uchumi na kuwezesha wananchi kuwa na pesa mifukoni. Wakenya wachanganue kwa undani mapendekezo yote yanayowasilishwa kwao,” akasema Katibu Mkuu wa ODM, Bw Edwin Sifuna.

Kwa upande wake, Katibu Mwandalizi wa Wiper, Bw Robert Mbui alisema katika mahojiano ya runinga: “Kinachofaa kupingwa ni jinsi wanasiasa wanavyosambazia wananchi pesa. Vijana wanafaa kujua taifa linawategemea wao, kuwa wanaweza kuanzisha biashara bali si kusubiri serikali iwasaidie. Tunataka wajue serikali ipo kuwasaidia. Ukiambia watu kuwa utawapa pesa kujiendeleza watakuwa wavivu wakisubiri hizo pesa.”

Hata hivyo, mtaalamu wa masuala ya kiuchumi, Bw Mohamed Wehliye aliwarai wananchi wajihadhari na mapendekezo yote yanayotolewa na wanasiasa kwani viongozi hawaelezi mipango yao kwa uwazi inavyofaa.

Kando na mbinu ya kufufua uchumi kuanzia chini, mbinu nyingine zinazoweza kuzingatiwa ni kuanzia ngazi za juu kwenda chini au kuanzia katikati.

“Mbinu yoyote ile inayopendekezwa kuinua uchumi itahitaji rasilimali. Wanasiasa wanaotaka kuwania urais hawafai tu kutuambia kuhusu mwelekeo watakaochukua bali pia jinsi watakavyotatua tatizo la madeni ambayo watarithi ili wapate fedha wanazohitaji kufadhili mipango yao,” akasema, kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter.

You can share this post!

Magoha azuia vyuo vikuu kuongeza karo, mageuzi

TAHARIRI: Kura si mwisho wa maisha, tulinde utu