• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Ufisadi: Karua atia ahadi yake doa kuu

Ufisadi: Karua atia ahadi yake doa kuu

NA WANDERI KAMAU

MGOMBEA mwenza wa urais wa muungano wa Azimio, Bi Martha Karua ameonekana kuteleza kuhusu ahadi zake za kukabiliana na ufisadi iwapo watashinda Agosti 9.

Hii ni kufuatia hatua ya Bi Karua pamoja na kinara wake, Raila Odinga kumkumbatia aliyekuwa gavana wa Nairobi, Mike Sonko ndani ya Azimio kuwania ugavana wa Mombasa, licha ya kesi za ufisadi zinazomkabili pamoja na kuwa alibanduliwa Nairobi 2020 kwa madai ya ufisadi.

Wadadisi wa siasa wanasema hatua ya Bi Karua pamoja na Bw Odinga kumkaribisha Bw Sonko katika Azimio inahujumu uwezo wao kupiga vita ufisadi wakishinda.

Bi Karua amekuwa akiapa kuwa hatasita kuwachukulia hatua kali washukiwa wa ufisadi, kauli ambayo imekuwa pia ikiendelezwa na wakuu wengine wa Azimio akiwemo Rais Uhuru Kenyatta na Bw Odinga.

Kulingana na mdadisi wa siasa Wycliffe Muga, hatua ya Bi Karua kumkumbatia Bw Sonko inatia doa hakikisho na ahadi ambazo amekuwa akitoa kuhusu kukabiliana na wafisadi.

“Hata ikiwa Bw Sonko ataibuka mshindi Mombasa, hilo halitaondoa doa la uadilifu wake kama kiongozi kutokana na kesi ambazo zimekuwa zikimkabili. Kama kiongozi ambaye amekuwa mstari wa mbele kukabiliana na ufisadi, ingetarajiwa Bw Sonko ni miongoni mwa wanasiasa ambao Bi Karua angeepuka kutangamana nao,” akasema Bw Muga.

Kinaya ni kuwa Bi Karua amekuwa akiwarai Wakenya kutowachagua washukiwa wa wafisadi.

Mdadisi wa siasa Dismus Mokua anasema kuwa lengo kuu la kujumuishwa kwa Bw Sonko kwenye kampeni za Azimio ni kuimarisha umaarufu wa Bw Odinga na wagombeaji wengine wa muungano huo.

“Licha ya kung’olewa mamlakani kama gavana, Bw Sonko bado ni maarufu sana miongoni mwa wakazi wa Nairobi. Hilo ndilo lilimfanya kuwekwa kwenye msafara wa kampeni wa Azimio jijini Nairobi. Uwepo wake utakuwa muhimu kupiga jeki kampeni za Azimio,” asema Bw Mokua.

Kukubaliwa kwa Bw Sonko kuwa debeni kunaongeza wasiwasi mkubwa wa idadi kubwa ya viongozi watakaochaguliwa kuwa na mienendo ya kutiliwa shaka.

Mbali na Bw Sonko baadhi ya washukiwa wengine wanaoweza kuwa serikalini ni John Waluke, ambaye rufaa yake dhidi ya kifungo cha miaka 34 kwa wizi wa Sh297 m.22ilioni iko kortini, na sasa anatetea ubunge wa Sirisia kwa tiketi ya chama cha Rais Kenyatta cha Jubilee.

Mwaniaji urais mwenza wa Dkt Ruto, Rigathi Gachagua kwa upande wake anakabiliwa na kesi ya ufisadi.

Bi Aisha Jumwa, ambaye anakabiliwa na kesi ya wizi wa Sh19 milioni za eneobunge la Malindi pamoja na nyingine ya mauaji ya Gumbao Jola mnamo 2019 naye anataka kuwa gavana wa Kilifi kwa chama cha United Democratic Alliance (UDA) chake Dkt Ruto.

Katika Kaunti ya Meru, Mithika Linturi, ambaye pia anasaka ugavana kwa UDA anakabiliwa na kesi za ulaghai wa Sh530 milioni, madai ya kujaribu kubaka na nyingine kuhusu stakabadhi ghushi za elimu.

Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi naye anatetea kiti chake kwa chama cha UDA akiwa na kesi ya uchochezi na ughushi wa vyeti vyake vya elimu.

Mwingine ni Evans Kidero, ambaye sasa anataka kuwa gavana wa Homa Bay licha ya kuwa na kesi ya ufujaji wa Sh204 milioni alipokuwa gavana wa Nairobi.

Wadadisi wanaonya kuwa washukiwa hawa na wengine wakishinda viti wanavyowania watafifisha uwezo wa serikali itakayochaguliwa kupiga vita ufisadi ambao umekolea nchini.

Hali ya kuwepo kwa washukiwa debeni imewezeshwa na mfumo duni wa kuwapiga msasa wagombeaji pamoja na mahakama kuwapitisha hata wale ambao Tume ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imewakataa, kama ilivyofanyika kwa Bw Sonko.

Kulingana na Mkurugenzi wa Masuala ya Sheria katika IEBC, Chrispine Owiye, udhaifu huo umetokana matukio ya awali ikiwemo Rais Kenyatta na Naibu Rais William Ruto kuruhusiwa kuwania urais mnao 2013 licha ya kukabiliwa na kesi ya uhalifu katika Mahakama ya Kimataifa ya ICC.

Juhudi za mwanaharakati Okiya Omtatah kutaka korti kuzima wote wanaokabiliwa na kesi ziligonga mwamba, hivyo kufungua mwanya mwa washukiwa kuwa debeni Agosti 9.

Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji naye amechangia hali hii kwa kusimamisha uendeshaji wa kesi za ufisadi dhidi ya wanasiasa hadi baada ya uchaguzi.

You can share this post!

Masonko Saudia wamezea Ronaldo

Faida za kiafya kunywa chai ya chamomile

T L