• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 4:42 PM
Sifuna asema Rais Kenyatta hahitaji kuunganisha vinara wa Nasa

Sifuna asema Rais Kenyatta hahitaji kuunganisha vinara wa Nasa

Na CHARLES WASONGA

KATIBU mkuu wa chama cha ODM Edwin Sifuna amesema muungano wa upinzani, Nasa, hauhitaji usaidizi wa Rais Uhuru Kenyatta ili waungane.

Huku akionekana kumjibu Naibu Rais William Ruto aliyedai Jumapili kwamba vigogo wa Nasa wanamsumbua rais wakimwomba awaunganishe, Bw Sifuna hata hivyo alisema wajibu wa Rais ni kuunganisha taifa lote.

“Ni wazi kuwa hamna kigogo yeyote katika Nasa ambaye amewasilisha ombi kwa rais akitaka awaunganishe. Hatujamwomba aingilie kati mivutano miongoni mwetu.”

“Lakini Rais ana wajibu wa kikatiba wa kupalilia umoja wa kitaifa na mshikamano miongoni mwa viongozi wa kitaifa. Hii ndio maana aliridhiana na kiongozi wetu Raila Odinga, kupitia handisheki,” Bw Sifuna akaeleza.

Alisema haya Jumanne usiku kwenye mahojiano katika runinga ya Citizen TV.

Mnamo Jumapili, Dkt Ruto akiongea baada ya kuhudhuria ibada katika kanisa moja mjini Kiambu, awataka vinara wa Nasa kukoma kumwingiza Rais Kenyatta katika tofauti zao.

“Waache Rais Kenyatta afanya kazi yake ya kuongoza taifa. Wakome kumvuta katika tofauti zao kwa sababu wameshindwa kujipanga. Sisi tumejipanga na kunasubiri kukabiliana nao,” akaeleza.

Seneta wa Kakamega Cleophas Malala ambaye pia alihojiwa katika kipindi hicho cha runinga alitofautiana na Bw Sifuna na kukariri kuwa Nasa ilikufa na haiwezi kufufuliwa tena.

Seneta huyo wa chama cha Amani National Congress (ANC), alisema kuwa muungano huo ulisambaratishwa na kiongozi wa ODM Raila Odinga.

“Muda wetu wa kuhudumu kama Nasa ulikuwa ni kati ya miaka ya 2017 na 2022. Tulisambaratika kutokana na kutoaminiana, ukosefu wa nidhamu miongoni mwa wanachama na usaliti kutoka kwa wenzetu wa ODM,” Malala akasema.

Seneta huyo wa Kakamega alisema Bw Odinga aliamua kuchukua mazuri yote ambayo yalitokana na handisheki, hatua ambayo inakwenda kinyume na moyo wa muungano wa “kugawana manufaa yote yatakayopatikana.”

“Katika kipengele cha 13 (2b), ni wazi kwamba fedha kutoka Hazina ya Vyama vya Kisiasa (PPF) zitagawanywa kwa njia sawa. Lakini ODM iliamua kuchukua kila kitu, na kukataa kutuma fedha zozote kwa vyama vingine washirika,” akasema Bw Malala.

Ni mivutano kama hii iliyomfanya Dkt Ruto kuwataka vinara wa upinzani kukoma kumsumbua rais.

“Rais hakuchaguliwa kuwatumikia watu watano au sita. Rais huwahudumia Wakenya 47 milioni, sio viongozi wa upinzani ambao hawawezi kusikilizana kwa chochote,” akasema.

Dkt Ruto pia alidai kuwa viongozi wa upinzani wanamsukuma Rais Kenyatta kuongoza juhudi za mageuzi ya Katiba ili kuleta mfumo wa uongozi utakaotoa nafasi kwao.

“Sasa huo mpango unapoonekana kugonga mwamba, wanataka Rais awaunganishe. Mmoja wao anasema bado ana risasi, mwingine anasema hawezi kufanya kazi na mtu fulani huku mwingine akitaka pesa kutoka hazina ya vyama vya kisiasa,” Dkt Ruto akawaambia waumini.

You can share this post!

KINA CHA FIKIRA: Wazazi watie bidii kuwalinda watoto wao...

Kiambaa kuamua mwelekeo wa Nyoro kisiasa – Wadadisi