• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 2:59 PM
Muhoozi apigwa marufuku kutoa maoni kuhusu masuala ya serikali kwenye Twitter

Muhoozi apigwa marufuku kutoa maoni kuhusu masuala ya serikali kwenye Twitter

NA MASHIRIKA

KAMPALA, UGANDA

MWANAWE RAIS wa Uganda, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, amepigwa marufuku kutoa maoni kuhusu masuala ya serikali katika mtandao wa kijamii ya Twitter.

Rais wa Uganda, Yoweri Museveni alitoa amri hiyo siku ya Jumatatu.

Amri hiyo inakuja wiki chache baada ya jenerali huyo kuzua mjadala mkali nchini Kenya baada ya kutishia kuvamia jiji la Nairobi kwenye mtandao wake wa kijamii ya Twitter.

Jenerali Kainerugaba, 48, mara nyingi amezua utata na maoni yake kwenye Twitter lakini ghasia zake zisizo za kidiplomasia mapema mwezi huu zilisababisha Museveni kuingilia kati.

“Jenerali huyo amepigwa marufuku kutoa maoni kuhusu masuala ya serikali. Sisemi kuwa hafai kuzungumza kwenye mtandao wa Twitter ila tatizo ni yale anayoandika kwenye mtandao huo wa kijamii,” akasema Rais Museveni.

Hata hivyo, alisema kuwa jenerali Kainerugaba, bado ataweza kuingia kwenye mitandao ya kijamii mradi tu ajizuie kutoa maoni kuhusu masuala ya serikali.

“Ataendelea kutumia mitandao ya kijamii mradi tu azingatie maoni yake. Asitoe maoni yanayoweza kuleta vurugu na kudorora uhusiano kati ya nchi yetu na nchi jirani,” akasema Rais Museveni.

“Kuzungumza kuhusu nchi nyingine na siasa za upendeleo za Uganda ni jambo ambalo hapaswi kufanya na hatalifanya,” akaongeza Rais Museveni.

Kufuatia matamshi hayo ya jenerali huyo, Rais Museveni alilazimika kuingilia kati na kuomba msamaha baada ya Kainerugaba, kuandika kuwa jeshi lake litateka Nairobi.

Kwenye mtandao huo wa kijamii, jenerali huyo pia alimkashifu rais wa zamani wa Kenya, Uhuru Kenyatta, kwa kutojaribu kuwania kiti cha urais kwa mara ya tatu kinyume na katiba ya Kenya.

Jenerali huyo ambaye ndiye kifungua mimba wa rais Museveni wiki jana pia alijinyenyekeza na kumuomba msamaha Rais William Ruto.

Katika mahojiano ya Jumatatu, Museveni hata hivyo alimtetea mwanawe na kumtaja kama jenerali mzuri baada ya kumpandisha cheo licha ya kumvua nafasi yake kama kiongozi wa majeshi ya nchi kavu ya Uganda.

Ingawa Kainerugaba amekanusha mara kwa mara madai kwamba ana nia ya kumrithi baba yake mwenye umri wa miaka 78, amefurahia jinsi alivyopanda ngazi kisiasa nchini Uganda.

  • Tags

You can share this post!

Wanyama kuondoka Montreal mwezi Novemba

UDA yaanza mikakati ya kutetea urais 2027

T L