• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Ziara ya Raila yafufua uhasama wa Kiraitu, Munya

Ziara ya Raila yafufua uhasama wa Kiraitu, Munya

Na DAVID MUCHUI

VITA vya ubabe kati ya Gavana wa Meru Kiraitu Murungi na Waziri wa Kilimo Peter Munya vimefufuliwa na ziara ya kiongozi wa ODM Raila Odinga eneo hilo kuanzia leo Jumatatu.

Uhasama wa kisiasa baina ya Mbw Munya na Murungi umetokota tangu 2016, Waziri Munya alipoanzisha kampeni za kumwondoa mamlakani gavana huyo.Wanasiasa hao wawili wameonyesha nia ya kuunga mkono azma ya Bw Odinga ya kuwania urais 2022.

Ziara ya Odinga imechochea vita vipya kati ya wanasiasa hao wenye ushawishi katika kaunti ya Meru huku kila mmoja aking’ang’ania kusimamia mikutano ya kiongozi huyo wa ODM.

Uhasama wa kisiasa sawa na huo ulishuhudiwa katika kaunti jirani ya Isiolo Jumamosi wafuasi wa Gavana Mohamed Kuti na gavana wa zamani walipokabiliana katika mkutano wa Bw Odinga.

Huku chama cha PNU chake waziri Munya kikiwa kimebuni muungano na ODM na kuidhinisha ndoto ya urais ya Bw Odinga, Bw Murungi na wandani wake nao walifanya mkutano na Bw Odinga na kumsifia kama mgombeaji bora.

“Sisi ndio tulimharibia jina Raila ili Mwai Kibaki aweze kushinda. Vile vile, tulimrushia maneno makali tena ili Rais Uhuru ashinde. Ninaweza kusema kwa ukweli kwamba kando na kufanya hivyo, Raila sio mtu mbaya…. Sasa ambapo Kibaki na Uhuru hawawanii, tuweke uwongo kando,” Bw Murungi akasema wakati wa mkutano uliofanywa katika mkahawa wa Safari Park, Nairobi, Septemba 2.

Kulingana na waandalizi wa mikutano ya Bw Odinga katika kaunti ya Meru, miongoni mwa watakaomkaribisha ni pamoja na Naibu Mwenyekiti wa Wakfu wa Mlima Kenya (MKF) Titus Ibui, Gavana Murungi, Waziri Munya na Mbunge wa Igembe Kaskazini Maoka Maore.

Hata hivyo, kaimu mwenyekiti wa PNU David Karithi aliambia Taifa Leo kwamba huenda wakasusia mikutano ya Bw Odinga ili kuwapisha gavana Murungi na wasaidizi wake.

“Bw Odinga amekaribishwa Meru lakini PNU haitashiriki katika mikutano yake Jumatatu. Gavana Kiraitu, Bw Ibui na Maore wametwaa udhibiti wa mikutano hiyo.Wanaweza kumtembeza kote sasa. PNU itapanga mkutano mwingine wa Raila,” Bw Karithi akasema.

Alilalamika kuwa Waziri Munya hakuhusishwa katika maandalizi ya mikutano hiyo licha ya kwamba PNU imebuni muungano na ODM.

“Tulikuwa tukifanya maandalizi ya mikutano hiyo lakini tuliposikia kuwa kundi la Karaitu limeshirikishwa, tuliamua kukaa kando. Chama cha Devolution Empowerment Party kinaweza kuendelea na mipango ya kumkaribisha Bw Odinga wakati huu,” akaeleza.

Mwenyekiti wa ODM kaunti ya Meru Robert Kathata alisema wanatarajia kuwa Gavana Murungi na Waziri Munya wataweka kando tofauti zao na kumkaribisha Bw Odinga kwa furaha.

“Kiongozi wa chama chetu ataanza ziara yake mjini Laare kabla ya kuhutubia mikutano ya kando mwa barabata katika miji ya Maua, Maili Tatu, Kangeta, Muthara, Kianjai na mjini Meru. Tunajuavyo ni kwamba Munya, Kiraitu Maoka na Titus Ibui watashiriki,” Bw Kathata akasema.

Kauli sawa na hiyo ilitolewa na Bi Winnie Kaburu, ambaye atapania kuwania kiti cha ugavana wa Meru kwa tiketi ya ODM.

Mwanasiasa huyo alitoa wito kwa Mbw Munya na Murungi kuonyesha umoja katika mkutano huo.

You can share this post!

Uthabiti wa Chelsea ni mtihani mgumu kwa wapinzani wao...

Serikali kuokoa wanyamapori ili wasiangamizwe na ukame

T L