• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 12:11 PM
Sasa madiwani watishia kumbandua Naibu Gavana wa Trans Nzoia

Sasa madiwani watishia kumbandua Naibu Gavana wa Trans Nzoia

NA EVANS JAOLA

Naibu Gavana wa Trans Nzoia Philomena Kapkory angali anaandamwa na masaibu baada ya Gavana George Natembeya kujisafisha mbele ya Senati na Tume ya Utangamano na Uwiano wa Kitaifa (NCIC) alipoulizwa kuhusu mvutano wao.

Bw Natembeya ambaye uhusiano wake na Naibu Gavana ulidorora mnamo Oktoba, aliambia kamati ya seneti kuhusu ugatuzi kwamba na NCIC kwamba madai ya Bi Kapkory dhidi yake ni harakati kisiasa.

Bw Natembeya alimtaka Bi Kapkory athibitishe madai yake, suala hilo likiongeza mpasuko baina ya wawili hao.

Mnamo wiki jana Gavana Natembeya alijitetea akisema naibu wake alilenga kumchafulia jina.

Madiwani (MCAs) sasa wamempa Bi Kapkory mwezi mmoja amuombe gavana msamaha la sivyo wambandue.

Nao MCAs wengine wanamlaumu Mbunge wa Kiminini Kakai Bisau na Seneta Allan Chesang kwa kufadhili siasa za migawanyiko kudunisha utawala wa Bw Natembeya.

MCAs wakiongozwa na kiongozi wa wachache Erick Wafula, ambaye ni diwani wa Hospital Ward, wametishia kumtimua Bi Kapkory endapo hataomba msamaha.

“Tunamjua anayemfadhili Naibu Gavana kumchafulia jina Gavana Natembeya. Hata tulipoenda Nairobi wakati Gavana akijitetea, tuliona jinsi seneta alivyojaribu kudhalilisha timu yetu. Naye (seneta) ajiandae kutukabili hapa nyumbani,” akasema Bw Wafula.

Bw Wafula na mwenzake wa wadi ya Sikhendu Bw Andrew Kutitila pia wamemuonya mbunge wa Kiminini Bw Bisau dhidi ya kumpangia Bw Natembeya njama mbaya.

Inadaiwa kwamba Bw Bisau anaegemea upande wa chama cha Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetangula cha Ford Kenya ambacho analenga kukitumia akijiandaa kupambana dhidi ya Bw Natembeya katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

Mnamo wiki jana Bw Bisau na mbunge wa Cherangany Patrick Simiyu walitangaza uwanjani Kitale National Polytechnic wakati wa mashindano ya kandanda yaliyofadhiliwa na Seneta Chesang kwamba wanaegemea upande wa Spika Wetang’ula.

Viongozi hao wawili walichaguliwa kwa tiketi ya Democratic Action Party (DAP-K) lakini katika siku za hivi karibuni kinara wa chama hicho, Bw Eugene Wamalwa amekuwa akiwasuta kwa kukosa uaminifu.

Mzozo unaoshuhudiwa Trans-Nzoia ni sawa na ule wa 2017-2022 ambapo aliyekuwa Gavana wa Pokot Magharibi Prof John Lonyangapuo alitekeleza majukumu yake kivyake baada ya kutofautiana na naibu gavana wakati huo Dkt Nicholas Atudonyang ambaye alirudi nchini Amerika kuchapa kazi ya udaktari.

  • Tags

You can share this post!

Watu sita waaga dunia Kikopey baada ya lori kupoteza...

Zuchu aweka ua kulinda ngome ya penzi lake

T L