• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 3:58 PM
Sonko anahatarisha kura Mombasa – IEBC

Sonko anahatarisha kura Mombasa – IEBC

WINNIE ATIENO NA VALENTINE OBARA

MUDA wa kuhudumu wa Gavana wa Mombasa, Hassan Joho, huenda ukaongezeka kufuatia mgogoro kuhusu iwapo aliyekuwa gavana wa Nairobi, Mike Sonko, anastahili kushindania urithi wa kiti hicho Agosti 9.

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Wafula Chebukati, Jumanne alisema kuna uwezekano wa uchaguzi wa ugavana kuahirishwa Mombasa iwapo Bw Sonko atathibitishia tume hiyo kwamba bado amekata rufaa dhidi ya kubanduliwa kwake mamlakani.

Mnamo Jumatatu, IEBC ilifutilia mbali uteuzi wa Bw Sonko kuwania kiti chochote cha kisiasa nchini baada ya Mahakama ya Juu kutupa nje rufaa yake wiki iliyopita.

Bw Sonko alikimbilia katika Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ) huku pia akiwasilisha ombi katika Mahakama ya Juu kutaka uamuzi uliotolewa uangaliwe upya.

Bw Chebukati akizungumza Nairobi jana Jumanne alisema tume bado haikuwa imepokea thibitisho lolote kuwa Bw Sonko amekata rufaa tena.

Kulingana naye, kesi hizo zinahatarisha kucheleweshwa kwa maandalizi ya uchaguzi na hivyo basi huenda ikalazimu IEBC kuahirisha uchaguzi huo.

“Kila raia ana haki ya kupigania haki yake. Huenda itatubidi tuahirishe uchaguzi wa ugavana katika Kaunti ya Mombasa. Tukisukumwa mahala ambapo hatutaweza kufanya uchaguzi wa ugavana Mombasa, itatubidi kuandaa kinyang’anyiro hicho baada ya Uchaguzi Mkuu,” alisema Bw Chebukati.

Wikendi, Bw Joho alitilia mkazo suala la kuwa bado yuko mamlakani hadi wakati atakapompisha gavana mpya atakayechaguliwa ambaye, kulingana naye, atakuwa ni Mbunge wa Mvita, Bw Abdulswamad Nassir.

Hali hii huenda ikaibua mtafaruku wa kisheria kuhusu iwapo Bw Joho anastahili kuendelea kushikilia afisi hiyo kwani wataalamu wa sheria huwa na mitazamo tofauti kuhusu ufasiri wa Katiba.

Kwa mujibu wa sehemu 182 (6) ya Katiba, gavana aliye mamlakani anafaa kuendelea kuhudumu hadi wakati gavana mwingine atakapoapishwa.

“Mtu anayeshikilia afisi ya gavana wa kaunti chini ya kifungu hiki cha Katiba, isipokuwa kama atabanduliwa kutoka afisini, atashikilia afisi hadi gavana mpya wa kaunti atakayechaguliwa ataingia afisini baada ya uchaguzi ufuatao utakaofanywa kwa msingi wa Kifungu 180 (1),” Katiba inaeleza.

Hata hivyo, Kifungu 180 (1) cha Katiba kinahitaji kuwa, gavana atachaguliwa siku ile ile ya Uchaguzi Mkuu wa Wabunge, ambayo ni Jumanne ya pili ya Agosti, kila mwaka wa tano.

Mbali na kutatiza uongozi wa Mombasa, wadadisi wa kisiasa wanaonya kuwa, kuahirishwa kwa uchaguzi wa ugavana huenda kukaathiri pia idadi ya wapigakura watakaojitokeza uchaguzini.

katika kaunti hiyo na hivyo kuathiri idadi ya kura za urais.

Eneo hilo ni mojawapo ya yale yanayotegemewa sana na mgombeaji urais wa Chama cha Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya, Bw Raila Odinga, na mpinzani wake wa karibu, Naibu Rais William Ruto, wa Chama cha UDA, kujitafutia ushindi.

Bw Sonko ambaye alikuwa Gavana wa Nairobi kabla ya kubanduliwa kwa shutma za ufisadi na utumizi mbaya wa mamlaka alikuwa ameidhinishwa na IEBC kuwania ugavana Mombasa kufuatia uamuzi wa majaji watatu wa Mahakama Kuu Jumatano wiki iliyopita waliosema rufaa yake ilikuwa haijaamuliwa na Mahakama ya Juu.

Majaji Olga Sewe, Ann Ong’injo’ na Stephen Githinji walimwamuru afisa msimamizi wa uchaguzi kaunti ya Mombasa Bi Swalhah Yusuf amwidhinishe Bw Sonko.

Lakini furaha ya Bw Sonko haikudumu muda mrefu kwani Mahakama ya Juu baadaye ilitoa uamuzi wa rufaa hiyo na kuamua alikuwa amebanduliwa kwa njia halali.

  • Tags

You can share this post!

Ashtakiwa kwa kuiba taa ya gari katika kituo cha polisi

Kusema ‘hatupangwingwi’ si uchochezi –...

T L