• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 1:01 PM
‘Simba’ wa Kisii kukumbukwa kwa kunguruma

‘Simba’ wa Kisii kukumbukwa kwa kunguruma

CHARLES WASONGA na NYAMBEGA GISESA

ALIYEKUWA ‘simba’ wa siasa za eneo la Kisii, Simeon Nyachae, ambaye aliaga dunia jana atakumbukwa kama mwanasiasa na afisa wa utawala aliyedhihirisha sifa ya kipekee ya ujasiri katika enzi ya tawala za marais Jomo Kenyatta, Daniel Moi na Mwai Kibaki.

Hadi kifo chake jana, marehemu Nyachae alikuwa msemaji wa jamii ya Abagusii katika nyanja za utawala na siasa kuanzia miaka ya sabini hadi 2007 alipopoteza kiti cha ubunge cha Nyaribari Chache kwa Dkt Robert Monda.

Katika maisha yake kama afisa wa utawala wakati wa enzi ya Mzee Kenyatta, Bw Nyachae alidhihirisha ujasiri mnamo 1975 aliposoma hotuba ya rais wakati wa mazishi ya aliyekuwa Mbunge wa Nyandarua Kaskazini J.M Kariuki katika mazingira ya taharuki. Hii ni kwa sababu Mzee Kenyatta alilaumiwa kwa kifo cha mwanasiasa huyo aliyekuwa maarufu kote nchini.

Katika utawala wa Mzee Moi, Bw Nyachae alihudumu kama mkuu wa mikoa ya Kati na Rift Valley, wakati ambao alijidhihirisha kuwa afisa mwenye ushawishi mkubwa hadi akapandishwa cheo kuwa Katiba wa Ushirikishi wa Maendeleo ya Kitaifa.

Baadaye alipanda ngazi na kuwa katibu mkuu wa serikali, cheo kilichokuwa na ushawishi mkubwa zaidi serikalini tangu uhuru.

Wandani wa Mzee Moi waliingiwa na hofu kuwa wadhifa huo ulimfanya Bw Nyachae kuwa na usemi mkubwa zaidi hata kuzidi mawaziri, kiasi kwamba alikuwa akirejelewa kama ‘Waziri Mkuu’.

Mzee Moi alishusha hadhi ya cheo hicho kuwa Mkuu wa Utumishi wa Umma na Katibu katika Baraza la Mawaziri hadi Bw Nyachae alipostaafu mnamo 1987 alipotimu umri wa miaka 55.

Alijishughulisha na biashara zake hadi 1992 Mzee Moi alipomshawishi kuwania kiti cha ubunge cha Nyaribari Chache kwa tiketi ya KANU baada ya jaribio lake la kwanza, mnamo 1988 kugonga mwamba.

Baada ya kushinda kiti cha ubunge, Rais Moi alimteua Nyachae kuwa Waziri wa Kilimo na baadaye akamtunukia hadhi ya Waziri wa Fedha.

Lakini mnamo 1998, ujasiri na ukakamavu wa Bw Nyachae ulimtumbukiza katika shida, alipotangaza kuwa serikali ilikuwa imefilisika. Mataifa fadhili yalikuwa yamekatiza misaada kwa Kenya kwa kile yalichodai ni hatua ya Mzee Moi kuhujumu utawala wa kidemokrasia nchini.

Mzee Moi alikasirishwa na kauli hiyo na akamhamisha hadi katika Wizara ya Ustawi wa Viwanda. Bw Nyachae alichukulia hatua hiyo kama kushushwa cheo na akajiuzulu mara moja kwa hasira, kitendo ambacho kilikuwa nadra kutokea katika utawala wa Mzee Moi.

Bw Nyachae pia alihudumu katika utawala serikali ya umoja wa taifa chini ya rais mstaafu Kibaki.

Nyachae pia aliwahi kudhihirisha hulka zake za hasira bungeni alipopiga meza kwa kutumia kiatu chake baada ya aliyekuwa Mbunge wa Nyakach, Ojwang’ K’Ombudo kumhusisha na kutoweka kwa mfanyabiashara na mwanasiasa Jared Kagwana.

Bw Nyachae pia aliwahi kutofautiana na alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Nyanza, Joseph Kaguthi hali iliyopelekea Mzee Moi kumhamisha afisa huyo hadi Nairobi.

Nyachae pia angepambana na mahasidi wake wa kisiasa kwa ujasiri kwani inakumbukwa kuwa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2007, Naibu Rais William Ruto wakati huo alishambuliwa na wahuni katika eneo la Nyamarambe Kisii, walioaminika kupata maagizo kutoka kwa kigogo huyo.

Ingawa alikana madai hayo, Bw Nyachae alinukuliwa akisema hivi: “Sina habari kuhusu hilo lakini ukicheza hatuwezi kuketi tukitazama ukiwaharibu watu wetu.”

Dkt Ruto alikuwa ameenda Kisii kumfanyia kampeni Raila Odinga waliyekosana na Bw Nyachae mnamo 2002 alipompendekeza Mzee Kibaki kuwa mgombea urais wa NARC kupitia kauli, “Kibaki Tosha”.

Biashara

Marehemu pia alikuwa mfanyabiashara shupavu ambaye aliwekeza katika sekta kadha kama vile kilimo, benki, ujenzi wa nyumba, uchukuzi na utengenezaji bidhaa jijini Nairobi na sehemu mbalimbali nchini.

Kwa mfano, Bw Nyachae ndiye mwasisi wa kundi la kampuni ya Sansora inayoendesha biashara ya usagaji nafaka kupitia kampuni ya Kabansora Millers.

Katika sekta ya benki, Bw Nyachae ni miongoni mwa wenyehisa katika National Commercial Bank of Africa (NCBA) pamoja na familia ya Kenyatta, Naushad Merali na aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu Nchini (CBK) Philip Ndegwa.

Marehemu Nyachae alikuwa na wake watano na watoto 20 akiwemo aliyekuwa Mwenyekiti wa iliyokuwa Kamati ya Utekelezaji wa Katiba (CIC), Charles Nyachae.

You can share this post!

Homeboyz wakiri ni pigo kwao kupoteza wanaraga wanne

Joho ashauriwa kuhusu urais 2022