• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 4:40 PM
Gachagua ataka Wakenya wampe Rais Ruto muda wa kuimarisha uchumi

Gachagua ataka Wakenya wampe Rais Ruto muda wa kuimarisha uchumi

DPCS na CHARLES WASONGA

NAIBU Rais Rigathi Gachagua amewataka Wakenya kuwa na imani kwamba Rais William Ruto ataimarisha uchumi wa nchi.

Kwa hivyo, amewataka wawe wavumilivu ili mikakati ambayo kiongozi wa taifa ameweka iweze kuzaa matunda.

“Rais Ruto anatia bidii kuboresha uchumi. Kulikuwa na shida kadha mwanzoni mwa mchakato huo lakini Rais ameweka mipango mizuri, nguvu na kikundi chenye bidii cha kuleta mageuzi nchini. Muwe wavumilivu, mmkumbuke katika maombi na mmuunge mkono tukitembea safari hii pamoja,” Bw Gachagua akasema.

Alisema hayo Jumapili katika Kanisa la AIC Zombe, Kitui Mashariki, Kaunti ya Kitui, ambako alihudhuria ibada ya Jumapili.

Bw Gachagua aliongeza kuwa Serikali ya Ruto haitabagua sehemu yoyote ya nchi katika mpango wa kwa kutekeleza maendeleo ya kiuchumi.

Kauli ya Bw Gachagua inajiri wiki moja baada yake kusema kuwa serikali ya Ruto itatumia miaka mitano kuweka mipango ya maendeleo kisha itumie miaka mingine mitano kutekeleza mipango hiyo.

Akiongea wakati wa ibada ya Jumapili katika eneo la Manyatta, Kaunti ya Embu, Jumapili, Desemba 10, 2023, Naibu Rais alisema miaka mitano haitoshi kufufua uchumi uliozorota.

Bw Gachagua alitoa wito kwa wakazi wa Embu kumchagua tena Rais Ruto mwaka 2027.

Alieleza kuwa hata rais wa zamani marehemu Mwai Kibaki aliandikisha kumbukumbu nzuri kupitia miradi aliyotekeleza katika muhula wake wa pili afisini.

“Kazi nzuri inahitaji miaka 10 ili miaka mitano ya kwanza iwe ni ya kuweka mipango. Si mwajua kuwa Mwai Kibaki alikuwa na matatizo mengi katika muhula wake wa kwanza? Si alitumalizia kila kitu katika muhula wake wa pili? Kwa hivyo, tunaomba mmpe Rais Ruto miaka yake 10 na Gavana Mbarire pia miaka yake 10 na hata huyo Mundigo (Seneta Alexander Mundigi),” Bw Gachagua akaeleza.

Desemba 17, 2023, Bw Gachagua alikariri kuwa Rais Ruto alirithi uchumi dhaifu uliozongwa na changamoto nyingi kama vile mzigo wa madeni wa kima cha Sh9.6 trilioni.

“Rais Ruto amefanya kazi na matokeo yatafurahiwa na watu wote hivi karibuni,” Bw Gachagua akasema.

Kuhusu shida ya barabara na maji katika eneo la Ukambani, Naibu Rais alisema serikali imejitolea kusuluhisha changamoto hizo ili kuchochea ukuaji wa kiuchumi katika maeneo hayo.

“Serikali inaendeleza ujenzi wa mabwawa ya Thwake na High Grand kuzima shida ya maji katika eneo hili. Mpango wa kuweka lami barabara ya Chiluni-Zombe-Mwitika unaendelea,” akasema.

“Serikali itasuluhisha matatizo ya maji Ukamba. Rais na mimi tutaendelea kuwasiadia wake wa eneo hili, kupiga jeki miradi ya maendeleo n ahata shughuli za kanisa,” Bw Gachagua akasema.

Alikuwa akijibu maombi ya viongozi wa eneo hilo waliotaka serikali ianzishe miradi ya maendeleo eneo hilo.

Bw Gachagua alisema kuwa miradi ya maji itaunua kilimo, uzalishaji chakula na ukuaji wa kiuchumi eneo hilo.

Lakini aliwataka viongozi wa Ukambani kunyoosha siasa zao kwa kugura upinzani.

“Mmekuwa mkimfuata Raila Odinga kwa miaka mingi ilhali alimdhalilisha kiongozi wa jamii yetu, Kalonzo Musyoka, kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022 kwa kumlazimisha afanyiwe mahojiano kwa nafasi ya mgombea mwenza. Huwezi kudhulumu jamii nzima kwa kumfanyia kiongozi wake mahojiano kwa nafasi kama hiyo. Tuheshimu jamii, haswa jamii ambayo imekuunga mkono katika chaguzi tano,” Bw Gachagua akasema, akirejelea mahojiano yaliyofanywa na Azimio la Umoja-One Kenya kusaka mgombea mwenza wa Bw Odinga.

Hatimaye kiongozi wa Narc Kenya Martha Karua ndiye aliyeteuliwa na Bw Musyoka akaahidi wadhifa wa Waziri Mkuu endapo Bw Odinga angeshinda katika uchaguzi huo wa Agosti 9, 2023.

Bw Gachagua aliandamana na Waziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Maeneo Kame Peninah Malonza na Katibu wa Idara ya Ugatuzi Teresiah Mbaika.

Pia walikuwepo wabunge kadha, miongoni mwao wakiwa ni; Nimrod Mbai (Kitui Mashariki), Rachael Nyamai (Kitui Kusini), Benjamin Gathiru, maarufu Mejja Donk, (Embakasi ya Kati), Zaheer Jhanda (Nyaribari Chache), Kivai Kagesi (Vihiga), Japheth Nyakundi (Kitutu Chache).

Wengine walikuwa wabunge wa zamani Victor Munyaka (Machakos Mjini), James Mbaluka (Kibwezi Magharibi) na Kisoi Munyao (Mbooni).

  • Tags

You can share this post!

Kang’ata aandika barua akilia kuhusu kuharibika kwa...

Uhuru ni kikwazo kwa maridhiano, adai Mudavadi

T L