• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
UDA yaanza mikakati ya kutetea urais 2027

UDA yaanza mikakati ya kutetea urais 2027

Rais Ruto ameagiza viongozi wa kitaifa wa chama hicho tawala kufanya uchaguzi wa viongozi katika ngazi za mashinani kote nchini.

Viongozi wa sasa wa UDA hawakuchaguliwa bali waliteuliwa kushikilia nyadhifa hizo kwa muda.

Chama cha UDA kilichoundwa 2020, kiliahirisha mara nne mpango wa kutaka kuandaa uchaguzi wa viongozi wake kabla ya uchaguzi wa Agosti 9.

Tovuti ya UDA inaonyesha kuwa chama hicho kina wanachama 6.9 milioni.

Mwenyekiti wa UDA Johnson Muthama, jana Jumanne aliambia Taifa Leo kuwa Rais Ruto ameagiza viongozi wa chama kuandaa uchaguzi kati ya Januari na Februari 2023.

Bw Muthama alisema kuwa uchaguzi huo ni njia mojawapo ya kuhakikisha kuwa chama kinakuwa imara na maarufu kabla ya uchaguzi wa 2027.

“Kiongozi wa chama ameniagiza kuandaa uchaguzi wa viongozi wa chama katika ngazi za mashinani haraka iwezekanavyo. Hiyo inamaanisha kuwa uchaguzi huo utafanyika mwanzoni mwa 2023,” alisema Bw Muthama.

Kulingana na seneta huyo wa zamani wa Machakos, wanachama wote wa UDA, wakiwemo viongozi waliochaguliwa, wako huru kuwania nyadhifa mbalimbali za chama hicho.

Alisema kuwa atatetea wadhifa wake iwapo chama kitamsihi kuwania.

“Niko tayari kujiuzulu kutoka wadhifa wa mwenyekiti iwapo nitapewa wadhifa serikalini,” akasema.

Bw Javas Bigambo, mdadisi wa masuala ya kisiasa, anasema kuwa viongozi wa UDA walihofia kuibua mgawanyiko chamani kwa kuandaa uchaguzi wa viongozi wa chama kabla ya uchaguzi wa Agosti 9.

“Vyama vya kisiasa vinaogopa kufanya uchaguzi wa viongozi wa mashinani miezi michache kabla ya uchaguzi mkuu. Hii inatokana na hofu kwamba uchaguzi unaweza kuzua mgawanyiko ambao unaweza kukosesha chama ushindi,” akasema.

Profesa Egara Kabaji, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Masinde Muliro, anasema kuwa uchaguzi wa viongozi wa chama unapofanywa karibu na uchaguzi mkuu unaweza kuwa hatari.

“Kuna hatari ya watu ambao hawajaridhishwa na mchakato wa uchaguzi kuhamia vyama vingine hivyo kulemaza chama,” akasema.

Bw Muthama alisema kuwa uchaguzi ujao utafanywa kupitia kura za siri.

Alifichua kuwa juhudi za kushawishi viongozi wa vyama tanzu vya muungano wa Kenya Kwanza kuvunja vyama vyao na kujiunga na UDA, zinaendelea.

“Hata hivyo, hatutalazimisha chama chochote kuvunjwa japo ni muhimu kuwezesha chama cha UDA kuwa kikubwa na imara,” akasema.

  • Tags

You can share this post!

Muhoozi apigwa marufuku kutoa maoni kuhusu masuala ya...

Faida anazozipata mtu kwa kula tanipu

T L