• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 9:16 PM
Raila ‘adandia’ sifa ya Kibaki kukwea Mlima Kenya

Raila ‘adandia’ sifa ya Kibaki kukwea Mlima Kenya

KIONGOZI wa ODM, Bw Raila Odinga, atategemea msukumo wa “kivuli” cha Rais Mstaafu Mwai Kibaki kumsaidia kupenya kisiasa katika eneo la Mlima Kenya uchaguzi mkuu wa Agosti unapokaribia.

Hatua ya Bw Odinga kumteua Gavana Nderitu Mureithi wa Laikipia kuongoza kampeni zake za urais mwaka huu, inatajwa kama njama ya kujaribu kutumia sifa ya Bw Kibaki kuwashawishi wenyeji wa eneo hilo kumuunga mkono.

Bw Nderitu ni mpwaye Bw Kibaki.Sawa na Bw Kibaki, yeye ni mwanauchumi. Tangu kuchaguliwa kama gavana wa Laikipia, amekuwa akisifiwa kwa kuistawisha sana kimaendeleo, hatua inayofananishwa na utendakazi wa Bw Kibaki.

Wadadisi wanasema ikizingatiwa wenyeji wa Mlima Kenya wamekuwa wakimsifia Bw Kibaki kwa mikakati aliyoweka kufufua uchumi wa nchi wakati wa utawala wake, lengo la Bw Odinga ni kuonyesha kwamba “yuko tayari kuoanisha mikakati yake ya kufufua uchumi na hatua alizochukua Bw Kibaki.”

“Ni wazi kuwa uchumi wa nchi umedorora. Wakenya wengi na wenyeji wa Mlima Kenya kwa jumla wamekuwa wakirejelea jinsi uchumi ulivyokuwa bora enzi ya Bw Kibaki kulinganisha na hali ya sasa. Lengo la Bw Odinga ni kuonyesha amejitayarisha vilivyo kufufua uchumi na kuirejesha nchi katika hali ilivyokuwa kiuchumi kati ya 2003 na 2013,” asema Bw Wycliffe Muga, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

Sababu nyingine inayoelezwa kuchangia Bw Odinga kuegemea “kivuli” cha Bw Kibaki ni kuonyesha “anamrudishia mkono” baada ya kumfanyia kampeni mnamo 2002 chini ya kauli ya ‘Kibaki Tosha.”

Kwenye majukwaa mbalimbali, Bw Odinga amekuwa akirejelea jinsi alivyomsaidia Bw Kibaki kuendesha kampeni zake baada yake (Kibaki) kupata ajali na kulazwa hospitali nchini Uingereza.

“Bw Odinga analenga kuonyesha kuwa hatimaye wakati umefika kwa Bw Kibaki kumrudishia mkono, hivyo wenyeji wa Kati wanafaa kufanya vivyo hivyo,” asema Prof Ngugi Njoroge, ambaye ni mdadisi wa siasa.

Sababu ya tatu ya Bw Odinga kulainisha mikakati yake na Bw Kibaki ni kuondoa dhana kwamba wawili hao ni mahasimu wa kisiasa, hasa baada ya ghasia zilizotokea nchini baada ya uchaguzi tata wa 2007.

Wadadisi wanasema Bw Odinga ana kibarua kuondoa dhana miongoni mwa wenyeji wa Mlima kwamba “alimsumbua” Bw Kibaki wakati alihudumu kama Waziri Mkuu kati ya mwaka 2008 na 2013.

Ingawa wanafisia mkakati huo, wanasema kibarua alicho nacho Bw Odinga ni kuuza mikakati yake kwa wenyeji, ikizingatiwa wengi wao ni vijana waliozaliwa baada ya 2002.

“Ni mkakati mzuri wa kisiasa kwani Bw Kibaki anakumbukwa kama kiongozi aliyeistawisha nchi katika nyanja zote. Hata hivyo, kibarua alicho nacho ni kudhihirisha wazi mikakati yake binafsi bila kujihusisha na Bw Kibaki, ambaye tayari ashastaafu,” akasema Prof Ngugi.

  • Tags

You can share this post!

Rigathi Gachagua na Moses Kuria wakabana koo kuhusu...

Undumakuwili wa Ruto huenda ukafifisha ari ya Mudavadi na...

T L