• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 9:01 PM
Vinara wa Kenya Kwanza wadai Uhuru anapoteza muda kuzuru Mlima Kenya

Vinara wa Kenya Kwanza wadai Uhuru anapoteza muda kuzuru Mlima Kenya

NA GEORGE MUNENE

VIONGOZI wa Muungano wa Kenya Kwanza wamemkashifu Rais Uhuru Kenyatta kwa kuamua kuzuru eneo la Mlima Kenya baada ya kulitelekeza kwa muda mrefu, huku wakipuuzilia ziara hiyo kama isiyo na maana yoyote.

Wakiongozwa na Mbunge wa Mathira Nderitu Gachagua, wabunge kutoka eneo hilo walisisitiza kuwa Rais Kenyatta hatafaulu kuwashawishi wakazi wamuunge mkono kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Rais Kenyatta ameratibiwa kuzuru eneo hilo la Mlima Kenya kuanzia Jumatano wiki ijayo ambapo ataongoza mkutano wa viongozi katika Ikulu ndogo ya Sagana.

Katika mkutano huo, maarufu kama Sagana III, kiongozi wa taifa anatarajiwa kutumia jukwaa hilo kuwaelezea ni kwa nini wakazi wanafaa kumpigia kura Bw Odinga katika uchaguzi wa urais Agosti 9.

“Rais amelitelekeza eneo hili. Wakazi wamekasirika na hawatamsikiza; anapoteza wakati wake kuja hapa kumpigia debe Raila,” Bw Gachagua akasema jana katika mikutano wa Kenya Kwanza katika Kaunti ya Embu.

Bw Gachagua alikariri kuwa wakazi wa Mlima Kenya hawajamwona Rais Kenyatta kwa muda mrefu na atakabiliwa na wakati mgumu katika juhudi zake za kumnadi Bw Odinga kwao.

Msururu wa mikutano ya kampeni ya Kenya Kwanza katika vituo mbalimbali Kaunti ya Embu iliongozwa na Naibu Rais William Ruto pamoja na kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi na mwenzake wa Ford Kenya Moses Wetang’ula.

Akiongea katika vituo vya kibiashara vya Kigumo na Kirii katika maeneo bunge ya Runyenjes na Mbeere Kaskazini, Dkt Ruto aliapa kuhakikisha kuwa muungano wa Kenya Kenya utashinda Azimio la Umoja unaoongozwa na Bw Odinga.

“Kinyang’anyiro cha urais ni mbio za farasi wawili; Kenya Kwanza na Azimio la Umoja,” akawaambia wananchi katika kituo cha kibiashara cha Kigumo.

Dkt Ruto alimtaka Bw Odinga kuwa tayari kupambana naye na akome kuning’inia katika umaarufu wa Rais Kenyatta katika eneo la Mlima Kenya ili apate uungwaji mkono.

“Ikiwa Bw Odinga anaamini kuwa ana uwezo wa kukabiliana nasi, akome kushikilia koti la Rais,” akasema.

Dkt Ruto alisisitiza kuwa muungano kati yake na Mabw Mudavadi na Wetang’ula haulengi ugavi wa mamlaka bali kufufua uchumi kwa manufaa ya Wakenya wote.

Alisema kuwa muungano wa Kenya Kwanza ukiingia mamlakani utaongeza mgao wa fedha kwa Idara ya Mahakama na Huduma ya Kitaifa ya Polisi ili ziweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Kwa upande wake, Bw Wetang’ula alimtaka Rais Kenyatta kuiga mfano wa mtangulizi wake, Mwai Kibaki, ambaye alistaafu kwa heshima badala ya kujiharibia sifa kwa kujaribu kumsaidi Bw Odinga aingie Ikulu.

Naye Bw Mudavadi alisema serikali ya Kenya Kwanza itaupa kipaumbele mpango wa kufufua kilimo ambacho ni tegemeo kuu kwa wananchi wengi.

Kwa mara nyingine, Bw Mudavadi alimtaja Bw Odinga kama ‘mradi’ ambaye atafeli katika uchaguzi wa urais.

“Nawahikikishia kuwa kwa usaidizi wenu tutamshinda Raila kwa zaidi ya asilimia 70 ya kura ili asipate nafasi ya kuelekea kortini,” akasema.

  • Tags

You can share this post!

Kenya yatahadhari polio ikigunduliwa Malawi

Shirika laonya mvua haitaleta afueni ya haraka dhidi ya njaa

T L