• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Ugavana Bonde la Ufa wanyima Ruto usingizi

Ugavana Bonde la Ufa wanyima Ruto usingizi

NA ONYANGO K’ONYANGO

NAIBU wa Rais William Ruto amejipata njiapanda huku wandani wake wanaomezea mate ugavana katika eneo la Bonde la Ufa wakimenyana kusaka tiketi ya chama cha United Democratic Alliance (UDA).

Bodi ya Uchaguzi ya UDA inatarajiwa kuandaa kura za mchujo Aprili 14 kote nchini. Kaunti zilizo na ushindani mkali ni Uasin Gishu, Nandi, Elgeyo Marakwet, Kericho na Bomet.

Dkt Ruto amejipata njiapanda kuhusu ikiwa anafaa kuingilia kati au la. Kujitenga kwake kutamaanisha kuwa huenda baadhi ya wandani wake wakapoteza.

Katika Kaunti ya Uasin Gishu, wawaniaji sita wa UDA wamejitokeza kutaka kurithi Gavana Jackson Mandago.

Wanajumuisha mwanasiasa Jonathan Bii (au Koti Moja), mbunge wa Soy Caleb Kositany, mabalozi Sarah Serem (China) Julius Bitok (Pakistan), aliyekuwa waziri wa Mazingira wa Kaunti ya Nairobi, Vesca Kangogo na diwani wa Ngenyilel David Sing’oei.

Bw Kositany na Prof Bitok wanaonekana kuwa wandani wa Dkt Ruto.

Bw Bii anaamini kuwa ana nafasi bora ya kushinda kura za mchujo wiki ijayo.

“Ninaamini kura za mchujo zitakuwa huru na haki licha ya kuwepo kwa ushindani mkali. Vilevile, nina matumaini nitaibuka mshindi,” akasema Prof Bitok.

Katika Kaunti ya Nandi, Gavana wa sasa, Bw Stephen Sang anaonekana kuwa karibu na Dkt Ruto. Gavana wa zamani Cleophas Lagat ameshirikiana na Spika wa Bunge la Kaunti ya Nandi, Joshua Kiptoo na kuunda vuguvugu linalojulikana kama ‘Nandi Kwanza Alliance’ katika juhudi za kumng’oa Bw Sang.

Wengine wanaomezeama mate ugavana wa Nandi ni mwana wa waziri wa zamani, Henry Kosgey, Allan Kosgey, mbunge wa zamani Elijah Lagat na meneja wa shirika la kusafirisha mafuta (KPC) Antipas Tirop.

Bw Tirop jana Alhamisi alisema kuwa ana nafasi bora ya kuibuka mshindi katika uteuzi wa UDA.

Katika Kaunti ya Elgeyo Marakwet, naibu gavana wa sasa Bw Wisley Rotich anaonekana kupendelewa na Dkt Ruto.

Bw Rotich amekuwa mtetezi mkuu wa Naibu wa Rais tangu masaibu yake yalipoanza ndani ya serikali ya Jubilee miaka minne iliyopita.

Bw Rotich anamenyana na aliyekuwa Inspekta wa Polisi Joseph Boinnet, Dkt Loice Kipkorir wa Chuo Kikuu cha Kabianga, mfanyabiashara Sammy Tangus, aliyekuwa mkuu wa Chuo cha Ufundi cha Eldoret Josphat Sawe na Bi Elizabeth Keittany. Bw Boinnet ameonya wakazi dhidi ya kuchagua wanasiasa wanaotoa ahadi hewa zisizotekelezwa.

Dkt Ruto pia anakabiliwa na kibarua kigumu katika Kaunti ya Kericho ambapo wandani wake wametangaza azma ya kumrithi Gavana Paul Chepkwony anayestaafu.

Aliyekuwa waziri wa Ugatuzi Charles Keter anamenyana na mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Embu, Erick Kipkoech Mutai, naibu gavana wa sasa Lily Ng’ok, Prof James Sang na Bw Fred Kirui kati ya wengineo.

Katika Kaunti ya Bomet, Gavana wa sasa Hillary Barchok anapambana na Dkt John Mosonik ambao wote ni wandani wa Dkt Ruto. Atakayeshinda tiketi ya UDA atamenyana na gavana wa zamani Isaac Ruto.

ambaye anawania kupitia Chama cha Mashinani (CCM).

  • Tags

You can share this post!

Kaya Godhoma: Wanaosingiziwa uchawi wahangaika mmiliki...

Wazazi wa Jimi Wanjigi waamriwa wafike kortini

T L