• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Serikali yawaonya Waluke na Barasa dhidi ya kujiita wanajeshi kwa kampeni

Serikali yawaonya Waluke na Barasa dhidi ya kujiita wanajeshi kwa kampeni

Na WALTER MENYA

TUME ya Maadili na Kukabiliana na Ufisadi (EACC), imewaonya wanasiasa dhidi ya kutumia vyeo vya kijeshi katika kampeni zao ikisema wanaofanya hivyo watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Tume hiyo imewataja wabunge John Waluke wa Sirisia ambaye amekuwa akijitambulisha kama Meja Mstaafu, na Didmus Barasa wa Kimilili ambaye amekuwa akidai ni Kapteni mstaafu wa jeshi kama wanaoweza kushtakiwa kwa kujidai hivyo.

Bw Waluke yuko nje kwa dhamana huku rufaa yake katika kesi ya ulaghai wa Sh297 milioni kupitia sakata ya Bodi ya Taifa ya Mazao na Nafaka (NCPB), ikiendelea kusikilizwa.

EACC inasema kwamba iligundua kuwa wawili hao hawakuwa wa vyeo hivyo walipokuwa wakihudumu kwenye jeshi. Tume hiyo sasa imewaandikia wabunge hao wawili kukoma kutumia vyeo hivyo mara moja.

“Tume imepokea habari kwamba umekuwa ukitumia cheo cha Meja Mstaafu katika shughuli zako rasmi ilhali hujawahi kufikia au kukabidhiwa cheo hicho ulipohudumu katika Jeshi la Ulinzi la Kenya,” inasema barua ya EACC kwa Bw Walukhe.

Bw Barasa pia alipokea barua kama hiyo. Nakala za barua zote mbili zimetumwa kwa Spika wa Bunge la Taifa, Bw Justin Muturi, Karani wa Bunge la Taifa, Michael Sialai na Mkuu wa Majeshi Jemedari Robert Kibochi.

“Ni wazi kuwa hukupata cheo cha Kapteni Mstaafu na kujitambua hivyo kwa umma na katika stakabadhi rasmi kama vile ofisi ya Karani wa Bunge ni ukiukaji wa maadili chini ya kifungu cha sita cha katiba na sharia ya uongozi na Maadili 2012,” inasema barua ya tume kwa Bw Barasa.

Bw Waluke alijiunga na jeshi Aprili 15, 1980 na kuondoka Mei 21, 1994 kwa hiari na akakubaliwa. Wakati wa kustaafu kwake alikuwa na cheo cha Senior Private, ambacho ni cha pili kutoka chini ya hadhi ya Private.

Katika tovuti ya bunge na majukwaa kadhaa, Bw Barasa anajitambulisha kama Kapteni akisema alijiunga na jeshi kuanzia 2001 hadi 2007.

Hata hivyo, rekodi za jeshi zinaonyesha kwamba alihudumu kwa mwaka mmoja na siku 76 katika jeshi kuanzia Oktoba 28, 2007 hadi Februari 26, 2009 alipofutwa kwa makosa ya kukosa kazini na kughushi saini ya mkubwa wake kuchukua mkopo.

Bw Barasa alikanusha kuwa EACC imemwandikia barua akisema tume inaendelea kumnyanyasa na akatishia kuishtaki alipwe fidia.

“Nimekuwa nikisikia suala hilo katika vyombo vya habari. Hawajawasiliana name na nimeagiza wakili wangu kufuatilia fidia,” alisema mbunge huyo.

You can share this post!

KANU yamteua Gedion Moi kuwania urais 2022

Kampuni zatakiwa kuimarisha usiri wa data za wateja