• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 9:16 PM
Undumakuwili wa Ruto huenda ukafifisha ari ya Mudavadi na Weta

Undumakuwili wa Ruto huenda ukafifisha ari ya Mudavadi na Weta

NAIBU Rais William Ruto ameonekana kuweka masharti katika mipango yake ya kuunda muungano na kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi na mwenzake wa Ford Kenya Moses Wetang’ula, ambayo yanaashiria kwamba mipango yake ina malengo fiche.

Hii ni licha kwamba wawili hao wamekana madai kuwa mazungumzo yanaendelea kati yao na kambi ya Dkt Ruto kwa lengo la kubuniwa kwa muungano kuelekea uchaguzi mkuu ujao.

Wakiongea na wanahabari Alhamisi katika mkahawa mmoja eneo la Karen, Nairobi Mbw Mudavadi na Wetang’ula walisema kuwa hawajapokea mwaliko wowote kwa kambi ya naibu rais.

“Habari zinasambaa kwamba ninafanya mazungumzo na mtu fulani kuhusu masuala ya uchaguzi ilhali hiyo sio kweli. Ikiwa nitazungumza na mtu fulani, nitasema; sitaficha,” Bw Mudavadi akasema.

Lakini mnamo Desemba mwaka jana, Dkt Ruto alifichua kuwa ameanzisha mazungumzo na Mbw Mudavadi na Wetang’ula kwa nia ya wao kufanyakazi pamoja kuelekea uchaguzi mkuu wa Agosti 9, mwaka huu.

“Ninaendelea kuongea na Mudavadi na Wetang’ula ili tuunde serikali pamoja, kwa mapenzi ya Mungu. Na hii ninaomba kwa unyenyekevu mkubwa zaidi,” Dkt Ruto akasema.

“Jambo muhimu wakati huu ni kwamba tunapaswa kufanya kazi pamoja ili tushinde uchaguzi mkuu ujao. Kwa hivyo, binafsi nitawatafuta Mudavadi na Wetang’ula ili kwa pamoja tufanye uamuzi wa mwisho,” akaongeza.

Dkt Ruto alirejelea kauli hii kwenye mahojiano katika runinga ya Citizen akisema, bila kutoa ithibati, kwamba chama chake cha United Democratic Alliance (UDA) kina maono sawa nay a vyama vya ANC na Ford Kenya.

Lakini naibu rais ameonekana kuwa mwanasiasa anayelenga kutumia ushawishi wa Bw Mudavadi na Wetang’ula, kunasa kura za urais kutoka eneo la magharibi kisha kuwatelekeza.

Kwa mfano, kwenye mahojiano hayo hayo kwenye runinga ya Citizen Dkt Ruto aliweka wazi kuwa suala la ugavi wa nyadhifa halitazingatiwa katika ushirikiano wake na vyama vya ANC na Ford Kenya.

Aidha, alishikilia kauli yake ya awali, kwamba UDA ni chama cha kitaifa na kitadhamini wagombeaji katika sehemu zote nchini, ikiwemo “maeneo ambayo yanachukuliwa kuwa ngome za wanasiasa fulani.”

“Sitaki tujenge urafiki wa kisiasa kisha uniambie kuwa katika maeneo fulani UDA haitadhamini wagombeaji kwa sababu ni ngome yako. Chama chetu cha UDA ni cha kitaifa na kitadhamini wagombeaji katika viti vyote kote nchini. Hii ni kwa sababu tunaongozwa na sera ya kuwasaidia wananchi wadogo sio ubabe wa kisiasa au ugavi wa vyeo,” Dkt Ruto akasema.

Kauli hii inaashiria kuwa Dkt Ruto ameanza kuweka masharti ambayo anataka vyama vya ANC na Ford-Kenya vizingatie kabla ya kukumbatiwa na UDA.

Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Dismus Mokua anasema itakuwa vigumu kwa Dkt Ruto kuwashawishi Mbw Mudavadi na Wetang’ula kukubali kuungana naye.

“Nguzo kuu katika mikataba ya miungano kati ya vyama huwa ni ugavi wa mamlaka. Ikutumbukwe kwamba kiongozi wa ODM Raila Odinga alikosana na Rais mstaafu Mwai Kibaki baada ya ushindi wa NARC mnamo 2002 kwa sababu Kibaki alidinda kutimiza ahadi ya kubadilisha Katiba ili kumtunuku Raila wadhifa wa Waziri Mkuu,” anasema Bw Mokua.

Anaongeza: “Hivi majuzi suala hilo hilo la mamlaka ndilo lilichangia kusambaratika kwa muungano wa NASA na hata chama cha Jubilee. Mbw Mudavadi na Wetang’ula na vinara wenzake walikosana na Raila, naye Dkt Ruto mwenyewe alikosana na Rais Uhuru Kenyatta baada ya kuchezewa shere kuhusiana na cheo cha urais.”

Lakini Katibu Mkuu wa UDA Veronica Maina amethibitisha kuwa chama hicho kina nia ya kufanya mazungumzo na ANC na Ford- Kenya japo hakutoa masharti sawa na alivyofanya bosi wake.

“Kama UDA, tumewaalika rasmi Mbw Mudavadi na Weteng’ula kwa mazungumzo. Tunasubiri majibu yao. Wakikubali tutawasikiliza kwa sababu UDA ni chama cha demokrasia. Hii ni tofauti na msimamo wetu wa awali kwamba yeyote anayetaka kutuunga mkono sharti ajiunge na UDA,” Bi Maina akaeleza.

Lakini mwenyekiti wa chama hicho Johnstone Muthama anasema kuwa nia yao ya kufanyakazi na baadhi ya vyama vya kisiasa kwa lengo la kushinda uchaguzi mkuu haijajikita katika kutia saini mikataba ya maelewano.

“Kufanya mazungumzo na vyama vingine vyenye maono sawa na UDA sio sawa na kubuni muungano. Hatuko tayari kuingia katika mkataba wa maelewano na chama fulani na kuwasilisha hati hiyo kwa msajili wa vyama vya kisiasa.

“Hatutaki kuvuta huku na kule kwa sababu ya mikataba ya maelewano ambayo wananchi hawafahamu. Hii italeta shida nyingi ilivyoshuhudiwa katika miungano ya awali kama vile NARC, CORD na Jubilee,” akaeleza Bw Muthama ambaye ametangaza kuwa atawani kiti cha ugavana wa Machakos kwa tiketi ya UDA.

Naye Mbunge wa Sirisia John Waluke ametoa wito kwa wakazi wa magharibi mwa Kenya kuwachagua wagombeaji wa UDA kuanzia ngazi ya udiwani hadi urais.

Hii inashadidia shauku iliyotanda miongoni mwa wafuasi wa ANC na Ford Kenya kwamba huenda UDA inawachezea shere.

  • Tags

You can share this post!

Raila ‘adandia’ sifa ya Kibaki kukwea Mlima...

Hatua ya Washiali kujiondoa kuwania ubunge yauma UDA

T L