• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 9:16 PM
Sababu za Ahmed Khalif kuwa waziri kwa siku 20 pekee

Sababu za Ahmed Khalif kuwa waziri kwa siku 20 pekee

NA KYB

Ahmed Mohammed Khalif, aliyekuwa mbunge wa Wajir Magharibi alikuwa mbunge wa pekee kutoka eneo la Kaskazini Mashariki aliyechaguliwa kwa tiketi ya chama cha Rais Mwai Kibaki cha National Rainbow Coalition (NARC).

Katika uchaguzi mkuu wa 2002, eneo hili lilimpigia kura kwa wingi Uhuru Kenyatta aliyekuwa mgombeaji wa chama cha KANU. Mnamo 2003, Kibaki alimteua Khalif waziri wa Leba na Ustawi wa wafanyakazi na kwa kufanya hivyo akawa ameingiza serikalini mmoja wa wapiganiaji mashuhuri wa ukombozi wa pili kutoka eneo la Kaskazini Mashariki.

Khalif alikuwa waziri wa kwanza kutoka kaunti ya Wajir na wa pili kutoka eneo la Kaskazini Mashariki baada ya Hussein Maalim Mohammed aliyetoka kaunti jirani ya Garissa. Akiwa mwanahabari aliyefanyia kazi Shirika la Utangazaji la BBC kabla ya kujiunga na siasa, Khalif alitoka familia ya viongozi.

Baba yake alikuwa mmoja wa maafisa wa polisi wa Waafrika wa cheo cha Inspekta nchini Kenya na baadaye akawa chifu huku kaka yake, Abdirashid Khalif, akiwa katika mkutano wa Lancaster uliotangulia uhuru, akiwakilisha eneo Kaskazini Mashariki lililofahamika kama Northern Frontier District (NFD.

Kaka mwingine wa Khalif, Abdisitar Khalif, ambaye alichukua hatamu za uongozi wa familia kutoka kwake, alikuwa mbunge tangu uhuru na mwiba kwa Mzee Jomo Kenyatta kwa kuungana na Jaramogi Oginga Odinga kwenye vita vyake vya kimaoni na Mzee Kenyatta.

Kabla ya uchaguzi mkuu wa 2002, Khalif alikuwa mwanachama wa vuguvugu la Ufungamano Initiative lililokuwa likipigania mageuzi ya katiba yaliyokuwa yakikataliwa vikali na serikali ya Moi.

Baada ya kuteuliwa waziri 2003 na mchango wake wa miaka mingi kupigania katiba maisha yake yalikatizwa ghafla alipofariki dunia kwenye ajali ya ndege iliyoua marubani wake Busia mnamo Januari 24 2003.

Mawaziri wengine waliokuwa kwenye ndege hiyo — Martha Karua, Raphael Tuju na Jebii Kilimo — walipata majeraha ndege yao ilipogonga nyaya za stima na kuanguka. Mawaziri wengine na maafisa wakuu wa serikali waliokuwa wametumia ndege hiyo kutoka Nairobi walikuwa wameamua kulala Busia. Maafisa hao walikuwa Busia- nyumbani kwa al – iyekuwa waziri wa Masuala ya Nyumbani Moody Awori — kama sehemu ya sherehe za ushindi wa Narc kwenye uchaguzi.

Khalif alikufa muda mfupi baada ya kufikishwa hospitalini akiwa ame – hudumu kama waziri kwa siku 20 pekee na kuwa waziri aliyehudumu kwa muda mfupi sana, sio tu katika serikali ya Kibaki lakini pia katika historia ya Kenya. Waziri msaidizi wa Khalif alikuwa Peter Odoyo, wakati huo akiwa mbunge wa Nyakach. Khalif alirithiwa na mwanawe aliyekuwa na umri wa miaka 23 Mohammed Khalif ambaye aliteuliwa waziri msaidizi.

Khalif alikuwa ameteuliwa waziri wa leba wakati ambao kulikuwa na wito wa kubadilishwa kwa sheria za zamani za leba ambazo Moi alitumia kuwakamata na kuwahangaisha viongozi wa vyama vya kutetea wafanyakazi.

  • Tags

You can share this post!

Bodi ya KPLC yapigwa darubini kuhusu kupotea kwa umeme

Wazo la Raila laweza kuzima mzozo ndani ya Azimio

T L