• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 7:15 PM
Ruto, Raila pabaya kwa kutumia ‘mali ya umma’ kujipigia debe

Ruto, Raila pabaya kwa kutumia ‘mali ya umma’ kujipigia debe

NA MERCY SIMIYU

MASHIRIKA sita ya kijamii yanataka wawaniaji wakuu kwenye uchaguzi wa urais mwezi Agosti wakome kutumia rasilmali za serikali kwenye kampeni zao.

Yanataka mwaniaji urais kupitia Azimio la Umoja One Kenya Alliance, Raila Odinga na mwenzake wa United Democratic Alliance (UDA), William Ruto, wafanye kampeni za kujipigia debe bila kutumia magari na mali nyingine ya umma.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari Jumapili, mashirika hayo yaliungana kukashifu hasa maafisa wa umma ambao wameonekana hadharani kupigia debe kambi mbalimbali za kisiasa.

“Tunasikitishwa, na vile maafisa wa umma wanatumali mali ya umma ili kufaidisha hisia zao za kisiasa. Si sawa kwamba kuna wale wanatumia mali ya umma na serikali na wale wanajitahidi kutotumia mali ya umma. Kulingana na sheria za Kenya, hakuna afisa wa umma anayeruhusiwa kutumia rasilimali za serikali kuonyesha mrengo wa kisiasa ambao ana unga mkono,” ikasema taarifa ya mashirika hayo yaliyojumuisha Transparency International.

Mengine ni Elections Observations Group (ELOG), Center for Multiparty Democracy (CMD Kenya), Mzalendo Trust, Constitution and Reform Education Consortium (CRECO) na Electoral Law and Governance Institute for Africa (ELGIA).

Majuzi Dkt Ruto aliandikia Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) na taasisi nyingine kulalama kuwa baadhi ya mawaziri wamekuwa wakionyesha hadharani kuwa wanamuunga mkono Bw Odinga.

Mashirika hayo pia yanataka IEBC itoe majina ya vituo vya uchaguzi nchini ambako hakuna mtandao wa 4G.

“Juzi IEBC ilitutangazia kuwa vituo vya uchaguzi 1,111 havifikiwi na mtandao wa 4G. Hata majaribio ya kupeperusha matangazo yalionyesha kulikuwa na ucheleweshaji, na ufanisi ulikuwa wa chini ya asilimia 50. Hili ni jambo la kutia shaka, ikizingatiwa kuwa zimebaki siku 58 pekee kabla ya siku ya uchaguzi,” ikasema taarifa ya mashirika hayo.

Mnamo Juni 8, IEBC iliahirisha uchapishaji wa sajili ya wapigakura, baada ya ripoti ya ukaguzi kuonyesha bado kuna masuala yanayohitaji kushughulikiwa.

Ripoti ya kampuni ya KMPG ilifichua kwamba kati ya wapigakura waliokuwa kwenye sajili ya IEBC, 266,465 wameshafariki. Wengine 481, 711 majina yao yanajirudia zaidi ya mara moja, na watu 226,143 nambari zao za vitambulisho au pasipoti si sahihi.

Mashirika hayo pia yalikashifu mtindo unaoendelea kujitokeza miongoni mwa vyama vya kisiasa kugawa maeneo ya nchi na kudai kuwa ngome zao.

Vinara mbalimbali wa mirengo ya siasa wamekuwa wakizunguka na kutangaza kuwa sehemu fulani ni ngome ya Azimio, Kenya Kwanza au vyama vingine, na kuwataka wakazi wapige kura mfumo wa suti.

Mfumo huo huhakikisha kuwa kura ya rais hadi ile ya MCA inapewa watu wanaotoka chama au mrengo mmoja.

  • Tags

You can share this post!

Wakazi waonywa wanasiasa hawawezi kuwatatulia shida za...

MWALIMU WA WIKI: Mulwa ana siri zote za mwalimu bora

T L