• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 5:17 PM
Uhuru asema hatageuza msimamo kuhusu Raila

Uhuru asema hatageuza msimamo kuhusu Raila

COLLINS OMULO Na BENSON MATHEKA

RAIS Uhuru Kenyatta amepuuza wanaomtusi kwa kumuunga kiongozi wa ODM, Raila Odinga kuwa mrithi wake, akisema wanaharibu wakati wao bure kwa kuwa hatabadilisha msimamo.

Naibu Rais William Ruto na washirika wake wamekuwa wakimlaumu Rais Kenyatta kwa kuingilia siasa za urithi wake kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Dkt Ruto amekuwa akimtaka ajitenge na kampeni na kumwacha ashindane na Bw Odinga debeni.

Lakini akizungumza Jumapili baada ya kuhudhuria ibada katika kanisa la AIC Pipeline Church, Nairobi, Rais Kenyatta alisema kwamba, hatishwi na matusi anayorushiwa kwa kuchagua kumuunga Bw Odinga akisema ana haki ya kuunga anayehisi anatosha kuwa mrithi wake.

Akionekana kumlenga Dkt Ruto, kiongozi wa nchi alisema kwamba, hababaishwi na matusi ya wasiofurahia uamuzi wake.

“Hata walikuja nyumbani kwangu Ichaweri huko Gatundu kunitusi katika mlango wangu lakini nikawaangalia tu. Yeyote anayefikiri matusi yatampatia kura, atashangaa sana,” alisema Rais Kenyatta.

Ni kwenye mkutano wa kampeni Gatundu mwezi Machi ambapo Dkt Ruto alimtaka Rais Kenya kuacha kumuunga Bw Odinga.

Kwenye mkutano huo, baadhi ya washirika wa naibu rais walikosoa familia ya rais.

“Ninajua nitakapopiga kura yangu na ni haki yangu. Au nimefanya makosa yoyote? Ukitaka kura, nenda ukaombe. Nikisema ninamuunga Baba, simaanishi yule mwingine ni mbaya,” aliongeza.

Rais Kenyatta alikuwa ameandamana na Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i, mwenzake wa Elimu Prof George Magoha, Eugene Wamalwa wa Ulinzi, Joe Mucheru wa ICT, Prof Margaret Kobia wa Utumishi wa Umma na Jinsia, Monica Juma wa Kawi miongoni mwa viongozi wengine akiwemo Gavana wa Nairobi Ann Kananu.

Akigusia shambulio dhidi ya msafara wa Bw Odinga akiwa Soy, Uasin Gishu na Iten, Elgeyo Marakwet mnamo Ijumaa, Rais Kenyatta alihimiza Wakenya kuepuka ghasia za kisiasa na kukumbatia amani na umoja wa nchi akisema “tunataka nchi ambayo tunajiona kama ndugu na dada na sio kama maadui.”

“Hakuna haja ya kuzua ghasia. Kwa nini mnarushia mawe helikopta inayobeba Baba? Hiyo itakusaidia vipi? Kama kitu kingetokea hapo hilo jiwe lipige huyo mzee, si huo ni moto ungewaka katika taifa letu la Kenya? Tunataka mambo kama haya? Tuombe kura kwa heshima na amani,” alisema Rais Kenyatta.

Rais alikuwa akizungumzia tukio la Ijumaa ambapo vijana walirushia mawe helikopita iliyombeba Bw Odinga kwenye mazishi ya mfanyabiashara maarufu Uasin Gishu, Jackson Kibor ambaye ni rafikiye wa karibu wa Bw Odinga.

  • Tags

You can share this post!

Uteuzi Ukambani sasa wamnyima Kalonzo usingizi

PAUKWA: Bahili akausha boda na kuipapia probox

T L