• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 3:46 PM
Ruto sasa ‘anyakua’ jukumu la Gachagua

Ruto sasa ‘anyakua’ jukumu la Gachagua

NA WANDERI KAMAU

RAIS William Ruto sasa anaonekana kuchukua jukumu la kulainisha sekta ya kahawa kutoka kwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, baada ya kutangaza Jumapili kwamba yeye binafsi ndiye atakabiliana na watu wenye ushawishi wanaoidhibiti sekta hiyo.

Hatua ya Rais inaonekana kusukumwa na ongezeko la vilio kutoka kwa wakulima, wengi wakilalama kwamba bado wanaendelea kupunjwa na madalali ambao wamekuwa wakiidhibiti sekta hiyo kwa muda mrefu.

Kwenye mahojiano na kituo kimoja cha televisheni Jumapili usiku, Rais Ruto alifichua kuhusu ushawishi na nguvu nyingi zilizo na madalali hao, akisema kuwa sasa ameamua kukabiliana nao moja kwa moja.

“Kuna shida. Ninajua. Kukabiliana na watu hao (makateli) ndilo jukumu langu. Hao watu watakutana na mimi ana kwa ana. Sababu ni kwamba tuna kahawa bora zaidi,” akasema Rais Ruto alipohojiwa katika Ikulu Ndogo ya Sagana, Kaunti ya Nyeri.

Kauli ya Rais ilionekana kumnyang’anya jukumu hilo Bw Gachagua, ambaye kulingana na Agizo la Kwanza la Rais alilotoa Januari kuhusu mpangilio wa serikali, alimkabidhi Bw Gachagua usimamizi wa mikakati ya kulainisha sekta za kilimo cha kahawa, majanichai na ufugaji.

Kutokana na jukumu hilo, Bw Gachagua amekuwa akiongoza mikakati ya kulainisha kilimo cha mazao hayo kupitia makongamano kadhaa katika sehemu tofauti za nchi.

Mnamo Juni, Bw Gachagua aliongoza Kongamano la Kahawa lililodumu siku tatu katika Kaunti ya Meru. Kongamano hilo lilifanyika kati ya Juni 8 na Juni 10, ambapo washiriki walijadili kuhusu mikakati mbalimbali ya kuimarisha sekta hiyo, nchini.

Kwenye kongamano hilo, Bw Gachagua alieleza kujitolea kwake katika kuhakikisha wafanyabiashara hao wamekabiliwa ifaavyo, ili kuwapa nafasi wakulima kupata mapato pia.

“Ningetaka kuwaambia watu hao kwamba wakati wao umekwisha. Lazima watupe nafasi kuifanyia mageuzi sekta hiyo au tutawaondoa sisi wenyewe. Hali si kama ilivyokuwa nyakati zilizopita. Huu ndio utawala utakaosuluhisha matatizo yanayohusishwa na watu hao wenye ushawishi katika sekta za kahawa, majanichai na ufugaji, na kuwarejeshea wakulima furaha waliyokuwa nayo nyakati za hapo nyuma,” akasema Bw Gachagua.

Baada ya kongamano hilo, Bw Gachagua aliongoza kongamano lingine mwezi uliopita, kuhusu mageuzi katika sekta ya majanichai katika Kaunti ya Kericho.

Kama mjini Meru, aliwarai wakulima kujitokeza na “kueleza na ukweli kuhusu mageuzi ambayo wangetaka serikali kuifanyia sekta hiyo”.

“Nawaalika na kuwataka muwe wakweli kuhusu mikakati ambayo mngetaka tuitekeleze. Tuelezeni changamoto ziko wapi. Haya ndiyo mazungumzo ya mwisho tutakayokuwa nayo kuhusu majanichai. Hatuwezi kuwa tukirudia masuala haya kila mwaka. Ni wakati mtwambie watu wanaowanyanyasa katika sekta hii ili tuwachukulie hatua,” akasema Bw Gachagua, kwenye hali iliyoonyesha kuwa ndiye nahodha kuu wa utawala wa Kenya Kwanza kwenye juhudi za kulainisha kilimo.

Bw Gachagua pia amepangiwa kuongoza kongamano lingine kuhusu ufufuzi wa kilimo cha zao la miraa.
Mara tu baada ya kongamano la kahawa mjini Meru, Bw Gachagua aliwarai Wakenya kumwombea, kwani “wafanyabiashara hao ni wenye nguvu sana.”

“Nawarai Wakenya kuiombea. Ninakabiliana na kibarua kigumu sana. Watu hao (makateli) ni wenye nguvu sana. Kama familia, wakati mwingine huwa tunatuhumu kwamba ndio waliomuua marehemu ndugu yangu Nderitu Gachagua kutokana na vita alivyokuwa ameanza dhidi yao. Lazima nitahadhari kuhusu watu ninaotangamana nao hata ikiwa nina usalama wa kutosha,” akasema Bw Gachagua.

Kutokana na kauli ya Jumatatu ya Rais Ruto, wadadisi wanasema kuwa hali hiyo inaonyesha kibarua walicho nacho viongozi hao wawili katika kuleta mageuzi katika sekta ya kilimo.

Wanasema ijapokuwa huenda Rais hakutangaza wazi kumnyang’anya Bw Gachagua jukumu hilo, kuna uwezekano limeibukua kuwa “mzigo mkubwa kuliko alivyodhani”.

Kwenye mahojiano hayo, Rais Ruto alijitetea vikali dhidi ya kuonekana “kuingilia” utendakazi wa baadhi ya mawaziri na makatibu wa wizara, akisema kuwa yeye ndiye atalaumiwa ikiwa watakosa kutimiza majukumu waliyopewa na Wakenya.

Hilo linafuatia kauli yake wiki iliyopita, ambapo aliwakosoa baadhi ya mawaziri wake kuchelewa na hata kutofahamu yale yanayoendelea katika wizara zao.

  • Tags

You can share this post!

Utawala wa kijeshi wafunga anga ya Niger

Uchunguzi waanzishwa baada ya mwanamume kufa kwa kujirusha...

T L