• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 3:46 PM
Sifadhili maandamano ya Azimio – Uhuru

Sifadhili maandamano ya Azimio – Uhuru

ROSELYNE OBALA Na BERNARD MWINZI

RAIS mstaafu Uhuru Kenyatta amekana madai kuwa anafadhili maandamano ya upinzani.

Kwenye mahojiano na nation.africa Jumatatu jijini Nairobi, Bw Kenyatta alisema kuwa ingawa anasalia mwenyekiti wa Baraza Kuu la Azimio la Umoja-One Kenya, hajishughulishi na uendeshaji wa shughuli za kila siku katika muungano huo.

Badala yake, Rais huyo mstaafu alisema anasubiri uongozi wa Azimio kuteua mrithi wake kwa sababu wakati huu amejiondoa katika siasa ili kuendesha michakato ya kuleta amani katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

“Mimi sio mfadhili wa maandamano ya Azimio,” Bw Kenyatta akasema.

“Mbona nifadhili maandamano? Raila Odinga ni kiongozi wa chama changu na nilimuunga mkono katika uchaguzi mkuu wa 2022. Je, nikatize uhusiano wangu naye kwa sababu anaongoza maandamano?” Bw Kenyatta akauliza.

Hata hivyo, alikubali kuwa amefanya mazungumzo na Bw Odinga kuhusu maandamano, lakini alifafanua kuwa mazungumzo yake yalijikita katika masuala ya maadili bali sio ufadhili.

“Ni yeye amefanya uamuzi wa kutetea watu wa Kenya. Siendelei kuchapa siasa, wao ndio hufanya maamuzi.”

Bw Kenyatta alisema Bw Odinga aliitisha maandamano hata nyakati za utawala wake na hata akajiapisha kuwa rais wa wananchi katika uwanja wa Uhuru Park, mita michache kutoka Ikulu.

Alishangaa ni kwa nini utawala wa Kenya Kwanza ukiongozwa na Rais William Ruto na Naibu wake Rigathi Gachagua umeendelea kumshambulia yeye na familia yake.

Rais Ruto, Bw Gachagua, mawaziri kadha na wabunge wa Kenya Kwanza, mara kadha wamedai kuwa Bw Kenyatta ndiye mfadhili wa maandamano yanayoongozwa na Bw Odinga. Kiongozi wa nchi ameapa mara sio moja kumkabili na ‘kumlemaza’ Bw Kenyatta.

Nyakati za mikutano ya Kundi la Wabunge katika Ikulu ya Nairobi na katika mikutano ya hadhara, viongozi wa Kenya Kwanza wameapa kumpa Bw Kenyatta somo ikiwa hatajitenga na Bw Odinga.

Juzi, Rais Ruto aliapa kumsafirisha Bw Kenyatta na Bw Odinga hadi katika jehanamu ya kisiasa ili kukomesha maandamano aliyodai yanayumbisha utendakazi wa serikali yake.

Ingawa hamna kiongozi wa Kenya Kwanza ambaye ametoa ithibati ya kumhusisha Bw Kenyatta moja kwa moja na ufadhili wa maandamano, wanashikilia kuwa maandamano hayo yanafadhiliwa.

Tafsiri: CHARLES WASONGA 

  • Tags

You can share this post!

Uwanja wa shule ya Gatina kukarabatiwa kwa Sh23 milioni

Kenya Kwanza wasema wako tayari kushauriana na Azimio

T L