• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
Uhuru kujiuzulu Azimio

Uhuru kujiuzulu Azimio

NA MOSES NYAMORI

RAIS mstaafu Uhuru Kenyatta anatarajiwa kujiuzu wadhifa wake kama Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Azimio la Umoja-One Kenya na kuelekeza juhudi zake kuleta amani katika mataifa yanayokumbwa na misukosuko Afrika.

Duru zimeambia Taifa Jumapili kwamba muungano huo unapanga kuandaa mkutano wa baraza lake kuu ambapo Bw Kenyatta atajiondoa rasmi.

Maafisa wa Azimio akiwe mwandani wa Bw Kenyatta wa muda mrefu David Murathe, wanasema kuwa tayari rais huyo mstaafu amejitenga na masuala ya uendeshaji wa shughuli za muungano huo tangu alichukua wadhifa wa kuwa mpatanishi mkuu katika shughuli za amani Ethiopia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Bw Kenyatta alipewa wajibu huo na mrithi wake Rais William Ruto mnamo Septemba 13, 2022 dakika chache baada ya kula kiapo kuwa Rais wa tano wa Jamhuri ya Kenya.

Mipango yake ya kujiuzulu pia imechangiwa na hitaji la kisheia kwamba hafai kushikilia wadhifa wowote wa kisiasa ili aweze kulipwa pensheni yake.

Bw Kenyatta ana muda wa hadi Februari 2023 kujiuzulu, kulingana an Sheria ya Malipo ya Pensheni ya Rais Mstaafu ya 2003.

Mipango ya kujiuzulu kwa rais huyo mstaafu inajiri wakati ambapo wanasiasa wengi wa mrengo wa Azimio, na wandani wa Odinga, wanahamia upande wa muungano tawala wa Kenya Kwanza.

Hatua ya wandani wa Odinga kuvutiwa na mrengo wa Rais Ruto na kujiondoa kwa Bw Kenyatta kutoka uongozi wa Azimio, inaonekana kama pigo jingine kwa Waziri huyo Mkuu wa zamani ambaye ameanza kuwaleta pamoja wafuasi wake kuanzisha harakati za kupinga serikali ya Rais Ruto.

Muungano wa Azimio wenye jumla ya vyama tanzu 26 ulibuni asasi mbili kuu katika uongozi wa wake; Baraza Kuu la Muungano na Baraza Kuu Tekelezi la Kitaifa ((NCEC).

Kuelekea uchaguzi mkuu wa Agosti 9, Bw Kenyatta aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Azimio- ambalo lenya mamlaka makuu zaidi. Bw Odinga aliteuliwa kiongozi wa muungano huo ambao pia ni chama huku aliyekuwa Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya akiteuliwa mwenyekiti wa NCEC.

Naibu mwenyekiti wa NCEC ni Bw Murathe ambaye pia ndiye naibu mwenyekiti wa chama cha Jubilee.

Katibu Mkuu wa NCEC ni Mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohamed ambaye ni kiranja wa wachache katika Bunge la Kitaifa. Bw Mohamed pia ni mkurugenzi wa uchaguzi katika chama cha ODM, mojawapo ya vyama vikuu tanzu katika Azimio. Bw Odinga pia ndiye kiongozi wa ODM.

Bw Murathe aliambia Taifa Jumapili kwamba baada ya kuondoka kwa Bw Kenyatta, Odinga ndiye atachukuwa wadhifa wa kiongozi wa Azimio kuendelea mbele.

“Tutakuwa na mkutano hivi karibuni ambapo Rais Kenyatta atajiuzulu rasmi kama mwenyekiti wa Baraza Kuu la Azimio. Bila shaka basi haliwezi kuendeshwa na madereva mawili. Hili basi linaloitwa Azimio sasa lina dereva mmoja na dereva huyo ni Jakom (Bw Odinga),” akasema Bw Murathe.

Mwanasiasa huyo alisema kuwa Bw Kenyatta ameamua kuelekeza juhudi zake katika wadhifa wake kama balozi wa amani katika ukanda huu.

“Sasa yuko juu ya siasa za humu nchini. Kuendelea mbele kila kitu katika Azimio kitaendesha na Odinga. Baraza litakutana na kuamua yule atachukua nafasi ya Bw Kenyatta lakini kiongozi rasmi wa Azimio ni Bw Odinga,” Bw Murathe akasema.

Bw Oparanya pia alisema Bw Kenyatta hajakuwa akijihusisha na shughuli za Azimio baada ya Bw Odinga kupoteza katika uchaguzi wa urais.

Gavana huyo wa zamani alisema ni nadra kwa Bw Kenyatta kuulizwa kuhusu masuala ya kisiasa kwa sababu “amezongwa na shughuli nyingi za kuongoza juhudi za kuleta amani DRC.”

Bw Oparanya pia alirejelea hitaji la kisheria kwamba Bw Kenyatta sharti ajiuzulu ili aweze kupokea pensheni yake.

“Ikiwa hatajiuzulu haweze kupata pensheni yake. Kujiuzulu kwake sio suala kubwa kwa sababu hatutarajii kuwa ataendelea kuchapa siasa kuendelea mbele,” akasema.

“Hajakuwa akishughulika zaidi na mambo ya siasa tangu baada ya uchaguzi. Imekuwa nadra kwetu kushauriana naye kuhusu masuala ya Azimio,” Bw Oparanya akasema.

Naye Katibu Mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni alisema japo hana habari kuwa kujiuzulu kwa Bw Kenyatta, ni wazi kuwa Rais huyo wa zamani hawezi kuendelea kujishughulisha na siasa za nchini ikizingatiwa kuwa anaongoza juhudi za kuleta amani katika mataifa ya kanda hii.

“Wakati huu masuala ya Azimio yanaendeshwa na wale ambao wako katika siasa. Japo sina habari kwamba anajiondoa lakini sidhani wadhifa anaoshikilia sasa wa kuongoza mchakato wa amani Ethiopia na DRC utampa nafasi ya kuendelea na siasa,” akasema Bw Kioni ambaye ni mbung wa zamani wa Ndaragua.

Kulingana na sehemu 6 (1) ya Sheria ya Pensheni ya Rais Mstaafu, Rais mstaafu hatashikilia wadhifa katika chama chochote cha kisiasa kwa zaidi ya miezi sita baada ya kuondoka afisini kama Rais.

Hitaji hili linamaanisha kuwa Bw Kenyatta pia atajiuzulu kama Kiongozi wa Jubilee mnamo Februati mwaka ujao, 2023, ambao ni miezi sita baada yake kumkabidhi Dkt Ruto mamlaka.

Sheria hiyo pia inasema kuwa Rais mstaafu atatarajiwa kutekeleza wajibu wa mushauri wa serikali na watu wa Kenya.

“Rais mstaafu anaweza kuomba na serikali kutekeleza majukumu fulani na atalipwa marupurupu fulani kwa kutekeleza majukumu hayo rasmi,” sheria hiyo inaongeza.

Msajili wa Vyama vya Kisiasa Anne Nderitu, kwa upande wake, akisema afisi yake haijapokea habari kuhusu kujiuzulu kwa Bw Kenyatta.

Bw Kenyata amekuwa ajihusisha katika mazungumzo ya amani kati ya Serikali ya Ethiopia na Kundi la waasi la Tigray People’s Liberation Front (TPLF).

Mwanzoni, rais huyo mstaafu alikosa kuhudhuri mkutano wa mwanzo katika ya pande hizo mbili uliofanyika Afrika Kusini, lakini sasa amekumbatia kikamilifu wajibu wake katika mchakato huo.

Aidha, Bw Kenyatta ni msimamizi wa mchakato wa kuleta amani DRC unaodhaminiwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Anaongoza upatanishi kati ya Serikali ya DRC na kundi la waasi la M23.

Kando na Kenyatta na Odinga wanachama wengine wa Baraza Kuu la Azimio ni; kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, kiongozi wa Narc-Kenya Martha Karua,  mwenyekiti wa Kanu, Gideon Moi, aliyekuwa Gavana wa Mombasa Hassan Joho, Mbunge Maalum Sabina Chege, aliyekuwa Mbunge wa Taveta Naomi Shaban, aliyekuwa Gavana wa Kitui  Charity Ngilu. Wengine ni; Wafula Wamunyinyi, Abdi Noor Omar Farah na  Junet ambaye huketi katika baraza hilo kwa misingi kuwa yeye ndiye katibu mkuu wa baraza la NCEC.

Tafsiri: CHARLES WASONGA

  • Tags

You can share this post!

DARUBINI YA WIKI: Toleo Nambari 15

Familia ya shabiki Isaac Juma yapewa makao mapya Mumias

T L