• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Ukuruba na Jubilee sumu ya Raila kwa ndoto yake 2022

Ukuruba na Jubilee sumu ya Raila kwa ndoto yake 2022

Na BENSON MATHEKA

UKURUBA wa kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga na Rais Uhuru Kenyatta unaweza kumharibia sifa kinara huyu wa upinzani ambaye kwa miaka mingi amekuwa mtetezi sugu wa haki na demokrasia. Hii ni ikiwa ushirikiano huu utamlazimu kuunga mkono sera na maamuzi ya serikali yanayokandamiza raia.

Wadadisi wa siasa wanasema hali hii inaweza kutumiwa na wapinzani wake wa kisiasa iwapo atagombea urais 2022.

Wanasema kwa miaka mingi Bw Odinga amejijenga kisiasa akiwa mtetezi wa raia dhidi ya unyanyasaji wa serikali lakini tangu handisheki yake na Rais Kenyatta, amebadilisha msimamo na kuunga sera za serikali zinazokandamiza masikini.

“Bw Odinga huenda alichimbia kaburi sifa zake kama mtetezi wa demokrasia na utawala bora. Msimamo wake tangu aanze kushirikiana na serikali unamsawiri kama kiongozi tofauti na yule ambaye Wakenya walimzoea. Anaunga maamuzi na miswada inayonuiwa kunufaisha wachache na kukandamiza mamilioni ya Wakenya anaotarajia watampa kura iwapo atagombea urais katika uchaguzi mkuu wa 2022,” asema Bw Peter Wainaina.

Bw Odinga binafsi hajatangaza iwapo atagombea urais katika uchaguzi mkuu wa 2022 lakini wandani wake wa karibu akiwemo kaka yake Oburu Odinga wamesema atakuwa kwenye debe.

Naibu mwenyekiti wa chama tawala cha Jubilee David Murathe ambaye ni mtetezi wa handisheki pia amenukuliwa akiambia wakazi wa eneo la Mlima Kenya wajiandae kwa urais wa Bw Odinga.

Hii ikiwa ishara kwamba ukuruba wa waziri mkuu huyo wa zamani na Rais Kenyatta unalenga kumsaidia kuongoza nchi. Ukuruba huu umemfanya Bw Odinga kufyata mdomo serikali inapohusishwa na maovu kama ufisadi, polisi kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya raia na kuunga sheria zinazokandamiza raia.

Wadadisi wanataja kimya cha Bw Odinga kuhusu sakata ya wizi wa mabilioni ya pesa zilizotolewa na wafadhili kusaidia Kenya kukabili janga la corona, mzozo kuhusu ugavi wa pesa za kaunti ambao unalenga kuhujumu lengo halisi la ugatuzi kwa kupokonya kaunti 19 masikini mabilioni ya pesa, ubomoaji wa makazi ya watu masikini na sera zinazofanya gharama ya maisha kulemea masikini mbali na polisi kutumiwa kuhangaisha wanaopinga serikali kama tisho kwa sifa ya Bw Odinga kama mtetezi wa usawa, demokrasia na utawala bora unaoongozwa na sheria.

“Hatua hii inawapa wapinzani wake silaha ya kumshambulia ikiwa atagombea urais. Watamsawiri kama anayeunga serikali inayoendeleza maovu ambayo amekuwa akiyalaani kwa miaka mingi. Wapinzani wake watadai kuwa amekuwa akijifanya mtu mzuri kwa miaka mingi ilhali kumbe yeye ni mbwa mwitu aliyevalia ngozi ya kondoo,” asema Bw Wainaina.

“Wapinzani wake, iwapo atagombea urais, watakuwa na orodha ya masuala ambayo hatayaepuka kwa kusema hakuwa serikalini hasa baada ya Naibu Rais William Ruto kutengwa katika maamuzi ya serikali kwa kutounga handisheki,” asema Bw Darius Mwanjala, mdadisi wa siasa wa miaka mingi.

“Bw Odinga ambaye amekuwa akilaumu serikali ya Kanu kwa ufisadi na kukandamiza uhuru na haki za Wakenya sasa anaunga serikali inayoendeleza maovu hayo. Atawaambia nini wapinzani wake wakati wa kampeni? Odinga ambaye amekuwa akitetea uhuru wa mahakama sasa anaunga mkono serikali inayouhujumu kwa kukataa kuapisha majaji.

Odinga ambaye amekuwa akitetea usawa na ushirikishi ananyamaza nyadhifa nyingi kuu serikalini zikikabidhiwa jamii moja,” anasema Bw Mwanjala. Wadadisi wanasema kuwa Wakenya wamejanjaruka na hawawezi kudanganywa kwa urahisi na wanasiasa ilivyokuwa zamani.

“Nina uhakika wapinzani wa Bw Odinga watatumia ushirika wake na serikali ya Jubilee kumuumbua wakati wa kampeni. Kutakuwa na miungano miwili mikubwa kwenye uchaguzi mkuu ujao.

“Mmoja utaongozwa na Bw Odinga na mwingine Bw Ruto ambaye ameanza kujijenga kama mpinzani kwa kukosoa baadhi ya maamuzi ya serikali ambayo Bw Odinga anaunga,” asema mdadisi wa siasa Tony Kagogo.

Anataja msimamo wa Bw Odinga kuhusu ugavi wa pesa za kaunti na ufisadi wa sasa kama baadhi ya masuala yatakayogeuka kuwa jinamizi kwake wakati wa kampeni.

You can share this post!

Serikali inavyojenga wanasiasa ikidhani inawatia adabu!

Sevilla yapiga Inter kutwaa Europa kwa mara ya 6