• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 2:49 PM
Spika atangaza nia ya kumrithi Gavana Mutua

Spika atangaza nia ya kumrithi Gavana Mutua

Na PIUS MAUNDU

SPIKA wa Bunge la Kaunti ya Machakos, Florence Mwangangi ametangaza nia ya kumrithi Gavana Alfred Mutua kwa kuwania wadhifa huo kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Hatua hii imefikisha sita, idadi ya wanasiasa ambao wanamezea mate kiti hicho kufikia sasa, na kukipa chama cha Wiper kibarua kigumu katika kuteua mgombeaji wa kupeperusha bendera yake katika kinyang’anyiro hicho.

Bi Mwangangi alisema amepata uzoefu mkubwa kuongoza kaunti hiyo katika muda ambapo amehudumu kama Spika wa Bunge hilo.

“Kufikia wakati huu, ninaelewa changamoto zote zinazowakabili watu wa Machakos, kuanzia ngazi ya mashinani. Vile vile, najua jinsi pesa za umma zinapaswa kutumiwa kwa sababu bunge la kaunti ndilo hupitisha bajeti na kuiwasilisha kwa gavana ili aitekeleze,” akasema Ijumaa.

Alikuwa akiongea wakati wa mazishi ya Mama Lucia Kitili, mamaka Alex Kitili, ambaye ni mwanachama wa Bodi ya Huduma za Bunge la Kaunti ya Machakos, katika kijiji cha Yamalwa, eneo la Mwala.Gavana Mutua, ambaye ni kiongozi wa chama cha Maendeleo Chap Chap (MCC), anahudumu kipindi cha pili na cha mwisho kwani Katiba haimruhusu kuwania muhula wa tatu.

Bi Mwangangi, ambaye ni mamake Waziri Msaidizi wa Afya Mercy Mwangangi, ni wakili mwenye tajriba kubwa na mfanyabiashara. Vile vile, yeye ni mwandani wa karibu wa kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka.

Ingawa haijulikani ni chama kipi Bi Mwangangi atatumia kuwania kiti hicho, tangazo lake limezua tumbojoto miongoni mwa wafuasi wa Waziri Msaidizi wa Uchukuzi Wavinja Ndeti na Mbunge wa Mavoko Patrick Makau.

Wawili hao ambao ni wandani wa Bw Musyoka pia wametangaza nia ya kuwania kiti ugavana wa Machakos.

You can share this post!

Majonzi watoto 60 waliokufa kwenye shambulio wakizikwa

Waomba serikali isiruhusu uuzaji wa nyama ya punda