• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Uwanja wa shule ya Gatina kukarabatiwa kwa Sh23 milioni

Uwanja wa shule ya Gatina kukarabatiwa kwa Sh23 milioni

NA JOHN ASHIHUNDU

UWANJA wa michezo wa Shule ya Msingi ya Gatina katika eneobunge la Dagoretti Kaskazini utafanyiwa ukarabati utakaogharimu Sh23 milioni.

Akitangaza habari hizo Jumapili baada ya kumalizika kwa Mama Dago Super Cup, Mbunge wa eneo hilo, Beatrice Elachi alisema vipaji vingi vimezimwa na ukosefu wa viwanja vya kutosha.

Mwanasiasa huyo aliahidi kushirikiana na Serikali ya Kunti ya Nairobi kuhakikisha ardhi ya umma iliyonyakuliwa katika sehemu hiyo imerejeshwa mara moja.

“Ardhi iliyotengwa na Serikali kusaidia kuimarisha vipaji vya vijana imetwaaliwa na watu binafsi na tutapigana kuhakikisha imerejeshwa,” alisema Elachi.

Mbunge wa Westlands Tim Wanyonyi aliyekuwa mgeni wa heshima wakati wa fainali hizo, alisema soka ndio mchezo unaopendwa zaidi kote duniani, na unapaswa kuheshimiwa.

“Kandanda imefanya wachezaji wengi kuibuka kuwa mabilionea hasa barani Ulaya. Dagoretti na Westlands ni miongoni mwa maeneo yaliyowahi kutoa wanasoka bora kwa miaka mingi ambao walifaulu kujiunga na klabu kubwa pamoja na timu ya taifa, Harambee Stars, na ninawahimiza wachezaji wa sasa watie bidii ili wanufaike kutokana na mchezo huu,” akasema Bw Wanyonyi.

Timu 32 za wanaume zilishiriki katika mashindano hayo, pamoja na nyingine sita za wanawake, ambapo timu ya FIFA Best ikiongozwa na aliyekuwa beki wa kimataifa Wesley Onguso ilitwaa ubingwa wa taji la wanaume baada ya kuchapa Kabiro Youth 3-1.

Diwani wa Gatina Ken Swaka, Mbunge wa Westlands Tim Wanyonyi, na Mbunge wa Dagoretti Kaskazini Beatrice Elachi wakati wa kupeana tuzo kwa washindi wa fainali za Mama Dago Super Cup katika uwanja wa Shule ya Msingi ya Gatina mnamo Julai 23, 2023. PICHA | JOHN ASHIHUNDU

Kikosi hicho kilichojumuisha mastaa kadhaa waliochezea klabu kubwa nchini kilipata Sh100,000 kutoka kwa mdhamini wa mashindano hayo, Elachi, mbali na zawadi nyingi za pesa kutoka kwa viongozi wengine akiwemo Wanyonyi na Gavana wa Nairobi Johnston Sakaja aliyetuma zawadi yake kupitia kwa msimamizi wa Bodi ya Kutoa Leseni ya Pombe eneo hilo, Francis Onyango.

Kabiro walipokea Sh50,000 kwa kumaliza katika nafasi ya pili, wakati Pirates FC na Dago Mixed zikipata Sh30,000 na Sh20,000 kwa kumaliza katika nafasi ya tatu na nne mtawalia.

Hafla ya kuwatuza washindi mbalimbali kwenye fainali ya Mama Dago Super Cup katika uwanja wa Shule ya Msingi ya Gatina mnamo Julai 23, 2023. FIFA Best waliwatandika Kabiro Youth 3-1 kwenye mechu ya fainali. PICHA | JOHN ASHIHUNDU

Mastaa wengine waliokuwa katika kikosi cha FIFA Best ni aliyekuwa mlinzi wa Gor Mahia Wellington Ochieng’, Musa Masika kutoka Wazito FC, John Gago (Ulinzi Stars) na Oliver Maloba wa Nairobi City. FIFA Best walijipatia mabao yao kupitia kwa Kelvin Etemesi aliyefunga mawili dakika za 34 na 82. Bao la tatu lilimiminwa wavuni na Eddie Bala katika dakika ya 87 zikibakia dakika tatu mechi kumalizika.

Kabiro walitangulia kupata bao mapema, dakika ya 14, kupitia kwa Steve Kimari baada ya kutawala mchezo katika kipindi cha kwanza.

FIFA Best waliilaza Dago Mixed 4-2 kwenye nusu-fainali kupitia kwa mikwaju ya penalti, wakati Kabiro wakifuzu baada ya kuandikisha ushindi wa 3-2 dhidi ya Pirates FC pia kupitia kwa mikwaju ya penalti.

Dago Mixed waliibuka mabingwa kwa upande wa timu za wanawake baada ya kuibwaga Joy Love 2-0 kupitia kwa mabao ya Saida Akinyi na Kiki Masika.

Dago walifuzu baada ya kuchapa Mountain Movers 2-1 katika nusu-fainali, huku Joy Love ikiibandua Soccer Queens 4-2 kwenye nusu-fainali nyingine.

  • Tags

You can share this post!

Kocha wa Soccer Assassins atuma onyo kwa Solasa

Sifadhili maandamano ya Azimio – Uhuru

T L