• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 6:50 AM
Usimwamini Uhuru, sasa Gachagua aonya Kalonzo

Usimwamini Uhuru, sasa Gachagua aonya Kalonzo

Na CHARLES WASONGA

MBUNGE wa Mathira Rigathi Gachagua amemtaka kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka kutoweka matumaini yake kwa Rais Uhuru Kenyatta kuwa mpatanishi bora kati yake na kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Akiongea Jumapili usiku katika kupindi cha “Checkpoint” kwenye runinga ya KTN mbunge huyo alisema Rais Kenyatta hatamfaa Bw Musyoka kwa sababu tayari ametangaza kuwa anamuunga mkono Bw Odinga katika kinyang’anyiro cha urais.

“Nashangaa ni vipi Uhuru ataongoza mazungumzo kati ya Kalonzo na Raila ilhali yeye pia ni mwanasiasa mwongo. Raila alimsaliti Kalonzo katika muungano wa NASA na Uhuru akamhadaa Dkt William Ruto katika Jubilee,” akasema.

Lakini wakili Martin Oloo, ambaye pia alishiriki katika kipindi hicho, alisema Dkt Ruto amewahi kusaliti wanasiasa wenzake.

“Ruto pia amewahi kumgeuka kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi mnamo 2012 siku chache baada ya yeye na Rais Kenyatta kuahidi wangemuunga mkono katika kinyang’anyiro cha urais. Baadaye walidai kuhadaiwa na mashetani,” akaeleza.

Bw Gachagua, ambaye ni mwandani wa karibu wa Dkt Ruto, alitaja muungano wa Azimio la Umoja kama ambao unaongozwa na watu aliowataja kama “wasaliti wa kisiasa”.

“Rais Kenyatta hawezi kuwa mpatanishi katika suala ambalo tayari amefikia uamuzi na kushikilia msimamo,” Bw Gachagua akasema.

Alimtaka Bw Musyoka kuwa mwangalifu katika mipango yake ya kushirikiana na Azimio la Umoja kwa sababu Bw Odinga ni “mwanasiasa asiyeaminika”.

“Raila alimsaliti kwa kukiuka ahadi kwamba angemuunga mkono kuwania urais 2022. Vile vile, alimsaliti pale alipofanya handisheki na Uhuru mnamo Machi 9, 2018,” akasema.

“Azimio ni muungano wa waongo. Waliwahadaa Kalonzo, Mudavadi na Wetang’ula hapo awali. Kwa upande mwingine Uhuru amemdanyanga William Ruto alipoahidi kumsaidia kuingia Ikulu mwaka huu, lakini sasa amemgeuka,” Bw Gachagua akaongeza.

Kenya Kwanza

Wanasiasa wanaoegemea mrengo wa muungano wa Kenya Kwanza wamekuwa wakimlaumu Rais Kenyatta kwa kuvunja ahadi yake ya kumuunga mkono Dkt Ruto katika kinyang’anyiro cha urais na badala yake kuunga mkono Bw Odinga.

Wiki jana, Bw Musyoka alisema kuwa yuko tayari kufanyakazi na Bw Odinga katika Azimio la Umoja lakini kwa sharti kwamba kiongozi huyo wa ODM aunge mkono ndoto yake ya urais.

Kwenye kikao na wanahabari, kiongozi huyo wa Wiper alifichua kuwa msimamo wake unawiana na mkataba kati yake na Bw Odinga kabla ya uchaguzi mkuu wa 2017.

“Ndugu yangu Raila aliahidi kwamba ataniunga mkono kwa kiti cha urais 2022 baada ya mimi kumuunga mkono 2017. Mkataba huo ungalipo na ahadi hiyo haijatimizwa. Nimekubali kushirikiana naye lakini kwa sharti kwamba atakubali kuniunga mkono kuwa mgombea urais wa muungano mkuu wa Azimio-One Kenya Alliace,” Bw Musyoka alisema kwenye kikao na wanahabari katika afisi zake zilizoko Karen, Nairobi.

You can share this post!

Ashtakiwa kwa madai ya kuiba Sh4.9m za mwajiri wake

ODM kuwafadhili wanachama wanawake watakaogombea ubunge...

T L