• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 7:55 AM
Uhuru atua Kisumu kisiri

Uhuru atua Kisumu kisiri

RUSHDIE OUDIA na CAROLINE WAFULA

RAIS Uhuru Kenyatta Jumapili aliwashtua wakazi wa Kaunti ya Kisumu kwa kufanya ziara ya ghafla mjini humo akiwa kwenye msafara wa ndege nne za kijeshi.

Hii ilikuwa ni mara ya sita katika muda wa miezi 20 ambapo Rais amezuru ngome hiyo ya kisiasa ya Kiongozi wa ODM, Raila Odinga kichinichini.

Sawa na ziara za awali, jana Rais alikuwa ameenda kukagua ukarabati wa bandari ya Kisumu ambayo imetajwa na wengi kuwa mojawapo ya matunda ya handisheki kati yake na Bw Odinga.

Helikopta ya kijeshi aliyokuwa ameabiri ilimpeleka moja kwa moja hadi katika bandari hiyo ambapo alilakiwa na Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Kenya Railways, Bw Phillip Mainga.

Maafisa wa kaunti na wanasiasa wa eneo hilo hawakufahamishwa mapema kuhusu mpango wa Rais kuzuru Kisumu, huku wanahabari wakizuiwa kuingia katika bandari hiyo.

‘Hii ni hafla isiyohitaji kuangaziwa sana, hata wanasiasa hawaruhusiwi hapa,’ afisa wa usalama wa ngazi ya juu katika bandari alisema kabla Rais kuwasili.Uzinduzi wa bandari hiyo umekuwa ukiahirishwa mara kwa mara licha ya wakuu wa serikali kuahidi kila mara kwamba utazinduliwa ‘hivi karibuni’.

Ziara ya kwanza ya kisiri ilifanyika Januari 19, 2019, na kabla ya jana, alikuwa amezuru bandari hiyo tena Oktoba 15, mwaka uliopita.

Ingawa aliandamana na Bw Odinga kwa ziara za awali, jana duru zilisema balozi huyo wa miundomsingi katika Muungano wa Afrika (AU) hakuonekana katika msafara uliotua bandarini.Ilibainika Rais alikuwa ameandamana na Mkuu wa Jeshi Jenerali Robert Kibochi, Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Vijana kwa Taifa (NYS) Matilda Sakwa na walinzi wachache kuliko ilivyo kawaida.

Maafisa wa kikosi cha polisi cha GSU waliweka ulinzi katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kisumu, sawa na bandarini.

Duru zilisema Rais alikuwa amepanga pia kutembelea bustani ya kibiashara ya Uhuru mjini humo, ambayo inatarajiwa kutumiwa na wafanyabiashara zaidi ya 10,000 ambao sehemu zao za kazi zilibomolewa kutoa nafasi kwa ukarabati wa bandari.

Hata hivyo, hakuenda katika bustani hiyo. Baada ya saa moja na dakika 15 hivi kukamilika, aliondoka bandarini kwa helikopta hiyo na kufululiza hadi uwanja wa ndege ambapo ndege ya kijeshi ilikuwa ikimsubiri.

Haikujulikana mara moja kama alirejea Nairobi kwa ndege hiyo ama alielekea kwingineko.Wakazi walieleza hisia mseto kuhusu ziara hizo za Rais, wengi wakisema wanafurahi anapotembelea kaunti hiyo lakini wakasema ingekuwa bora zaidi iwapo angewahutubia.

‘Tumefurahi kwamba Rais alikuja. Tangu handisheki kati yake na kiongozi wa chama chetu (Bw Odinga), tumeona maendeleo Kisumu hasa katika bandari na Bustani ya Biashara ya Uhuru. Tunatarajia kutakuwa na nafasi nyingi za ajira katika miradi hiyo miwili,’ akasema Bw Phillip Manasse, mmoja wa wakazi.

Kumekuwa na wasiwasi kuhusu hali ya bandari hiyo kutokana na jinsi serikali inavyoahirisha uzinduzi wake mara kwa mara, hali inayotilia shaka iwapo kweli Kenya imejitolea kufufua usafiri wa maji kwa kutumia Ziwa Victoria.

Ingawa baadhi ya maafisa mwaka uliopita walisema uzinduzi uliahirishwa kwa sababu viongozi wengine wa Afrika Mashariki hawakupata muda kuhudhuria, imefichuka kuna sehemu muhimu ambazo bado hazijakamilika kukarabatiwa.

Vile vile, faida ya bandari hiyo itategemea bandari katika upande wa Tanzania na Uganda ilhali nchi hizo mbili hazina haraka kufanikisha mradi huo.

You can share this post!

Ruto aongoza wimbo akirejea kanisani kwa kishindo

Kingi aahidi kuadhibu waliomumunya mamilioni ya corona