• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 6:50 AM
ODM kuwafadhili wanachama wanawake watakaogombea ubunge maeneo 290 nchini

ODM kuwafadhili wanachama wanawake watakaogombea ubunge maeneo 290 nchini

NA JUSTUS OCHIENG

CHAMA cha ODM kinachoongozwa na aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga, kimepata ufadhili kusaidia wanawake wanaowania viti vya ubunge katika maeneobunge yote 290 kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Katibu Mkuu wa ODM, Edwin Sifuna alitaja hatua hiyo kama zawadi ya siku ya wanawake iliyoadhimishwa Jumanne kwa wawaniaji wanawake wa chama hicho.

Bw Sifuna ambaye pia ni mdhamini wa mpango wa “HE for SHE” wa kundi la wanawake wa ODM, pia alifichua kwamba wanaogombea viti vya Mwakilishi wa Kike hawajumuishwi katika mpango huo.

“Usaidizi huu unalenga kuhakikisha thuluthi mbili ya wabunge katika Bunge la Kitaifa sio wa jinsia moja baada ya uchaguzi mkuu wa Agosti,” alisema Bw Sifuna.

Ufadhili huo, alisema, utatumiwa kulipia watakaochaguliwa katika mpango huo ada za uanachama wa maisha wa ODM (Sh20,000), ada za mchujo na ada za uteuzi zinazotozwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) baada ya kushinda tiketi ya chama kwenye mchujo.

“Mfumo utakaotumiwa ni kwamba mmoja ni lazima awe mwanamke, mwanachama wa ODM, lazima awe anawania ubunge katika eneobunge lolote kati ya 290 nchini lakini sio wagombeaji wa kiti cha Mwakilishi wa Wanawake,” alisema.

Alifafanua kuwa watakaopata ufadhili huo, ni wale ambao hawajawahi kuchaguliwa katika wadhifa wowote nchini Kenya.

“Wawaniaji wanawake walio na umri wa chini ya miaka 35 na wale wanaoishi na ulemavu wanahimizwa kutuma maombi. Wanaotimiza mahitaji yaliyotajwa hapo juu wanaweza kutumia maombi yao kwa Katibu Mkuu kupitia baruapepe pekee; [email protected] kabla au Machi 9 2022,” Bw Sifuna alisema kwenye taarifa.

You can share this post!

Usimwamini Uhuru, sasa Gachagua aonya Kalonzo

Pigo Leeds United mvamizi tegemeo akitarajiwa kusalia...

T L