• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 6:50 AM
Sijateka wakaguzi nyara, asema Ole Lenku

Sijateka wakaguzi nyara, asema Ole Lenku

Na PETER MBURU

KAMATI ya Seneti Kuhusu Uwekezaji na Matumizi ya Pesa za Kaunti (CPAIC) Jumanne ililazimika kusitisha kikao na maafisa wa serikali ya Kaunti ya Kajiado, baada ya maafisa wa ukaguzi kutoka afisi ya Dkt Edward Ouko kukosa kufika.

Maafisa kutoka afisi ya Mkaguzi Mkuu ambao walifanya ukaguzi kuhusu jinsi serikali ya Kaunti ya Kajiado ilitumia pesa walikosa kufika mbele ya kamati hiyo jana, huku juhudi za kuwatafuta zikifeli.

Ni maafisa hao ambao walitarajiwa kuelezea kamati jinsi kaunti hiyo ilitumia pesa, wakiwa kama mashahidi wa kushtaki.

Wakati wa kikao hicho, afisa wa kuhakikisha kuna mawasiliano baina ya Seneti na afisi ya Dkt Ouko Akaka Ramweya alisema alijaribu kuwatafuta kwa simu, lakini hawakuwa wakipatikana.

Karani wa kamati hiyo naye alitoa madai ya kushangaza, aliposema kuwa Katibu wa kaunti hiyo alikuwa amempigia simu na kumfahamisha kuwa maafisa hao wa ukaguzi hawangefika, hivyo akimtaka kuahirisha kikao hicho cha jana.

Katibu huyo, hata hivyo, alikana kufanya hivyo, akisema mawasiliano yake na Seneti yalikuwa kupitia barua ambayo kaunti iliandikia Bunge pekee, ikiomba muda zaidi kabla ya kufika mbele yake, kwa kuwa Gavana Joseph Ole Lenku alikuwa nje ya nchi.

“Sijazungumza chochote kuhusu maafisa hao, hata sina namba zao. Nilichofanya ni kuandikia Bunge kuomba muda zaidi kwa kuwa gavana alikuwa nje ya nchi,” akasema katibu huyo.

Gavana Lenku, ambaye alikuwa mbele ya kamati hiyo alijiepusha kuhusiana na kukosekana kwa maafisa hao, akipinga madai ya kamati hiyo, ya kutaka kumhusisha na kukosekana kwao.

“Hatuwezi kuhusishwa na kukosekana kwa maafisa hao, tumekuja kujiwakilisha kama serikali ya kaunti. Sio sisi tunafaa kueleza walipo. Mimi sikuhudumu enzi za KANU wakati watu walikuwa wakitekwa nyara,” Bw Lenku akasema, baada ya seta wa Kiambu kutaka kujua ikiwa huenda alihusika na kukosekana kwao.

“Katibu wa Kaunti aliandikia Bunge rasmi nilipokuwa nje ya nchi akitaka tupewe muda, hatujakuwa na mawasiliano yoyote yasiyo rasmi na maafisa wa afisi hiyo,” akasema gavana huyo.

Lakini maseneta walikuwa wakilemea afisi ya Mkaguzi Mkuu kwa kukosa kutoa mawasiliano mapema, na serikali ya kaunti kutokana na madai hayo.

“Tunahitaji maafisa waliofanya huu ukaguzi kuelekeza kamati kwa masuala ambayo tunauliza. Hatujawahi kuona hivi, wakaguzi ni mashahidi,” seneta wa Narok Ledama Ole Kina akasema.

Seneta maalum, Mary Seneta naye alishuku kuwa kukosa kufika kwa maafisa hao ni njama, ili wapate muda zaidi wa kujipanga watakavyosema mbele ya kamati.

Kutokana na kukosekana kwao, mwenyekiti wa kamati Moses Kajwang alifunga kikao na kuamrisha maafisa hao waitwe kwa lazima, naye Mkaguzi Mkuu Edward Ouko awaadhibu ikiwa hawana sababu tosha kuhusu kukosekana kwao.

“Tuombe kuwe na sababu ya kutosha kwa mkaguzi kukosa kufika mbele ya kamati. Ikiwa hawataeleza ni kwanini hawakuja, tutachukua hatua za kisheria. Tutamtaka Edward Ouko kuwachukulia hatua vilevile,” akasema Bw Kajwang, ambaye pia ni seneta wa Homa Bay.

“Haifai kuendelea na kikao bila uwepo wa maafisa waliofanya ukaguzi,” akasema, akiamrisha kikao hicho kiandaliwe tena Jumatatu wiki ijayo.

  • Tags

You can share this post!

Ingwe wasajili mnyakaji wa UG Ochan

NLC na KR lawamani kukosa kufidia wakazi Sh5.8b

adminleo