• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 3:24 PM
Ruto na Raila wang’ang’ania Magharibi

Ruto na Raila wang’ang’ania Magharibi

NA JUSTUS OCHIENG

UTEUZI wa aliyekuwa Seneta wa Kakamega, Cleophas Malala, kama Katibu Mkuu mpya wa chama tawala cha UDA umezua mwelekeo mpya kwenye juhudi za kupigania uongozi wa eneo la Magharibi miongoni mwa wanasiasa tofauti.

Kwa sasa, Bw Malala anajiunga na wanasiasa wengine saba wanaowaunga mkono Rais William Ruto na kiongozi wa Azimio, Raila Odinga, wanaopigania uongozi wa jamii ya Abaluhya, ambapo watatu kati yao washatangaza nia za kuwania urais.

Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi, Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula, Naibu Kiongozi wa ODM Wycliffe Oparanya, aliyekuwa Waziri wa Ulinzi Eugene Wamalwa, aliyekuwa mwaniaji urais George Wajackoyah, Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna na Waziri wa Michezo Ababu Namwamba wote wanapigania uongozi wa jamii ya Mulembe.

Bw Malala anasema kuwa amejitayarisha kuivumisha UDA katika eneo hilo na nchi nzima kwa jumla. Ni hali inayotajwa kuwa huenda ikawaathiri washirika wake wa zamani.

Kwenye juhudi zake za kushinikiza vyama vyote washirika katika muungano wa Kenya Kwanza kuvunjwa, huenda Bw Malala akawa katika nafasi yenye ushawishi kisiasa kuwaliko Bw Mudavadi na Bw Wetang’ula katika upande wa serikali.

Hata hivyo, kwenye juhudi za kutuliza joto la kisiasa, Bw Malala alipuuzilia mbali madai kuwa Bw Mudavadi hakufurahishwa na hatua yake kuhama kutoka chama cha ANC, ambacho alitumia kuwania ugavana katika Kaunti ya Kakamega kwenye uchaguzi wa Agosti 9 mwaka uliopita. Alisema Bw Mudavadi alikuwa na ufahamu kuhusu uamuzi wake.

“Yeye (Mudavadi) aliniruhusu kujiunga na UDA, hivyo nawataka kujua kwamba hakuna jambo lolote tulilofanya kisiri. Hatuwezi kuchukua mwelekeo kama huo bila kumfahamisha. Hata Gavana Issa Timamy, ambaye ndiye kaimu kiongozi wa chama, anafahamu,” akasema Bw Malala.

Ijapokuwa Bw Mudavadi amesema hatawania urais 2027 na badala yake atamuunga mkono Dkt Ruto, washirika wake wanalenga siasa za urithi 2032, hali inayoonekana kutomfurahisha Naibu Rais Rigathi Gachagua.

Hatua ya Bw Wetang’ula kuendelea kushikilia uongozi wa chama cha Ford Kenya licha ya kuwa mfanyakazi wa serikali inaonekana kama njama ya kuendeleza ushawishi wa kisiasa na udhibiti wa eneo hilo.

Kwa Bw Oparanya, Bw Wamalwa na Prof Wajackoyah—aliyewania urais kwenye Uchaguzi Mkuu mwaka uliopita—wametangaza watawania urais huku nafasi za Bw Sifuna na Bw Namwamba katika mirengo ya Bw Odinga na Rais Ruto mtawalia zikiwapandisha hadhi kisiasa.

Bw Mudavadi hatawania urais 2027 kumkabili Dkt Ruto.

  • Tags

You can share this post!

Mafuta yaanza kupungua tena vituoni

Bunge la Kenya na la Hungary kuimarisha ushirikiano, asema...

T L