• Nairobi
  • Last Updated February 22nd, 2024 2:11 PM
Utawala wa kijeshi wafunga anga ya Niger

Utawala wa kijeshi wafunga anga ya Niger

NA MASHIRIKA

NIAMEY, NIGER

VIONGOZI wa utawala wa kijeshi nchini Niger, sasa wamefunga anga ya taifa hilo, baada ya kukaidi makataa waliyokuwa wamepewa na mataifa ya ukanda wa Afrika Magharibi kumrejesha mamlakani Rais Mohamed Bazoum.

Viongozi hao walikuwa wamepewa makataa ya hadi Jumapili kumrejesha kiongozi huyo mamlakani, la sivyo taifa hilo likabiliwe kijeshi.

Tishio hilo lilitolewa na mataifa wanachama wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi (ECOWAS), ambapo yamepata uungwaji mkono wa nchini kama Ufaransa.

Hatua hiyo ilitangazwa Jumapili jioni, huku maelfu ya watu wanaouunga mkono utawala huo wakijitokeza kwa wingi katika uwanja mmoja ulio katika jiji kuu la taifa hilo, Niamey. Waliwashangilia majenerali wa kijeshi walioipindua serikali —au Baraza Kuu la Kuilinda Nchi (CNSP).

Akitoa tangazo hilo, msemaji wa utawala huo, Amadou Abdramane, alitangaza tishio la uvamizi wa kijeshi kutoka kwa ECOWAS kama hatua ya kufanya maamuzi hayo.

Kwenye taarifa iliyosomwa katika kituo cha televisheni cha serikali, msemaji huyo alieleza kuwa tayari, mataifa mawili ya eneo la Afrika ya Kati yamewatuma wanajeshi wake nchini humo tayari kutekeleza uvamizi, ijapokuwa hakuyataja.

“Kutokana na tishio zinazoendelea kutukabili kutoka kwa mataifa jirani, tumefunga anga ya Niger kutoka siku hii (Jumapili). Hakuna ndege itakayokubaliwa kupaa hadi tutakapotoa tangazo jingine,” akasema.

Akaongeza: “Jeshi la Niger na vikosi vyote vya usalama, kupitia uungwaji mkono wa raia, viko tayari kuitetea na kuilinda nchi yetu.”

Mapinduzi hayo ya kijeshi yaliyotokea mwezi uliopita, ndiyo ya saba katika nchi zilizo katika ukanda wa Magharibi na Kati mwa Afrika, kwa muda wa miaka mitatu iliyopita.

Mapinduzi hayo yamekuwa yakitokea katika mataifa yaliyo katika eneo la Sahel, licha ya mengi kukabili uvamizi wa makundi ya wanamgambo yanayohusishwa na mitandao ya kigaidi ya Al-Qaeda na Islamic State (ISIL). Eneo hilo ni miongoni mwa maeneo maskini zaidi duniani.

ECOWAS imekashifu vikali mapinduzi hayo, kwa kuweka vikwazo kadhaa vya kiuchumi na usafiri kwa viongozi wa mapinduzi hayo. Pia, imesimamisha utoaji umeme kwa Niger.

Viongozi wa kijeshi katika mataifa hayo wamekubaliana kwa pamoja kuhusu hatua ya kuiingilia nchi hiyo kijeshi, ikiwa Rais Bazoum hataachiliwa na kurejeshwa mamlakani.

Kufikia Jumatatu, ECOWAS haikuwa imetoa taarifa yoyote kuhusu hatua itakayochukua dhidi ya Niger, baada ya makataa yake kwa utawala huo wa kijeshi kuondoka mamlakani kuisha Jumapili.

Wadadisi wanasema kuwa hatua ya viongozi hao kufunga anga ya Niger inaonyesha ukaidi wa wazi dhidi ya vitisho vya ECOWAS.

Licha ya tishio hilo, mataifa kadhaa ya ukanda huo bado hayajachukua msimamo rasmi. Nigeria, Senegal na Ivory Coast zimesema zitawatuma wanajeshi, ijapokuwa Bunge la Seneti nchini Nigeria lilikataa ombi la Rais Bola Tinubu kukubaliwa kutuma jeshi nchini humo.

  • Tags

You can share this post!

Mwanamume anayedaiwa kuwaua kwa kuwachinja wanawe akamatwa

Ruto sasa ‘anyakua’ jukumu la Gachagua

T L