• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Aliyeiba kipakatalishi kanisani atupwa jela miaka mitatu bila faini

Aliyeiba kipakatalishi kanisani atupwa jela miaka mitatu bila faini

NA JOSEPH NDUNDA

MWANAMUME mmoja aliyeiba kipakatalishi na vifaa vingine vyenye thamani ya Sh110,000 kanisani baada ya kuhudhuria misa katika kanisa hilo amefungwa kifungo cha miaka mitatu na nusu.

Hakimu mwandamizi wa korti ya Kibera, Esther Bhoke, alimhukumu Joseph Kamau Ndung’u baada ya kukubali kuwa alivamia afisi moja katika kanisa la Nairobi Chapel kando ya barabara ya Ngong na kuiba vifaa hivyo.

Joseph Kamau Ndung’u hakuruhusiwa kulipa faini.

Bi Bhoke alisema kuwa ripoti iliyowasilishwa mbele yake haikumruhusu Ndung’u kulipa faini bali kufungwa.

Vifaa alivyoiba vilikuwa vya Rodgers Koome Kinyua, ambaye ni fundi wa mitambo katika kanisa hilo.

Ndung’u pia aliiba Sh200 na mwavuli ambao Bw Kinyua alikuwa amehifadhi kwenye mkoba wake.

Mfungwa huyo baadaye aliviuza vifaa hivyo vyote kwa jumla ya Sh7000.

Bw Kinyua alikuwa ameacha vitu hivyo afisini mwake na kutoka kidogo, aliporudi, alipata havipo.

Picha za CCTV katika jumba hilo zilikaguliwa ambapo Ndung’u alinaswa akiondoka katika jumba hilo na begi.

Mahakama ilielezwa kwamba Ndung’u alionekana ndani ya kanisa hilo wakati wa ibada mnamo Mei 15 akiwa amevalia nguo zilezile alizokuwa amevaa alipoiba vitu hivyo.

Maafisa wa polisi waliitwa na kumkamata ndani ya kanisa.

  • Tags

You can share this post!

Viongozi wa Kenya Kwanza waahidi kuondoa mashine za kuvuna...

Kalonzo akosa njia, Azimio wamtarajia

T L